‘‘SERIKALI yoyote ambayo ina kiu ya kuleta mabadiliko na maendeleo, inatakiwa kutambua manufaa ya ukosoaji chanya” Haya maneno yaliwahi kusemwa na Hamad bin Isa Al Khalifa wa Qatar.
Ni dhahiri tangu Mheshimiwa John Pombe Magufuli atawazwe kuwa Rais, wananchi wengi hasusani wanyonge wanaonekana kuwa na matumaini makubwa katika mustakabali wa maisha yao licha ya kuwapo changamoto za hapa na pale.
Katika kuzunguka kwangu mijini na vijijini ili kupata mawili, matatu kutoka kwa wananchi kuhusu tathmini ya uongozi wa Rais Magufuli, nimefanikiwa kuyanasa yafuatayo:.
“Magufuli ni jembe maana tangu awe Rais, amethubutu kuwawajibisha viongozi wengi bila kuangalia sura zao’’
“Aaa! Hiyo si kweli kwamba Magufuli anapowajibisha haangalii sura ya mtu, bali na yeye anao watu wake anaowapendelea kiasi kwamba hata wakikosea mkalalamika hawezi kutengua nyadhifa zao’’
“Siku hizi ukienda ofisini kupata huduma, nidhamu ipo juu kwa watumishi wa umma ukilinganisha na uongozi uliopita maana wanaogopa kutumbuliwa’’
“Japo maisha ni magumu lakini Magufuli amerudisha kuheshimiana kwani sasa ni ngoma droo kati ya matajiri na maskini maana wote tunalia’’
‘‘Huyu jamaa aliwahi kusema watu wanadharau pesa kwa kuita shilingi mia tano Jero hivyo ni lazima pesa iheshimiwe na ni kweli sasa hivi baada ya yeye kuingia madarakani kuna nidhamu ya pesa maana lugha za Jero na Buku zimepungua mitaani’’
“Mimi namkubali Magufuli kuwa ni kiboko ya mafisadi tatizo lake anaoogopa kukosolewa’’
“Rais Magufuli angeweza kuboresha demokrasia, watu wakawa huru kutoa maoni yao bila hofu nakwambia angekuwa kiongozi bora kuliko hata Nyerere na Mandela.’’
‘‘Viongozi wengine waliitafuna nchi mpaka wakawa wanaenda Ughaibuni kustarehe lakini Magufuli tangu aingie madarakani hata Ulaya hajaenda.’’
‘‘Kwangu binafsi siwezi kumfagilia Rais Magufuli kwani kama anajiamini mbona anawabana wapinzani wake waliosaidia kuufichua ufisadi wa Serikali katika miaka iliyopita?’’
Hayo yakiwa ni baadhi ya mawazo ya wananchi kuhusu utendaji wa Rais Magufuli bado kuna mijadala kwamba kiongozi huyu anaogopwa sana na wasaidizi wake linapokuja suala la kukosolewa.
Kama si uzushi kwamba Rais Magufuli anaogopwa sana katika kukosolewa, basi huenda zipo sababu kadhaa zinazoweza kusababisha hali hii kulingana na mazingira yaliyopo.
Rais Magufuli kuonekana anapendwa na kukubalika kwa wananchi inaweza ikawa sababu ya wasaidizi wake kumchukulia kama malaika asiye na doa wala kunyanzi.
Tumbua tumbua ya kiongozi huyu ambayo haiangalii sura ya nyani inaweza kuwa chanzo cha wasaidizi wake kujipendekeza kwake ili wasije kutemeshwa tonge mdomoni hata kama kuna udhaifu wanauona kwake.
Kitendo cha Rais Magufuli kuonyesha nia ya kuwashughulikia mafisadi bila kujali walihudumu katika awamu ipi, inaweza kusababisha kuibuka kwa wanasiasa fulani kuweka ‘defence mechanism’ kwa kujidai wamenogewa na uongozi wake hivyo Katiba ibadilishwe ili muhula wa Urais uongezwe badala ya kuonyesha upungufu.
Inasemekana Rais Magufuli anapenda sana wanaomsifia kuliko wanaomkosoa na ndiyo maana hata siku ya kumwapisha Jaji mkuu Prof. Ibrahim Juma, aliwalaumu viongozi wastaafu wenye kidomodomo, hali ambayo inaweza kuchochea wasaidizi wake wawe ni wa “Ndiyo Mzee.
Yote katika yote Rais Magufuli tambua kuwa wanadamu huwa ni vigeugeu maana wanaokusifia bila kukukosoa, siku moja mambo yakiharibika wanaweza kukusaliti kama Yuda Iskariote huku ukitamani ni heri ungewakumbatia wakosoaji wako, kwani ukosoaji humfanya mtu aimarike kama alivyowahi kujisemea Le Bron James raia wa Marekani.