21.2 C
Dar es Salaam
Sunday, August 14, 2022

Taasisi za kupambana na ufisadi katikati ya vita vya kisiasa

ISIJI DOMINIC

SERIKALI ya Rais Uhuru Kenyatta imedhamiria kupambana na ufisadi lakini cheche za wanasiasa zikilenga hususani Uchaguzi Mkuu wa 2022 inaipa wakati mgumu taasisi za kupambana na ufisadi kufanya kazi yao.

Rais Uhuru alipoapishwa kuhudumu muhula wake wa pili aliweka wazi dhamira yake ya kupambana na ufisadi na moja ya hatua aliyochukua ni kuwateua makachero kushika nyadhifa nyeti za taasisi za serikali zinazopambana na vita hivyo.

Mkurugenzi wa Upelelezi Makosa ya Jinai (DCI), George Kinoti, Mkurugenzi wa Mashtaka ya Jinai (DPP), Noordin Haji na Ofisa Mtendaji Mkuu wa Tume ya Maadili na Kupambana na Ufisadi (EACC), Twalib Mbarak, wote wameshawahi kuwa majasusi na hawaogopi kuwakamata, kuwahoji na hata kuwafikisha mahakamani watu maarufu, matajiri, mawaziri na wanasiasa wenye majina makubwa.

Rais Uhuru ameonesha imani yake kwa taasisi hizi tatu na hata Wakenya wengi wanaunga mkono utendaji kazi wa DCI, DPP na EACC. Aidha Rais Uhuru mara nyingi amekuwa akisisitiza rushwa haina uhusiano na kabila lolote mbali ni hulka ya mtu na kuongeza wote waliotafuna mali ya umma watakabiliwa na mkono wa sheria.

Wanasiasa kwa upande wao wamekuwa wakihusisha vita dhidi ya ufisadi na uchaguzi mkuu wa 2022 huku wakisema inalenga kabila fulani au njama ya kumzuia kiongozi fulani kutowania nafasi ya urais pindi Uhuru atakapomaliza muda wake.

Wanaotajwa sana kumrithi Rais Uhuru ni Naibu Rais William Ruto na kinara wa upinzani Raila Odinga. Wawili hawa pamoja na washirika wao kisiasa wamekuwa wakitumia majukwaa kulumbana hadharani huku wakitaja taasisi za kupambana na ufisadi.

Moja ya sakata kubwa ya ufisadi iliyogonga vichwa vya habari kwa siku za hivi karibuni hadi kupelekea Waziri wa Fedha, Henry Rotich, kuhojiwa ofisi za DCI kwa siku kadhaa ni namna Shilingi bilioni 21 (sawa na Shilingi bilioni 487 za Tanzania) zilivyotumika katika ujenzi wa mabwawa mawili kaunti ya Elgeyo Marakwet.

Hata hivyo, Naibu Rais Ruto, amesisitiza Serikali inafuatilia matumizi ya kila shilingi inayotolewa na kinachopaswa kuhojiwa ni Shilingi bilioni saba (sawa na Shilingi bilioni 162 za Tanzania).

Raila ambaye ni kiongozi wa ODM ameendelea kumtaka Rais Uhuru kukaza kamba vita dhidi ya ufisadi na kusema katika vita hivi hakuna aliyejuu ya sheria.

“Kama kuna mtu ameiba pesa, usiende na kupiga kelele eti Shilingi bilioni 7 sio kitu. Shilingi bilioni 7 sio salio kuweka mfukoni! Sio pesa ya kununua mandazi halafu wanaenda pande hii wanasema ooh sisi ni wakulima… akitoka pale ooh mimi ni mfugaji… yeye ni kama popo,” alisema Raila akidaiwa kumlenga Naibu Rais.

Ni kauli iliyomuibua Ruto akimshutumu kiongozi huyo wa upinzani kwa nia yake ya kuhukumu kila mradi unaoanzishwa na serikali.

“Wamebuni dhana zao kwamba kila mipango ya serikali ina harufu ya ufisadi. Hatutawaruhusu wale ambao wamepania kufanya watu wawe masikini na kupiga vita kila miradi ya maendeleo kwa kutumia takwimu za uongo, habari za uongo na taarifa za uongo kwa malengo ya kufifisha ajenda za maendeleo ya nchi yetu,” alisema Naibu Rais.

Aliendelea kuwaonya kuhusu uvumi wao wa mabwawa ya Arror na Kimwarerr usiokuwa na ushahidi kwamba wanapaswa kufahamu unawalenga takribani watu 100,000 wanaotegemea maji kutoka mabwawa hayo na sio yeye Naibu Rais au mtu yeyote.

Wanachotaka wananchi chini ya uongozi wa Rais Uhuru ni siasa ziwekwe pembeni na kuacha mamlaka za serikali zinazopambana na ufisadi kufanya kazi yao ili kujua mbivu na mbichi.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
198,656FollowersFollow
550,000SubscribersSubscribe

Latest Articles