26.2 C
Dar es Salaam
Sunday, August 14, 2022

Nyuma ya pazia tambo za Trump, ‘kifo’ cha ISIS

HASSAN DAUDI NA MITANDAO

HAKUNA ubishi kuwa chimbuko la kundi la Dola ya Kiislamu nchini Syria (ISIS) ni uvamizi wa Marekani nchini Iraq mwaka 2003. Likitokana na lililokuwa kundi tishio kwa nchi za Magharibi kipindi hicho, Al-Qaeda, ISIS ni matokeo ya hasira dhidi ya walichokifanya Wamarekani kipindi hicho.

Mwaka 2011, ISIS, ambalo kipindi hicho lilikuwa likifahamika kwa jina la Dola ya Kiislamu ya Iraq (ISI), lilianza kupanua mbawa zake kwa kujipenyeza katika vurugu za Syria, likiwaunga mkono waliokuwa wakimpinga Rais Bashar al-Assad.

Kuanzia hapo, ISIS halijawahi kuipumzisha Syria, ambapo mauaji, vitendo vya udhalilishaji dhidi ya wanawake na uharibifu wa mali unaofanywa na kundi hilo umeendelea kuwa sehemu ya maisha ya wananchi wa taifa hilo.

Kufikia mwaka 2014, kundi hilo linaloamini dhehebu la Sunni ndilo sahihi katika Dini ya Uislamu na si Shia lilishajimilikisha asilimia 95 ya ardhi ya Syria.

Haijasahaulika kuwa miezi miwili iliyopita, mlipuko wa bomu uliua raia wanne wa Marekani na wengine kumi wa Syria mjini Manbij na baadaye ISIS walitangaza kupitia mitandao ya kijamii kuwa wao ndiyo waliohusika.

Hata hivyo, taarifa ya hivi karibuni iliyotolewa na Rais wa Marekani, Donald Trump, ilionekana kuibua matumaini mapya juu ya vita dhidi ya ubabe wa kundi hilo.

Ilikuwa ni Alhamisi ya wiki iliyopita, ambapo Rais Trump aliutangazia ulimwengu kuwa wamefanikiwa kwa kiasi kikubwa katika mapambano yao dhidi ya ISIS.

Wafuatiliaji wa siasa za Mashariki ya Kati watakumbuka kuwa hii si mara ya kwanza kwa Rais huyo kujitangazia ushindi dhidi ya wanamgambo wa ISIS kwani aliwahi kufanya hivyo mwishoni mwa mwaka jana.

“Tumeshinda (vita dhidi ya ISIS),” ulikuwa ni ujumbe aliouposti Desemba 19, mwaka jana, katika ukurasa wake wa mtandao wa kijamii wa Twitter.

Safari hii, kwa mujibu wa kiongozi huyo, ISIS wameshapoteza asilimia 100 ya maeneo waliyokuwa wakiyashikilia, akiongeza kuwa wanamgambo zaidi ya 10,000 wa kundi hilo wameshakimbia na wengine wanashikiliwa.

Lakini Je, Rais Trump na washirika wake wanaamini kuyakomboa maeneo yaliyokuwa chini ya kundi hilo, kuwaua au kuwakimbiza wanamgambo wake ndiyo kumaliza tatizo? Kama watakuwa na imani hiyo, basi huenda watakuwa wamejipumbaza.

Tatizo kubwa, ambalo huenda lisionekane kirahisi ni kwamba tayari sehemu kubwa ya wananchi wa taifa hilo wameshatekwa na itikadi ya Dola ya Kiislamu. 

Ni kweli hakuna ambaye alikuwa akifurahishwa na vurugu zilizokuwa zikifanywa na ISIS lakini bado walichokuwa wakikipigania kimeonekana kukubalika zaidi.

Mfano wa hilo, katika mahojiano yake na kituo cha televisheni cha CNN, bibiye Um Bassam (25), ambaye ni mkazi wa mjini Aleppo anasema bado wanatamani kuishi maisha yaliyokuwa yakishinikizwa na ISIS.

Hivi sasa, Um na wanawake wenzake, pamoja na watoto wao, wanaishi kambini baada ya kuokolewa katika kundi hilo lakini bado wameendelea na msimamo wao wa kuitambua ISIS.

