24.1 C
Dar es Salaam
Thursday, October 21, 2021

NJIA WANAZOTUMIA POLISI KUKAMATA PIKIPIKI SI SALAMA

Na FARAJA MASINDE


PAMOJA na changamoto mbalimbali zinazowakabili barabarani, bado mnaendelea kufanya kazi bila hatua madhubuti za kumaliza changamoto hizo kuchukuliwa.

Ni wazi kuwa waendesha pikipiki mnakabiliwa na changamoto nyingi ikiwamo kukimbizwa na kuvamiwa na waliopata tenda ya kuzikamata bodaboda zote zinazoingia mjini.

Nasema ni bodaboda zote kwa sababu uvamizi unavyofanyika wa kuikamata pikipiki hauchagui mwenye kibali ama asiyekuwa na kibali. Ukamataji wa vijana hao unatia aibu na kusikitisha, pia ni hatari na unaweza kuhatarisha maisha ya anayekamatwa na anayekamata.

Hilo limekuwa likipigiwa kelele lakini wakamataji wameona hiyo ya kuvamia pikipiki kwa nyuma ndio mbinu nzuri ya kuwadhibiti madereva wa bodaboda.

Nimeshuhudia mkamataji akikimbiza pikipiki kati kati ya magari na ilipopunguza mwendo alimvamia dereva kwa nyuma akamvuta wakaanza kunyang’anyana funguo.

Tukio hilo lilitokea hivi karibuni katika eneo la Salenda saa nne asubuhi, tukio hilo lilikusanya watu ambao wengi walihisi kwamba aliyekamatwa atakuwa kaiba pikipiki jambo ambalo si kweli.

Kijana alipokamatwa akashuka katika pikipiki, watu wakakusanyika huku wengine wakishuka katika magari sababu foleni ilikuwa kubwa.

Walipokusanyika kusikiliza tatizo wakasikia mkamataji akitaka kibali cha kuingia na pikipiki mjini, akaanza kumhoji ndipo watu waliposhtuka na kuanza kusonya.

Askari wa usalama barabarani aliyekuwapo jirani aliwaambia wazi kwamba huo si ukamataji, mnaweza kusababisha madhara makubwa. Wananchi walikuwa na hasira, mmoja aliinua kofi akampiga aliyemkamata yule dereva, kwamba hakuwa mstaarabu na amesumbua watu. Walichukua dakika kadhaa kuzozana na baadaye aliyempiga kofi mkamataji akaonekana kaingilia kazi za watu.

Pamoja na kumuona kaingilia kazi za watu na kujichukulia sheria mkononi ukweli utaendelea kubakia kwamba utaratibu si mzuri, hivyo kupigwa ni tukio endelevu. Wakamataji mmekuwa hamjifunzi kutokana na mazingira, hivi karibu yametokea matukio mengi yanayohusu mapambano kati ya askari na bodaboda, yote hayo ni kutokana na mchakato huo huo wa kukamatana kama wote vibaka.

Kwa hali ilivyo atakayewadhuru ninyi wakamataji si bodaboda pekee bali hata wananchi wa pembeni ambao watawadhani ninyi ni wezi ama mwenye bodaboda ndiye mwizi. Vijana wanaokamata bodaboda wamepewa mafunzo na kama hili haliwezekani, serikali ipange utaratibu mwingine, uliopo sasa haufai.

Wanaokamata hawana tahadhari ya aina yoyote anapovamia pikipiki, sijui hata wanajiamini nini kufanya hivyo.

Wanatakiwa kujua kwamba si kila aliyekuwa na pikipiki anaufahamu utaratibu wao wa kuvamia pikipiki, wajue katika Jiji la Dar es Salaam kila kukicha wanakuja wageni wapya hivyo utaratibu huo usipoangaliwa kwa macho mawili utasababisha madhara.

Kwani tunashuhudia kwa nyakati tofauti Jeshi la Polisi likiendelea kutilia mkazo juu ya kukamatwa kwa pikipiki zote zinazothubutu kuingia katikati ya mji licha ya ukweli kwamba namna ukamataji unavyofanyika bado ni hatari kwa usalama wa waendeshaji.

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

66,457FansLike
162,644FollowersFollow
522,000SubscribersSubscribe

Latest Articles