31.2 C
Dar es Salaam
Friday, March 29, 2024

Contact us: [email protected]

Ni mwisho wa zama za Zia na BNP yake nchini Bangladesh?

JOSEPH HIZA NA MTANDAO

UNAPOSAFIRI hadi kusini kabisa mwa Bara la Asia, utakuwa unaingia katika taifa lenye Waislamu wengi;  Bangladesh, ambako utakutana na wanawake wawili wa shoka, ingawa mmoja nguvu zake zinaelekea kupungua kutokana na kibano cha jela.

Siasa za taifa hilo lenye watu milioni 160 tangu lipate uhuru, kutoka ubavuni mwa Pakistan ile miaka ya 1970 zimetawaliwa na familia mbili achilia mbali kipindi fulani zilipozimwa na utawala wa kijeshi.

Si hivyo tu bali pia familia hizo zina uwezekano mkubwa wa kuendelea kuongoza nchi hiyo kwa miaka mingi ijayo kwa kizazi cha tatu baada ya hiki cha pili kilicho kusudio la makala haya.

Kizazi cha sasa ni cha viongozi wanawake waliotawala siasa za Bangladeshi na kuipelekesha nchi vibaya, kushuhudia matukio ya kulipizana kisasi, migomo, maandamano, machafuko, mauaji na vitendo vya rushwa.

Ni aina ya mwelekeo, ambao ni tofauti na ule waliokuwa wakiuhubiri wanawake hao katika miaka ya 1980 wakati wakipigania kurudishwa kwa utawala wa kidemokrasia na ondoko la ule wa kijeshi, ambao uliondoa nguzo muhimu za waasisi wa taifa.

Viongozi hawa ni Sheikh Hasina (72), binti wa baba mwasisi wa taifa hilo Bangabandhu Sheikh Mujibur Rahman na Khaleda Ziab (74), mke wa shujaa aliyetukuka wa ukombozi wa taifa hilo, Shaheed Ziaur Rahman.

Wanawake hao wameliongoza taifa hilo kwa zamu kipindi cha miongo miwili iliyopita, lakini badala ya kuijenga nchi na kuendeleza ndoto zilizokatishwa za waasisi wa taifa hilo, wawili hao wamekuwa wakichakaza kwa maslahi yao licha ya vipindi fulani kufanikiwa kukuza uchumi wa taifa hilo.

Ni vigumu kutofautisha dhamira na malengo ya wanawake hao; kwa maneno mengine unaweza kusema Sheikh Hasina na Khaleda Zia ni taswira mbili tofauti katika sarafu ile ile.

Kwa wanaowaangalia kwa jicho baya wanasema Sheikh Hasina, ambaye ndiye waziri mkuu aliyetawala muda mrefu zaidi katika historia ya Bangladesh, anaamini Taifa hilo ikiwamo watu wake ni mali ya baba yake na kwa upande mwingine Khaleda Zia pia anaamini Bangladesh ni mali ya mume wake.

Kwa mtazamo na imani hiyo iliyojikita katika nyoyo zao na kujenga mwelekeo wa tamaa ya madaraka n a heshima umepelekea washindane kuitawala nchi hata kwa kumwaga damu ili familia zao zitawale milele kwa vile wanaamini ni haki na stahili yao.

Hata hivyo, ili kutawala wote wanahitaji mamlaka na fedha. Mbali ya kupata madaraka na fedha wanahitaji kushinda chaguzi; hivyo, ili kushinda chaguzi kwa makusudi hutumia ndimi zao laghai na kutoa matumaini au ahadi za uongo hasa nyakati za uchaguzi.

Huwalaghai Wabangladesh, ambao kwa bahati mbaya wanaonekana kukosa chaguo lingine mbadala zaidi ya kuwachagua baina ya wanawake hao wawili.

Katika hali ya kustaajabisha pale wote wawili wanapokosekana madarakani kama ilivyowahi kutokea wakati jeshi lilipoingilia kati kuwazuia wasigombee, maisha huwa kana kwamba hayaendi kwao na kwa wafuasi wao na hivyo kila aina ya mbinu hufanyika kuwarudisha katika siasa hata kama wananuka ufisadi na mwelekeo wa kuivuruga nchi.

Kwa sababu ya njaa na tamaa zao za madaraka na fedha, wamekuwa wakicheza na maisha ya mamilioni ya watu wa Bangladesh.

Hali kadhalika nchi hii inatawaliwa na vyama vyao viwili tu vyenye nguvu kati ya lundo la vyama vya siasa lililopo nchini humo, utitiri ambao ni ushirika wa vyama hivyo vinavyonuka sana rushwa.

Inadaiwa na wakosoaji wa wawili hao utitiri huo upo kwa ajili ya ‘biashara ya kisiasa’ ya kutengeneza fedha iwe kutoka kwa wafanyabiashara au kuiba fedha za umma.

Aidha wakosoaji hao wanaenda mbali kuwa hakuna chama cha siasa au mwanasiasa baina yao anayewajali kutoka moyoni watu na nchi zaidi ya kujali madaraka na fedha na matokeo yake ni watu wa kawaida wanaoumia.

Visasi, machafuko na mauaji ya kisiasa yamekuwa sehemu ya taifa hilo kwa vile kila mmoja wa wanawake hao anapokalia madaraka wawili hao hufanyiziana.

Mmoja anapokuwa nje ya madaraka hutumia nguvu na ushawishi wake kuitisha migomo, maandamano na kila aina ya harakati kuhakikisha nchi haitawaliki huku aliye madarakani akitumia ‘kushikilia kwake mpini dhidi ya makali ya upanga’ kumkandamiza mwenzake au wafuasi wake huku vitendo vya utekaji nyara vikishamiri.

Sheikh Hasina mapema 2014 alitetea kiti cha uwaziri mkuu kupitia uchaguzi uliojaa vurugu na machafuko ya umwagaji damu, wingi wa utata na uliolaaniwa vikali ndani na nje ya nchi.

Idadi ya wapiga kura waliojitokeza katika vituo vya kupiga kura wakati wa uchaguzi huo ilikuwa aibu na zaidi ya nusu ya viti vya ubunge havikushindaniwa katika uchaguzi uliofanyika Jumapili ya Januari 5.

Wakati wa kuelekea siku ya uchaguzi huo uliosusiwa na Zia na washirika wake, vituo 200 vya kupiga kura vilipigwa mabomu na watu zaidi ya 100 walikufa katika mapigano yanayohusiana na kampeni za uchaguzi huku wengine 20 wakiuawa siku ya uchaguzi.

Awali sehemu kubwa ya mwaka 2013, chama cha upinzani cha Bangladesh Nationalist (BNP) na ushirika wake wa vyama 18 ukiongozwa na Zia, Waziri Mkuu wa zamani wa mara tatu na kiongozi wa chama hicho, uliitisha siku zaidi ya 85 za migomo na maandamano na kulifanya taifa zima kusimama.

Upinzani ulidai kuwa chama tawala cha Awami League kinachoongozwa na Waziri Mkuu aliyekuwa akitetea kiti hicho Sheikh Hasina kirekebishe Katiba, kivunje Bunge baada ya kutimiza miaka mitano Januari 24, 2014 na kisha kikabidhi kwa serikali ya mpito ambayo itaongozwa na wataalamu kwa siku 90.

Kazi ya Serikali ya Mpito ya Bangladesh ingekuwa kushirikiana na Tume ya Uchaguzi ya Bangladesh kusaidia kuendesha, kupanga na kusimamia Uchaguzi Mkuu wa Januari 5 na kukabidhi madaraka kwa serikali mpya iliyochaguliwa.

Akihofia wizi wa kura katika uchaguzi mkuu, Zia alitaka kutekelezwa kwa masuala hayo hasa la kuundwa kwa serikali hiyo ya mpito isiyoegemea upande wowote kusimamia chaguzi hizo.

Wakati Hasina kwa kutumia madaraka yake alipokataa, Zia kama ilivyotarajiwa akaanzisha maandamano na migomo mikubwa kususia uchaguzi kitu ambacho kiligharimu mali na maisha ya wengi.

Desemba 3, 2013, chama cha Jatiya kilichoongozwa na Rais wa zamani Hussain Mohammad Ershad, pia kilitangaza nia ya kususia uchaguzi huo.

Wawakilishi wa Umoja wa Ulaya (EU) walionana na kiongozi wa BNP, Khaleda Zia na kumwomba kutosusia uchaguzi huo wakijua madhara ambayo yangetokea iwapo msuso ungetekelezwa pamoja na kumtaka asitishe migomo na mikwamo iliyokwamisha nchi badala yake ajikite zaidi katika meza ya majadiliano na serikali.

Juhudi  kumshawishi ziliposhindikana Zia akajikuta akiwekwa katika kizuizi cha nyumbani huku Ershad akitishia kujiua baada ya majeshi kuzingira nyumba yake pia.

Makamu Rais wa BNP,  Shamsher Chowdhury alisema mwitikio mdogo wa wapiga kura wa asilimia 20 unaashiria kuwa watu wanataka chaguzi mpya na hivyo umuhimu wa kutoutambua uchaguzi huo.

Lakini pia Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa (UN), Ban Ki-moon wakati huo alikosoa vyama vyote vya BNP na Awami League akisema vilikuwa na uwezo wa kutumia busara kumaliza mivutano yao kwa amani iwapo maslahi ya nchi yangewekwa mbele.

Alizitaka pande zote mbili kuanzisha mijadala ya maana kushughulikia matarajio ya watu wa Bangladesh kwa ajili ya mchakato jumuishi wa kisiasa.

Uchaguzi huo wa 2014 ni kielelezo cha chaguzi nyingi zilizofanyika nyuma zikihusisha wanawake hao na vyama vyao ambazo pia hushuhudia vitendo vya utekaji nyara hata mauaji ya wafuasi wao muhimu wakiwamo wagombea ubunge kwa lengo la kupunguzana nguvu.

Iwapo utaangalia wa kumtupia lawama kwa mlolongo huo wa machafuko, vifo na uharibifu ambao umechokwa na jumuiya ya kimataifa, unaweza kuanza kutazama historia ndefu na mnyang’anyano katili wa madaraka baina ya wanawake hao wawili katika harakati zao za kuitaka heshima ya kukalia kiti cha enzi.

Wachambuzi wengi wa mambo wanakubaliana kuwa inawezekana kabisa kuzuia upotevu wa maisha na hasara ya uharibifu wa mali na miundombinu nchini humo iwapo wababe hao wangeweka pembeni ubinafsi, hasira na maslahi yao binafsi ili kufikia makubaliano ya jambo fulani.

Kwa kipindi cha miaka  35 iliyopita, Sheikh Hasina , amekiongoza chama cha Awami League, ambacho kilishinda uchaguzi huo wa Januari 5.

Binti huyo wa Sheikh Mujibur Rehman, baba mwasisi wa Bangladesh, amekuwa waziri mkuu wa taifa hilo tangu mwaka 2009 na aliwahi kuishika kazi hiyo kuanzia mwaka 1996 hadi 2001.

Baba yake sambamba na sehemu kubwa ya familia yake walinyongwa na maofisa wa jeshi mwaka 1975 huku mumewe akifariki dunia baada ya kuugua muda mrefu, miezi minne tangu aingie madarakani kwa muhula wa pili.

Kwa upande mwingine hasimu wake mkubwa, Begum Khaleda Zia, mke wa kiongozi wa kijeshi Ziaur Rahman, ambaye aliunda BNP mwaka 1978 na alikuwa Rais wa nchi kabla ya kuuawa katika Mapinduzi ya kijeshi mwaka 1981.

Zia alikuwa waziri mkuu kuanzia mwaka 1991 hadi mwaka 1996 na kuanzia mwaka 2001 hadi mwaka  2006.

Wakiwa wametokea kwenye majanga yanayofanana, wote wawili wakaingia kwenye siasa kwa hasira za kuuawa kwa wapendwa wao na wakati huo huo wakitaka kuionesha jamii namna ya kuijenga nchi kidemokrasia

Lakini tangu 2006 Zia aliposhika wadhifa wa uwaziri mkuu ni kama ameporomoka na kumwachia mwenzake kuendelea kutamba mara ya tatu mfululizo na ni ama ameshindwa vita hii baina yao.

Uchaguzi wa Desemba  31 mwaka jana, ulimpa Sheikh Hasina uwaziri mkuu wa muhula wa tatu mfululizo kwa ushindi wa kishindo katika uchaguzi wa taifa wa Bangladesh na kuzua wasiwasi taifa hilo linageuka kuwa nchi ya chama kimoja.

Chama cha Sheikh Hasina, Awami League (AL), na washirika wake walishinda karibu viti vyote 300 vya ubunge ukiwa ushindi bora kabisa katika historia ya chama hicho.

Ushirika mkuu wa upinzani ukiongozwa na Bangladesh Nationalist Party (BNP), kwa upande wake ulijipatia viti vya aibu; saba tu.

Matukio hayo ya kushtusha na kukatisha tamaa ya BNP katika uchaguzi huo yalisababisha wachambuzi wengi wa Bangladesh kuhoji iwapo chama hicho tawala cha zamani ambacho kilishinda chaguzi nne za taifa na mbili za urais tangu kuundwa kwake mwaka 1978 na ambacho hakijawa madarakani tangu mwaka 2006 kitaweza kwa mara nyingine kurudia katika nafasi yake ya kisiasa katika taifa hilo.

Mwenyekiti wa chama hicho Khaleda Zia yupo jela kwa mashtaka ya rushwa na mwanae ambaye ni Kaimu Mwenyekiti Tarique Rahman amekuwa akiishi uhamishoni mjini London kwa miaka zaidi ya 10.

Oktoba 2018, Mahakama ya Bangladeshi ilitoa adhabu ya kifungo cha maisha jela dhidi ya Tarique kwa jaribio la mauaji la mwaka 2004 dhidi ya Sheikh Hasina, ambalo liliua watu 24 na kujeruhi wengine wengi.

Wengi wa viongozi wengine wa chama hicho na wafuasi mashuhuri wako jela ama wamejificha au wako ugenini na wengine waliobakia wanaishi maisha ya kutojionesha.

Chama hicho kimekuwa kikikana kufanya kosa lolote na kusema kwamba mashtaka yana harufu ya kisiasa.

Hata hivyo, BNP imepoteza wafuasi wengi kutokana na matokeo ya tuhuma hizo mbaya.

Migomo na maandamano ya mitaani ya mwaka 2013, kususia uchaguzi Januari 2014 kwa madai ya kutaka haki ni kaburi lingine.

Serikali ya Sheikh Hasina alipuuza hayo na kwenda kushinda chaguzi kirahisi bila upinzani.

Kwa sababu ya hilo,  BNP iliendelea na maandamano, migomo ambayo mabasi yalichomwa moto, mabomu yalirushwa, na mifumo ya maisha ilivurugwa. Hilo lilisababisha umma kukigeukia chama hicho cha upinzani.

Mwaka 2018, BNP ililazimika kukubali kushiriki kwa amani lakini kilishindwa kurudisha umaarufu wake.

Wakati sehemu kubwa ya viongozi na wanaharakati wake wakijificha au wako jela, chama hicho hakikuweza kuonekana kabisa, yaani kama kilizikwa wakati wa kampeni na siku ya uchaguzi. Licha ya kuwapo upendeleo wa wazi kwa chama tawala na kutokuwapo uwanja sawa wa ushindani, umma haukuihurumia BNP.

Hii haina maana ya kusema kwamba BNP haina nafasi ya kushinda chaguzi au kurejesha umaarufu wake iwapo kura zingekuwa huru na za haki.

Kwamba kutokana na sifa na tuhuma chafu zinazoikabili BNP za kweli au uongo na viongozi wake zinaonesha wazi iwapo kutakuwa na ufufuo wowote wa BNP utakuwa ni matokeo ya hasira za wapiga kura dhidi ya serikali ya Hasina na si kuunga mkono upinzani.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
585,000SubscribersSubscribe

Latest Articles