“Tulitaka kuishi kwa amani lakini tukiwa ndani ya mavazi ya Kiislamu, si kutoka nje na kukutana na wanaume. Tunataka kuendana na sheria za Mungu,” alisema mama huyo na kuungwa mkono na wanawake wenzake, ambao pia walikuwa wamezifunika nyuso zao kwa ‘niqab’.

Kiongozi wa wataalamu wa afya waliojitolea kuwahudumia kambini, David Eubanks, anasema kumekuwapo na changamoto ya wanawake hao kutotaka kutibiwa, wakisema ni kinyume cha mafundisho ya Dini ya Kiislamu miili yao kushikwa ovyo.

“Mfano, madaktari wa kujitolea kutoka Jamii ya Wakristo ya Free Burma Rangers wamepata tabu kumshawishi mwanamke raia wa Morocco. Hawataki kuguswa. Anasema mumewe hatakubali mwili wake kuguswa na mtu mwingine,” anasema Eubanks na kusisitiza kuwa wamekuwa wakiwaona wahudumu kama ‘makafiri’

Mumewe aliuawa miaka miwili iliyopita wakati lilipofanywa shambulio la anga dhidi ya ISIS mjini Raqqa. Je, anazungumziaje mpasuko uliopo kati ya waumini wa madhehebu ya Sunni (wanaoungwa mkono na ISIS) na Shia?

“Tunachokijua ni kitabu na sheria za Mungu, ambazo zinasema yeyote anayewapiga au kuwaua Sunni, au anayeshindwa kuishi kwa misingi ya sheria za Mungu, anatakiwa kuuliwa tu…”

Um anasema hata kama ISIS haitakuwapo tena, ataendelea na itikadi yao, akiamini ilikuwa ikimpendeza Mungu. “Ni kweli, yapo waliyokuwa wakizidisha, lakini bado walikuwa ndani ya Uislamu na hicho ndicho tulichokitaka,” alisema.

Alipoulizwa kwanini watu wengi wamekuwa wakikerwa na kutaka Kundi la ISIS litokomezwe,Um anasema: “Wengi wao ni wakulima. Wanawake wao hawafuniki nyuso zao. ISIS ilipokuja, ilikuwa ikiwalazimisha wanawake kujisitiri, hivyo wakakerwa na hilo,”

Aidha, aliulizwa pia juu ya video ambazo ISIS wamekuwa wakizitupia mitandaoni, zikionesha matukio yao ya kinyama dhidi ya wale wasiotaka kukubaliana nao.

“Ndiyo, walikuwa wanatisha na kushitusha lakini hiyo ndiyo amri ya Mungu… Yeyote anayekataa kufuata sheria za Mungu, anatakiwa kufanyiwa hivyo. Wanapaswa kuuliwa. Ndivyo anavyotaka Mungu na hatuwezi kulibadili hilo,” anasisitiza Um.

Ukiacha Um, itikadi ya ISIS imeonekana kuwa na nguvu pia kwa vijana, hasa wa kiume, ambao baadhi yao wametamka wazi kuwa Syria ilipaswa kuwa chini ya utawala wa kundi hilo ili kufuata misingi ya dini ya Kiislamu.

Huyu hapa ni Mahmoud, kijana mwenye umri wa miaka 15, ambaye pia anatokea mjini Aleppo. Katika mahojiano yake na CNN, aliulizwa endapo anaona itikadi ya ISIS ikiendelea baada ya ‘kufa’ kwa kundi hilo.

“Kwani hujasoma Qur’an? Hujui aya ya Qur’an inayosema Dola ya Kiislamu itapitia nyakati ngumu na ndipo Mungu atakapoiletea ushindi? alihoji Mahmoud, akiongeza kuwa haamini kuwa utawala wa ISIS utatokomezwa moja kwa moja.

Kauli yake hiyo iliungwa mkono na mwanamke aliyekuwa karibu yake, ambaye kama ilivyokuwa kwa Um, alikuwa amevalia hijab. “Mungu anatupima. Wasio na imani wataondoka, watu sahihi watabaki,” alisema.

Ni kwa mantiki hiyo basi, wachambuzi wa siasa wanaweza kuibua madai kuwa huenda juhudi za kutokomeza ISIS zikawa za muda kwani bado itikadi ya kundi hilo imebaki vichwani mwa wananchi wa Syria.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
198,663FollowersFollow
550,000SubscribersSubscribe

Latest Articles