31.2 C
Dar es Salaam
Tuesday, November 5, 2024

Contact us: [email protected]

Pamba yaongezeka asilimia 67 baada TADB kuwekeza

Na Mwandishi Wetu



UNAWEZA kusema bila kukosea kuwa wakulima wa zao la pamba ‘wameula’ kwa kupata msaada stahiki kwenye kilimo chao kuhusu pembejeo na viuadudu (viuatilifu) kutoka benki mahususi ya kilimo kitendo kilichomfurahisha Rais Dk. John Magufuli na kummwagia sifa Kaimu Mkurugenzi wake, Japhet Justine.

Benki hiyo imesimama kidedea katika ununuzi wa zao la korosho mwaka huu baada ya wafanyabiashara uchwara kugomea ununuzi korosho ili waipate kwa bei mchekea lakini Rais Magufuli amekataa njama hizo za kinyonyaji.

Wakati wa kuwaapisha mawaziri Ikulu katika mabadiliko ya Baraza la Mawaziri la hivi karibuni kutokana na sakata la korosho, Rais Magufuli, alimsifia Mkurugenzi wa TADB kuagiza mamlaka za uajiri ya benki hiyo ya umma kumthibitisha mara moja kwenye ukurugenzi wake kwani anasema anafanya vizuri kwa kuwapa mikopo wakulima wakati viongozi kabla yake walikuwa hawatoi mikopo hiyo na kujali  sana wafanyabiashara badala ya wakulima waliokusudiwa kuanzishwa kwa benki hiyo.

Kihistoria Benki ya Maendeleo ya Kilimo Tanzania (TADB), imetoa matrekta 50, yenye thamani ya zaidi ya Sh bilioni 2.7, kwa Vyama vya Ushirika 50 vya Msingi vya Masoko (AMCOS), vinavyolima pamba katika mikoa ya Kanda ya Ziwa, ili kuongeza tija na uzalishaji wa zao hilo.

Mikoa saba ya ziwa ya Simiyu, Shinyanga, Mwanza, Mara na Geita ndio wakulima wakuu wa zao la pamba kwa kuzalisha asilimia 90. Ukiungana na Singida, Tabora, Pwani, Kigoma na Katavi hufanya asilimia 99 ya zao hilo.

Akizungumza wakati wa makabidhiano hayo, wakati huo Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa TADB, Japhet Justine, alisema benki hiyo inalenga kuwawezesha wakulima wa zao la pamba ili waweze kuongeza tija na uzalishaji, kama inavyobainishwa katika Mpango wa Maendeleo ya Kilimo Awamu ya Pili (ASDP-11).

“Matrekta ni moja ya nyenzo itakayowawezesha wakulima kuongeza uzalishaji kwa kulima maeneo makubwa zaidi kwa kufuata kanuni bora za kilimo cha pamba, tofauti na kutumia jembe la mkono,” alisema Justine.

Alisema matrekta ni sehemu ya utekelezaji wa ASDP-11 katika kuhakikisha nyenzo bora za kilimo zinawafikia wakulima na kuchagiza uzalishaji zaidi wa malighafi zitakazotumika kwenye viwanda vilivyopo na vinavyokuja  vya kuongeza thamani ya mazao na kufanikisha azma ya Serikali ya kujenga uchumi wa kati na viwanda ifikapo mwaka 2025.

“TADB ndiyo benki yenye dhamana kubwa kwa mkulima, hivyo tutaendelea kuboresha mazingira katika sekta ya kilimo kwa kutoa mikopo kwa wakati pamoja na nyenzo za kilimo, lengo likiwa kumtoa mkulima katika kutumia jembe la mkono,” alisema Justine.

Alisema katika maeneo mengi nchini, bado wakulima wanatumia jembe la mkono linaloendelea kudumaza sekta hiyo kwa kufanya kilimo cha mazoea, hivyo benki imejipanga kuwa mkombozi wa mkulima na kufanya kilimo biashara kupitia huduma mbalimbali watakazozitoa.

“Tumeanza na wakulima wa pamba kwa kuwapatia matrekta kupitia vyama vyao na tutaendelea katika maeneo mengine ili kuhakikisha mazao yote ya kipaumbele yanatengenezewa mazingira bora ili uzalishaji wake uongezeke,” alisema.

Serikali imepanga mazao matano kuwa ya kimkakati yakiwamo pamba, kahawa, korosho, chai na tumbaku na hivyo yanahitaji usaidizi wa hali na mali.

Mkurugenzi wa Bodi ya Pamba, Marco Mtunga, aliisifia sana TADB na kusema kupitia mkopo wa viuadudu uliotolewa msimu uliopita na TADB, ambapo uliwanufaisha zaidi ya wakulima 600,000 wa zao la pamba, umewezesha kuongeza uzalishaji kufikia tani 221,600, ikiwa ni ongezeko la asilimia 67, ikilinganishwa na tani 133,000, zilizozalishwa msimu wa 2017/18.

“TADB mkombozi wetu wa kweli kwani imefanikisha upatikanaji wa pembejeo kwa wakati na kuongeza uzalishaji wa zao la pamba,” alisema Mtunga na kutoa wito kwa taasisi nyingine kushirikiana ili kuongeza tija na uzalishaji wa zao la pamba ambalo limeonesha kurudi kwa nguvu kubwa.

Alisema benki hiyo imerejesha matumaini makubwa kwa wakulima, hivyo ni muhimu wajiunge katika vyama vya ushirika, ambavyo vitarahisisha uratibu wa kuwapatia mikopo na zana za kilimo yakiwemo matrekta.

“TADB ina matumaini makubwa kuwa utoaji matrekta utaongeza hamasa kwa wakulima, hususan vijana kujikita katika sekta ya kilimo kwa kuwa Serikali imeshaonyesha nia thabiti ya kukuza sekta hii,” alisema.

Mmoja wa wakulima walionufaika na matrekta hayo aliishukuru Serikali kupitia benki ya maendeleo ya kilimo kwa kuwakopesha matrekta hayo, hali itakayoongeza uzalishaji.

Pamba au dhahabu nyeupe lilikuwa zao muhimu sana kwa uchumi wa Tanzania ambayo ilikuwa ni nchi ya nne wakati huo kwa uzalishaji katika Afrika.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles