Na HUSSEIN JUMA,SHINYANGA
Â
SHUKRANI Â nyingi sana kwa serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, hasa uongozi wa Awamu ya Nne, kwa ujenzi wa chuo kikuu cha Dodoma; chuo kikubwa Afrika Mashariki na Kati. Chuo hiki kimetusaidia sisi wanyonge, watoto wa walalahoi kupata elimu ya juu, elimu ambayo kwa nchi yetu ni ghali sana na ni muhimu kwa maisha yetu.
Ni ukweli usiopingika kwamba, ujenzi wa chuo kikuu cha Dodoma umelisaidia kwa kiasi kikubwa sana Taifa hasa kwa kuwasaidia watoto wa maskini, wavuja jasho wa hali ya chini kabisa kufikia ndoto zao za kupata elimu ya juu.
Tunaposema chuo hiki ni kikubwa, tunamaanisha ni chuo kikubwa kweli kweli. Ni chuo chenye koleji takribani sita ndani yake na kinao uwezo wa kuchukua wanafunzi zaidi ya 35,000 kwa mwaka hivyo kufanya historia ya kubeba wanafunzi karibu wote wanaomaliza elimu ya sekondari ya juu (Advanced Secondary Education) mbali na ufaulu wao.
Binafsi nasoma Koleji ya Elimu (COED) ya chuo hiki. Jumla ya majengo yaliyopo kwenye koleji hii pekee ni 20 yenye uwezo wa kuchukua wanafunzi 500 kila moja; kwa hiyo koleji hii pekee inao uwezo wa kuchukua wanafunzi 10,000.
Pamoja na haya yote, chuo hiki bado hakijakamilika ujenzi wake kwa asilimia zote; kwa mujibu wa hotuba ya Mkuu wa Chuo Rais (mstaafu) Benjamini  Mkapa, chuo hiki kimekamilika kwa asilimia 40 tu na kinatarajiwa kukabidhiwa serikalini mwaka 2025. Kwa maana hiyo, baadhi ya miundombinu ya chuo hiki haijakamilika kikamilifu kama inavyotakiwa. Miundombinu kama barabara, njia za viunga vya chuo na hata baadhi ya sehemu za ndani za majengo haya.
Pamoja na upungufu huu wote, sina budi kuisifu Serikali kwa ujenzi wa chuo hiki kikubwa kabisa, kiukweli kimeleta matumaini mapya kwa watoto wa Kitanzania wanaotoka kwenye familia duni wakiwa na ndoto za kufikia elimu ya juu.
Hata hivyo, ningependa Serikali ijaribu kuangalia kwa jicho la pili na kuendelea kutusaidia Watanzania sisi maskini tulioko chuo hiki na baadhi ya mambo ambayo ningependa Serikali itusaidie ni haya hasa mwaka huu unaokuja wa masomo, yaani 2017/2018.
Kupandishwa gharama za malazi (Direct Cost)
Tangazo lililotolewa na uongozi wa chuo na kupachikwa kwenye website ya chuo la Septemba 9, 2017 limeonesha mabadiliko makubwa sana ya gharama za malazi. Kwa mujibu wa tangazo hilo, mwaka wa kwanza watakojiunga na chuo hiki wanatakiwa kulipa Sh. 295,000 kwa mwaka, tofauti na mwaka tulioanza sisi ambapo tulilipa Sh. 205,000, ongezeko la Sh. 90,000 nzima bila maelezo ya msingi.
Kwa wanafunzi wanaoendelea na masomo watatakiwa kulipa Sh. 263,500 badala ya Sh. 169,000 iliyokuwapo awali; ongezeko la Sh. 94,500 nzima pasi na maelezo ya msingi.
Septemba 20, 2017 kwa njia ya mitandao ya kijamii, mimi na wanafunzi wenzangu tulijaribu kuulizia sababu ya kupanda kwa gharama hiyo ghafla bila hata kushirikishwa. Tuliutaka uongozi wa Serikali ya Wanafunzi (UDOSO) kulifuatilia hili ili waje na majibu juu ya kwanini hasa gharama hizi zimepanda kiasi kile. Uongozi huo, kupitia rais wa Koleji ya Elimu, Yohana Ashery na Makamu wa Rais Monica Elias, uliahidi kulifuatilia na kutuhakikishia kuwa wangekuja na majibu kabla ya kesho yake, yaani Septemba 21, 2017.
Siku hiyo hiyo kabla hata ya siku tajwa, Makamu wa Rais aliandika ujumbe kujibu madai hayo na kusema kwamba, Chuo Kikuu cha Dodoma kimeamua kuongeza gharama hizo kutokana na;
- Gharama za maisha kupanda,
- Serikali kupunguza ruzuku ya chuo na
- Marekebisho na ukarabati wa miundombinu ya chuo unaoendelea.
Awali, kwa ajili ya malazi, kila mwanafunzi alilipa Sh 500 kwa siku. Kutokana na maelezo ya Makamu wa Rais ni kwamba, chuo kiliamua kupandisha kutoka Sh. 500 kwa siku hadi Sh. 950 kwa siku.
Akaongezea  wamejitahidi kuushawishi uongozi wa chuo na hatimaye kushusha gharama hizo kutoka ongezeko la Sh. 950 kwa siku hadi Sh. 750 kwa siku, hivyo kufanya upungufu wa gharama za malazi (direct cost) kutoka Sh. 263,500  hadi Sh. 228,500.
Kinachozidi kutupa wasiwasi ni kwamba, hiki ni Chuo cha Umma (Serikali), Je, inawezekanaje uongozi wa chuo peke yake kupandisha gharama za malazi ambazo kwa mujibu wa maelezo ya Makamu wa Rais wa Koleji ya Elimu zimejadiliwa toka mwaka jana na baadaye kushushwa ndani ya masaa mawili baada ya wanafunzi kulalamika?
Kama ni ukarabati wa miundombinu, tuliambiwa chuo hiki bado kinaendelea na ujenzi na wala hakijakamilika. Inakuwaje gharama za ukarabati huu atwishwe mwanafunzi? Kwa sheria ipi? Kwa utaratibu upi?
Serikali imepunguza ruzuku kwa chuo. Kwa akili yangu ya kawaida kabisa, Serikali hii ni ya kubana matumizi. Maana yake ni kwamba, Serikali ilipunguza matumizi bila shaka baada ya kujiridhisha pasi na shaka kwamba, chuo kinaingiza mapato makubwa lakini matumizi madogo kuliko mapato. Kama ndivyo, kwa nini chuo kisiilalamikie Serikali na badala yake kumtwisha mwanafunzi msalaba wa kupunguzwa kwa ruzuku ya chuo na Serikali?
Gharama za maisha kupanda. Kwa siku, Serikali kupitia Bodi ya Mikopo (HESLB) kwa wanufaika humpa kila mwanafunzi Sh. 8,500, kwa ajili ya kula. Kama ndivyo maisha kupanda, sasa kwa nini bodi haijaongeza fedha hiyo? Je, maisha yamepanda kwa chuo tu, ila kwa wanafunzi hayajapanda? Na hapa ni kwa mnufaika, vipi anayejiendeleza (in service), mshahara wake umepanda kwa kuwa maisha yamepanda?
Mimi kama mwanafunzi wa chuo hiki, ningependa sana Serikali ilione hili na ione namna ya kutusaidia.
Uongozi Serikali ya Wanafunzi (UDOSO), kuwa chini ya chama
Waziri Mkuu, Majaliwa Kassim Majaliwa, akiwa mjini Dodoma mwaka jana aliwahi kutuasa wanafunzi tuachane kabisa na siasa, tusome. Mimi nadhani ulikuwa ni ushauri mzuri kabisa.
Badala yake, kwa sasa, ili uwe Rais wa aidha shirikisho ama koleji kwa Chuo Kikuu cha Dodoma, ni lazima uwe na kadi ya chama fulani (nasema kwa kujiamini kwa kuwa ninao ushahidi huo) ambao ni sahihi.
Suala hili la kadi limekuwa likitunyima fursa ya kuchagua viongozi tunaowaamini na wenye uwezo kwa kukosa tu sifa ya kuwa kada wa chama. Sasa, pamoja na mengine, ningependa sana Serikalj yangu sikivu kupitia kwa Mkuu wa Chuo ijaribu kuliangalia upya suala hili. Sitaki kuamini kwamba Serikali inayajua mambo haya, yawezekana hawayajui kabisa, ila ukweli ndiyo huu.
Nimalize kwa kusema kuwa, Serikali yetu naamini ni sikivu na masuala haya yanatekelezeka, hivyo kwa moyo wote naamini kabisa kuwa, Serikali itatusaidia watoto wa Kitanzania; wanyonge ili tuendelee kupata elimu hii muhimu katika maisha yetu kwa amani.
Natanguliza shukrani!
+255 759 947 397