23.2 C
Dar es Salaam
Friday, May 10, 2024

Contact us: [email protected]

OLE NANGOLE ATAKIWA KUWASILISHA HOJA YA KUKATA RUFAA

Na JANETH MUSHI-ARUSHA


MAWAKILI wa aliyekuwa Mbunge wa Longido, Onesmo Ole Nangole (Chadema), wametakiwa kuwasilisha hoja zao za maombi ya kuomba kuongezewa muda wa kuwasilisha kusudio la kukata rufaa nje ya muda kwa njia ya maandishi Oktoba 3, mwaka huu.

Uamuzi huo ulitolewa na Jaji wa Mahakama Kuu Kanda ya Arusha, Dk. Modester Opiyo jana, wakati mahakama hiyo ilipotaja maombi hayo kwa ajili ya kupanga utaratibu wa kuyasikiliza.

Katika maombi hayo namba 108 ya mwaka huu, Ole Nangole aliwakilishwa na Wakili John Mallya, huku mjibu maombi wa kwanza ambaye alikuwa mgombea ubunge wa jimbo hilo kwa tiketi ya CCM, Dk. Steven Kiruswa, akiwakilishwa na Wakili Daudi Haraka.

Jaji Dk. Opiyo alikubaliana na mawakili hao kuwa maombi hayo yasikilizwe kwa njia ya maandishi, ambapo upande wa mleta mambi wanapaswa kuwasilisha hoja zao Oktoba 3, upande wa wajibu maombi Oktoba 10 na 16 mwaka huu, mawakili wa pande zote mbili watawasilisha hoja za nyongeza.

“Tukubaliane mfanye ‘submission’ kwa njia ya maandishi na isichukue muda mrefu tufanye kwa haraka na baada ya pande zote kuwasilisha hoja tukutane hapa mahakamani Oktoba 17 mwaka huu kwa ajili ya kupanga tarehe ya kutoa uamuzi, muwajulishe na wajibu maombi wa pili (upande wa Jamhuri),” alisema Dk. Opiyo.

Mawakili wa pande zote mbili walikubaliana na maamuzi hayo ya Jaji huyo ambapo maombi hayo yalipokelewa mahakamani hapo Septemba 18, mwaka huu.

Ole Nangole anaiomba mahakama hiyo kibali cha kuongezewa muda ili awasilishe upya rufaa yake Mahakama ya Rufaa nchini kupinga kuvuliwa ubunge.

“Tumeleta maombi ya kuomba kuongezewa muda ili tupeleke notisi ya kufungua rufaa nje ya muda Mahakama ya Rufaa. Uamuzi wa kumvua ubunge ulifanyika mwaka mmoja na nusu uliopita na tumeleta maombi haya licha ya Mahakama ya Rufaa kuzitupa rufaa mbili za Nangole, ila bado tuna nafasi ya kupeleka rufaa nyingine,” alisema Wakili Mallya.

Awali  Juni 29 mwaka jana, Mahakama Kuu Kanda ya Arusha ilimvua ubunge katika kesi ya uchaguzi namba 36 ya Mwaka 2015 iliyofunguliwa na Dk. Kiruswa, ambaye alikuwa akipinga matokeo yaliyompa ushindi Ole Nangole, ambaye katika uchaguzi huo alipata kura 20,076, huku Dk. Kiruswa akipata kura 19,352.

Hii ni mara ya pili Ole Nangole kuomba kuongezewa muda kwa ajili ya kukata rufaa nje ya muda ambapo Aprili 27, mwaka huu, mahakama hiyo ilimwongezea muda wa siku 14 wa kuwasilisha notisi ya kukata rufaa nje ya muda Mahakama ya Rufaa Tanzania.

Uamuzi huo ulitolewa na Kaimu Jaji Mfawidhi wa Mahakama hiyo, Sekela Moshi, katika maombi namba 18 ya mwaka huu ya Ole Nangole, aliyekuwa akiomba kuongezewa upya muda wa maombi ya rufaa baada ya ile ya mwanzo kuondolewa pamoja na rufaa.

Februari 23, mwaka huu, Mahakama ya Rufaa Tanzania iliondoa kwa gharama rufaa ya Ole Nangole, baada ya kushindwa  kuzingatia amri ya mahakama hiyo iliyowataka kufanyia marekebisho rufaa hiyo na badala yake kuandika rufaa upya.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
587,000SubscribersSubscribe

Latest Articles