Na WALTER MGULUCHUMA -SUMBAWANGA
MCHUNGAJI wa ng’ombe, Nyarobi Chaimaziwa (25), amenusurika kutumikia kifungo cha miaka mitatu jela baada ya kulipa faini ya Sh 300,000.
Nyarobi, ambaye alikuwa akichunga ng’ombe wapatao 387, mali ya baba yake, alitiwa hatiani na Mahakama ya Wilaya ya Sumbawanga, mkoani Rukwa kwa makosa mawili ya kuingiza wanyama hao kinyume cha sheria ndani ya Hifadhi ya Misitu ya Uwanda na kuchungia humo.
Aidha, mahakama hiyo ilitaifisha ng’ombe wote 387 waliokamatwa ndani ya Hifadhi hiyo katika Bonde la Ziwa Rukwa, wilayani Sumbawanga na kuwa mali ya Serikali.
Akitoa hukumu hiyo, Hakimu Rozalia Mugusa alisema kuwa, mshtakiwa alikimbia na kutelekeza ng’ombe zake siku ya tukio, lakini aliweza kukamatwa baada ya kurudi na kuwatambua wanyama hao wote wapatao 387.
“Nikizingatia kuwa mkosaji ni kosa lake la kwanza, lakini pia nimezingatia uzito wa kosa lenyewe, ili iwe fundisho kwa watu wenye mifugo mingi wanayoingiza hifadhini kinyume cha sheria, natoa adhabu kali kwa mkosaji ambapo kwa kosa la kwanza atalipa faini ya Sh 300,000 au kutumikia kifungo cha miaka miwili.
“Kosa la pili atalipa faini ya Sh 300,000 au kutumikia kifungo cha miaka mitatu na adhabu hii itakwenda pamoja,” alisema hakimu huyo.
Hakimu Mugisa akisoma hukumu yake, aliamuru ng’ombe wote 387 wataifishwe na kuwa mali ya Serikali, huku akisema kuwa haki ya kukata rufaa iko wazi.
Upande wa mashitaka uliita mahakamani hapo mashahidi wane, huku upande wa utetezi ukiita mashahidi watano, akiwamo baba mzazi wa mshtakiwa.
Awali Mwendesha Mashtaka, Wakili wa Serikali, Adolf Lema, alidai mahakamani hapo kuwa mshtakiwa alitenda makosa hayo Mei 11, mwaka huu, katika Hifadhi ya Misitu ya Uwanda, katika Bonde la Ziwa Rukwa wilayani Sumbawanga.