28.2 C
Dar es Salaam
Tuesday, June 6, 2023

Contact us: [email protected]

NMB yatoa mafunzo ya ujasiriamali kwa vijana 200 Dodoma

Na Mwandishi Wetu, Dodoma

ZAIDI ya vijana 200 wanaojishughulisha na usafishaji wa abiria kwa bodaboda na pikipiki za miguu mitatu(Bajaji), mwishoni mwa wiki wamepatiwa mafunzo ya namna ya kujiongezea kipato yaliyotolewa na benki ya NMB.

Lengo la mafunzo hayo ni kuwapa elimu ya mikopo inayotolewa na benki hiyo katika mpango wao wa miliki chombo na NMB ambao umetenga Sh bilioni 5 katika kundi hilo.

Naibu Meya wa Jiji la Dodoma, Emmanuel Chibago (wa pili kushoto) akikata utepe kuashiria uzinduzi rasmi wa kampeni ya Mastaboda Jijini Dodoma inayolenga kuwakopesha vijana bodaboda na pikipiki za miguu mkitatu,hafla ya uzinduzi huo ilifanyika jijini Dodoma mwishoni wa wiki. Kushoto ni Meneja wa benki ya NMB Kanda ya Kati, Nsolo Mlozi na mwisho kulia ni Mkuu wa Idara ya Kadi NMB, Philbert Casmir, Mkuu wa Idara ya Biashara, Alex Mageni na Mwenyekiti wa Wendesha Bodaboda Dodoma, Kenneth Chimoti.

Wengi wa vijana hao walikuwa wahitimu wa vyuo vikuu ambao waliamua kujiajiri kupitia bodaboda na pikipiki za miguu mitatu ambao hata hivyo waliomba NMB kuangalia upya sharti la mtu kuwekeza asilimia 20 ndipo akopeshwe kwamba utazamwe kwani unawakosesha fursa vijana wengi.

Akizungumza muda mfupi baada ya uzinduzi wa mikopo ya Pikipiki za miguu miwili na Mitatu, Mwendesha boda boda wa jijini Dodoma Chacha Marwa alisema mpango wa NMB ni mkombozi kwa vijana ambao wanaanza maisha kwa kuwa utasaidia kuwapatia vifaa vya kuwaingizia fedha.

Marwa ambaye ni mhitimu wa Shahada ya sayansi ya baiolojia ya Chuo Kikuu cha Dodoma, alisema mpango wa kusubiri ajira unawachelewesha na kuwapotezea malengo vijana wengi lakini kwenye bodaboda na pikipiki za miguu mitatu kuna fedha zaidi ya mshahara.

“Binafsi nimepita katika mapito mengi, nimeendesha bodaboda za watu nikaingia mikataba lakini hadi sasa naendesha gari ndogo yangu na pikipiki na pikipiki za miguu mitatu nimewapa vijana,” alisema Marwa.

Akizungumzia asilimia 20 ambazo zinatakiwa na NMB kama zamana ya mkopo, alisema kiasi hicho kinawakosesha sifa vijana wengi licha ya kuwa wanauwezo wa kurejesha lakini ni pale wanapoanza maisha huwa hawana kianzio.

Kwa mujibu wa Chacha kama benki ingetengeneza utaratibu wa kuwapatia vijana bila kuweka hiyo asilimia ingekuwa mkombozi mkubwa kwa  vijana wengi ambao huzunguka na vyeti kusaka ajira bila mafanikio.

Meneja wa NMB kanda ya kati Nsolo Mlozi alisema miliki chombo na NMB imeshafika katika mikoa ya Dar es Salaam, Mwanza na Dodoma na sehemu kubwa inalenga vijana wanaoanza maisha.

Mlozi alisema benki hiyo hutumia changamoto zinazojitokeza kwa Watanzania na kuwapelekea mawazo ya kuwa fursa hivyo mambo mengi wanayozungumza vijana yanafanyiwa kazi kwa kufuata taratibu.

Kwa upande wake Naibu Meya wa Jiji la Dodoma, Emmanuel Chibago aliomba benki kuwawezesha vijana hao kupitia Umoja wa Mabajaji na Pikipiki Dodoma (UMAPIDO) kwani wamekuwa wasimamizi wazuri kwa wanaokopa.

Chibago alitolea mfano kuwa mwaka jana halmashauri ya Jiji la Dodoma ilitoa mkopo kwa UMAPIDO wa Sh milioni 305 lakini hawajawahi kuchelewesha marejesho na kila mwezi wanarejesha Sh milioni 12.5.

Naibu Meya aliwataka vijana kuwa waaminifu kwa Taasisi na mashirika yanayowatambua na kuwapatia mikopo ili waweke malengo ya kujikomboa kimaisha.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
213,307FollowersFollow
568,000SubscribersSubscribe

Latest Articles