23.6 C
Dar es Salaam
Saturday, April 27, 2024

Contact us: [email protected]

Pereira Silima apandisha joto Uchaguzi Z’bar

MWANDISHI WETU-ZANZIBAR

HEKAHEKA za kupata mrithi wa Rais wa Zanzibar wa awamu ya nane, zimepamba moto baada ya kada mwingine wa chama hicho, Pereira Ame Silima kuchukua fomu ya kuwania nafasi hiyo.

Silima ambaye amewahi kushika nafasi mbalimbali katika Serikali ya Mapinduzi Zanzibar pamoja na ya Muungano, anaungana na makada wengine 28 wa chama hicho kuwania nafasi hiyo.

Mwanachama huyo ambaye amewahikushika nafasi mbalimbali ndani ya Serikali ya Mapinduzi Zanzibar ikiwamo Katibu Mkuu wa Wizara za Biashara Masoko na Utalii, Kilimo, Mifugo na Maliasili tangu Machi 2017 hadi sasa amekuwa Katibu wa Halmashauri Kuu ya CCM Taifa na Mjumbe wa Kamati Kuu ya CCM, Dodoma, Tanzania.

Akizungumza mara baada ya kukabidhiwa fomu ndani ya Ofisi Kuu ya CCM Kisiwandui Zanzibar,  Silima amesema kikubwa kilichomsukuma ni nia yake thabiti ya kukuza uchumi wa wananchi wa Zanzibar.

Amesema kuwa licha ya viongozi waliopo na waliotangulia kufanya kazi nzuri, ameona kuna changamoto katika ukusanyaji mapato ya ndani na kwamba kasi yake haiendani na uwezo wa kuzalisha.

“Nchi inahitaji maendeleo ya kiuchumi yatakayochagiza ukuaji kipato cha taifa na mwananchi mmojammoja, lakini sasa kipato cha wananchi ni kidogo na hivyo wengi kuangukia kwenye umaskini, kama nikipata ridhaa ya kuongoza nitahakikisha taifa linapiga hatua kimaendeleo,” amesema Silima.

Kuhusu kuongeza wigo wa ukusanyaji kodi, Silima ambaye pia ni mtaalam wa masuala ya Usimamizi wa Fedha na Biashara za Kimataifa amesema Zanzibar kwa sasa inategemea sekta za Utalii na Bahari kukuza mapato jambo ambalo linahitaji kufanyiwa maboresho.

“Uchumi wa Zanzibar unategemea sekta chache ikiwemo Utalii na uchumi wa bahari ambao haujawekezwa ipasavyo, hivyo kama chama nitachaguliwa kuwa Rais wa Zanzibar jukumu langu la kwanza litakuwa kuhakikisha kunakuwa na miundombinu ya kutosha ya kukuza uchumi,” amesema.

Akizungumzia umoja wa kitaifa amesema kwa sasa Zanzibar inahitaji jamii yenye umoja kuliko iliyopo sasa katika upatikanaji wa huduma muhimu kama elimu bora, afya na maji, yaani asiwepo wa kumwogopa mwenzake kwa sababu yoyote ile.

“Baadhi ya wanasiasa walitugawa Wanzanzibar kutokana tu na itikadi za kisiasa hadi kufikia watu kuogopana, katika zama zangu kila mtu atakuwa huru kufanya vile atakavyo katika misingi ya kisiasa au kidini ili mradi tu havunji katika ya nchi, amesema Silima.

Kwa upande wa ustawi wa jamii Ame Silima ambaye ni mtaalam katika Utayarishaji na Uchambuzi wa Sera mbalimbali amesema atatumia uzoefu wake kuhakikisha Zanzibar inakuwa na mkakati maalum wa kukomesha vitendo vya unyanyasaji wa watoto na wanawake.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles