23.6 C
Dar es Salaam
Saturday, April 27, 2024

Contact us: [email protected]

PASPOTI YA KAKOBE YAZUIWA UHAMIAJI

Na LEONARD MANG’OHA-DAR ES SALAAM


IDARA ya Uhamiaji Mkoa wa Dar es Salaam, inashikilia hati ya kusafiria ya Askofu Mkuu wa Kanisa la Full Gospel Bible Fellowship, Zachary Kakobe, kuchunguza uraia wake.

Hati ya kiongozi huyo wa kiroho ilishikiliwa jana alipokwenda kuitikia wito wa idara hiyo.

Askofu Kakobe aliwasili katika ofisi za idara hiyo saa 4:52 asubuhi akiongozana na wasaidizi wake wanne na alihojiwa kwa takribani saa tatu.

Akizungumza na waandishi wa habari baada ya mahojiano hayo, Askofu Kakobe alisema yeye ni raia halali wa Tanzania.

“Anayesema mimi si raia wa Tanzania aniambie ni raia wa nchi gani,” alisema

Alisema Uhamiaji wanaweza kuwa na nia njema, lakini alihoji kwanini kwa sasa wanahojiwa watu fulani kutoka Kigoma.

“Kwanini sasa, kwanini wanahojiwa watu wa aina fulani wa kutoka eneo fulani la Kigoma. Mbona hatujasikia kutoka Dodoma, Kaskazini wakihojiwa?

“Mimi ni Mtanzania na kama kuna mtu anasema si raia, basi aniambie mimi ni raia wa nchi gani,” alisema Askofu Kakobe.

Alisema katika mahojiano hayo, ametakiwa kuacha hati yake ya kusafiria ili iweze kuwasaidia kupata taarifa zake muhimu.

“Hiki wanachokifanya kinatia shaka. Biblia inasema muovu anakimbia hata kabla ya kufuatwa na mtu ila mwenye haki ni jasiri kama simba.

“Lakini wamesema ni kitu ambacho kitachukua siku moja au mbili kwa sababu wanataka kuangalia kwenye mafaili ili kupata taarifa za hizo (affidavit) zinazotakiwa,” alisema.

Kuhusu kuchunguzwa uraia wake Askofu Kakobe alisema si jambo la ajabu kutokana na sheria kuruhusu idara hiyo kumhoji mtu yeyote ila wasiwasi wake ni muda ambao suala hilo linafanyika.

“Wamekuwa rafiki katika mahojiano na ni kazi yao sawa, lakini wakati mwingine inaleta shaka kidogo ile ‘timing’ kwanini sasa, ile kwanini sasa ndiyo inaleta shida kidogo,” alisema.

Askofu Kakobe alisema maelezo aliyoyatoa ni ya wazi, hivyo anaamini kutakuwa na uwazi katika jambo hilo.

Alisema kabla ya jana kuhojiwa, maofisa wa idara hiyo wamekuwa wakienda nyumbani kwao Kijiji cha Mbizi, Wilaya ya Kakonko mkoani Kigoma kumfuatilia na yeye amekuwa akipata taarifa hizo kwa ndugu zake.

Askofu Kakobe alisema katika mahojiano hayo, walimuuliza kama ana vyeti vya kuzaliwa, akawambia kabla ya uhuru hapakuwa na vyeti hiyo na kwamba mwaka 1981 ndipo ilifanyika jaribio la kwanza la kutoa vyeti hivyo katika wilaya sita tu.

“Kwahiyo ni vitu vigeni kidogo nchini kwetu, kwa mfano mimi nimezaliwa mwaka 1955 enzi hizo ‘Birth Certificate’ hazikuwapo, achilia mbali kwa baba, mama. Hata ukizungumza kwa watu wanaofahamu waliokuwapo enzi hizo, hicho kitu hakikuwapo,” alisema Askofu Kakobe.

Alisema anashangazwa uraia wake kutiliwa shaka sasa hivi wakati mwaka 1974 alilitumikia Jeshi la Kujenga Taifa kupitia Operesheni Ukombozi.

Askofu Kakobe alisema kuhojiwa na vyombo mbalimbali si jambo baya ila halitakuwa jambo jema endapo itatumika kama fimbo.

“Ndiyo maana inaleta shida kwanini sasa, kwanini baada ya hiki na kile ndiyo mahojiano yatokee, kama inatumika kama fimbo sasa inapoteza maana.

“Kama ikiwa Uhamiaji, hata TRA tulikoanzia ni vitu vizuri, lakini ikiwa inatumika kama fimbo inapoteza ile maana yake.

“Ni kwanini mtu unawaza kama hivyo, ni pale ile ‘timing’ kama hivi naona umetaja Nondo, umetaja Niwemugizi utaona ‘line’ zote zinafanana, ningetarajia lingekuwa ni zoezi la watu wote sasa ili kucheki na kuthibitisha, ingeeleweka zaidi,” alisema.

Desemba 12, mwaka jana, Idara ya Uhamiaji ilimhoji Askofu wa Jimbo la Ngara – Rulenge, Severine Niwemugizi, kuhusu uhalali wa uraia wake baada ya Septemba mwaka huo kuibua hoja ya kutaka kupatikana kwa Katiba Mpya.

Wakati huo huo, Aprili 4, mwaka huu, idara hiyo ilimhoji mwanafunzi wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Abdul Nondo, kuhusu uraia wake, siku chache baada ya kudaiwa kutekwa na baadaye kupatikana mkoani Iringa.

 

KAULI YA UHAMIAJI

Akizungumzia suala hilo, Ofisa Uhamiaji Mkoa wa Dar es Salaam, Naibu Kamishna wa Uhamiaji, Crispin Ngonyani, alisema walimwita Askofu Kakobe kwa mahojiano baada ya wiki iliyopita kushindwa kuitikia wito wa idara hiyo.

“Tulimpelekea wito hakuitika na alisema ilikuwa wiki ya Pasaka, lakini jana mwenyewe aliandika kwenye mitandao kuwa ameitwa hivyo atakuja kutusikiliza,” alisema Ngonyani.

Alisema ofisi yake ina mamlaka ya kumwita mtu yeyote kumhoji na kwamba suala hilo halifanyiki kisiasa.

“Tunapopata taarifa za mtu yeyote kutoka vyanzo mbalimbali tunalazimika kumwita, lakini kuhusu mahojiano hayo yanahusu nini sitawaambia kwa sasa, mpaka tumalize mahojiano,” alisema.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles