23.4 C
Dar es Salaam
Saturday, April 27, 2024

Contact us: [email protected]

PAC yampongeza Waziri Kalemani kwa usimamizi mzuri wa miradi ya REA

Na Dorina Makaya, Manyara

Kamati ya kudumu ya Hesabu za Serikali (PAC) imempongeza Waziri Kalemani kwa kusimamia vema utekelezaji wa Miradi ya Wakala wa Nishati Vijijini (REA).

Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Hesabu za Serikali Mhe. Naghenjwa Livingstone Kaboyoke ametoa pongezi hizo kwa niaba ya kamati ya kudumu ya Hesabu za Serikali (PAC) tarehe 24 mwezi April 2021, mara baada ya kamati ya Kudumu ya Bunge ya Hesabu za Serikali kutembelea maeneo ya Miradi ya REA hususan kijiji cha Arri na Sigino vilivyoko mkoani Manyara ambapo pamoja na kuunganishwa umeme kwenye kaya, taasisi za elimu na afya pia zimeunganishiwa umeme.

Mwenyekiti huyo wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Hesabu za Serikali Mhe. Naghenjwa  Kaboyoke ameeleza kuwa, kamati yake imeridhishwa na Taarifa ya Utekelezaji ya REA iliyowasilishwa kwao na Waziri Kalemani baada ya kutembelea maeneo husika na kufanya mikutano na wananchi wa vijiji husika vikiwemo Arri na Sigino na kusikia kutoka kwa wananchi wenyewe namna Miradi ya REA ilivyotekelezwa katika vijiji hivyo.

Wajumbe wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Hesabu za Serikali wakimsikiliza Waziri wa Nishati Dkt. Medard Kalemani, wakati akiwasilisha Taarifa ya Wizara ya Nishati Kuhusu utekelezaji wa Miradi ya REA mkoani Manyara. (Waziri Kalemani hayumo pichani)

Pia, Kamati hiyo ya kudumu ya Bunge ya Hesabu za Serikali, imelisifia Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) kwa kutekeleza vema majukumu yake na kuwa mfano wa kuigwa katika nchi nyingine.

Awali akiwasilisha Taarifa ya Wizara ya Nishati kuhusu utekelezaji wa Miradi ya REA, Waziri Kalemani alieleza kuwa, kati ya shule 18 za Sekondari zilizomo katika wilaya ya Babati mjini tayari shule 14 za sekondari zimeunganishiwa umeme na ni shule 4 tu ambazo bado hazijaunganishiwa umeme.

Aidha, Waziri Kalemani ameeleza kuwa Kati ya shule za Msingi 56 zilizopo katika Wilaya ya Babati Mjini, tayari shule 24 zimeunganishiwa umeme, na shule 32 zilizobakia zitaunganishiwa umeme mara baada ya taratibu za ujenzi kukamilika.

Akizungumzia kwa Upande wa Wilaya ya Babati Vijijini, Dkt. Kalemani ameeleza kuwa, kati ya shule 35 za Sekondari zilizomo katika Wilaya ya Babati vijijini, Jumla ya shule za Sekondari 29 tayari zimeunganishiwa umeme na shule 06 zilizobakia zitaunganishiwa umeme. Aidha, amesema, kati ya shule 142 za msingi zilizopo katika Wilaya ya Babati Vijijini tayari shule 56 zimeunganishiwa umeme na zilizobakia pia zitaunganishiwa umeme.

Pia, Dkt. Kalemani ameileza kamati ya Kudumu ya Bunge ya Hesabu za Serikali kuwa, mbali ya kuunganishwa umeme kwenye kaya, taasisi za elimu na afya pia zimeunganishiwa umeme.

Akifafanua kuhusu upatikanaji wa fedha zinazotumika kuendesha Miradi ya REA, Dkt. Medard Kalemani ameeleza kuwa, hadi sasa kuna vyanzo vitatu vinavyochangia katika uendeshaji wa Miradi ya REA vikiwemo, Tozo ya asilimia 3 kwenye uzalishaji wa umeme wa biashara kwenye gridi ya Taifa, Tozo ya mafuta; ambapo kwa sasa ni shilingi 100 kwa lita kwenye mauzo ya mafuta ya Petroli na dizeli na shilingi 150 kwa lita ya mafuta ya taa pamoja na michango kutoka kwa wakala na taasisi za fedha za kimataifa na washirika wa maendeleo.

Akijibu swali  ni kwa nini mchango wa dizeli ni mdogo ikilinganishwa na mchango wa mafuta ya taa ambayo wananchi wenye kipato kidogo wanatumia, Waziri Kalemani ameweka wazi kuwa, kwa sasa mafuta ya taa hayatumiki kwa wingi ikilinganishwa na mafuta ya Dizeli kwa kuwa tayari Serikali imepeleka umeme vijijini,

Aidha, Waziri Kalemani amekumbushia kuwa, Miradi ya REA haina fidia kwa wananchi ambao maeneo yao yamepitiwa na miradi ya REA kwani Serikali imelenga kuwafikishia umeme wananchi kwa gharama nafuu sana ya shilingi elfu 27,000 tu na kuwa inatolewa kama huduma kwa wananchi na hakuna mteja yeyote anayetakiwa kulipia nguzo ili kuunganishiwa umeme.

Amesema, kwa wananchi wanaotumia umeme usiozidi unit 75 kwa mwezi wateja hao wanapaswa kulipia shilingi 100 kwa unit na kwa wateja wenye matumizi ya zaidi ya unit 75 wanapaswa kulipia shilingi 294 kwa unit moja.

Pia, Waziri Kalemani amempongeza Meneja wa TANESCO wa Mkoa wa Manyara Mha. Rehema Mashinji kwa utendaji mzuri na kumtaka kuendelea kuzimamia vema kazi ya kuwaunganishia umeme wateja waliolipia kuunganishiwa umeme kwa gharama ya shilingi 27,000 tu.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles