26.4 C
Dar es Salaam
Wednesday, December 6, 2023

Contact us: [email protected]

Nilivyopokewa kwa tabasamu, kushuhudia mengi Thailand

Bakari Kimwanga-Aliyekuwa Bangkok, Thailand

SAWADIKA ni salamu ambayo hutolewa kwa mwanamke, na Sawadikrapu hutolewa kwa mwanamume ikimaanisha habari pindi uingiapo nchini Thailand.

Unaponunua au kumpa mtu chochote basi utajibiwa kwa neno Koponhka, likiwa na maana ya ahsante sana.

Haikuwa kazi rahisi kufika katika Jiji la Bangkok nchini Thailand, lakini tu kwa uwezo wa Mungu, nami nilibahatika kufika nchini humo.

Ilikuwa Agosti 17, mwaka huu, ilipofika saa 7 mchana nilianza safari kutoka nyumbani na kueleka Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere, ambapo nilisoma maelezo ya tiketi yangu ya ndege ya Shirika la Ndege la Qatar ikiniambia kwamba ninataka kuwa uwanja wa ndege mpya wa Terminal III kuanzia saa 9:5 alasiri kwa ajili ya safari.

Nilifika Uwanja wa Ndege wa Julius Nyerere saa 8 mchana, ambapo mimi na wasafiri wenzangu ambao tulikuwa tukisafiri na ndege ya Qatar tulipewa maelezo ya kututaka kuanza kukaguliwa kuanzia saa 9:5 alasiri. Nikiwa nimekaa kwenye viti na abiria wenzangu nilianza kuvutataswira nzito kuhusu safari itakavyokuwa kutoka Dar es Salaam hadi katika Jiji la Bangkok nchini Thailand.

Mmoja wa watumishi wa USAIDWildlife Asia, akimkaribisha Bakari Kimwanga chakula cha utamaduni kwa Thailand

Hakika muda ukafika tukakaguliwa na kuingia ndani ya uwanja mpya wa ndege huku mawazo yaliyoambatana na usingizi yalikuwa ni jinsi nitakavyoshuhudia mji huo.

Naam; ilipofika saa 11 jioni abiria tulitangaziwa kwamba sasa tunaaza kuingia ndani ndege awamu kwa awamu, ambapo mimi nakumbuka tiketi yangu ilikuwa imeandika ‘Zone 3’ tukaitwa nami nikajongea huku nikiwa na picha sasa tunaanza safari lakini je, ndani ya ndege itakuwaje?

Nikiwa ndani ya ndege kwenye kiti changu namba 24 E huku jirani yangu akiwa ameketi mwenzangu, Exper Pius, ambaye ni mtaalamu wa mazingira na mtumishi wa Taasisi ya Kimataifa ya RTI iliyo chini ya USAID Protect Tanzania, chini ya mradi wa Wildlife Combating Crime, ikiwa inaangazia masuala ya usafirishaji haramu wa wanyama.

Ndani ya ndege nikaanza kumuuliza maswali kadhaa je, hii safari yetu itakuwaje? Jibu lake lilikuwa jepesi, tuombe Mungu tutafika salama Thailand, hakika tunakwenda mashariki ya mbali, ambapo tutafika kesho mchana wakati huku kwetu itakuwa ni asubuhi.

Licha ya wahudumu kupita na kunipa viburudisho, lakini bado akili yangu ilikuwa ikipiga picha Thailand hasa Bangkok ikoje!

Ilipofika saa 12 jioni abiria wote tuliokuwamo ndani ya ndege, tukatangaziwa tena umuhimu wa kufunga mikanda huku wahudumu wa ndege wakiwa wanapita katika kila kiti na kumkagua abiria kama amefunga mkanda.

Kazi hiyo ikakamilika likatoka tangazo ya kwamba sasa tunaanza safari, mara ndege ikachochewa injini kelele zikawa nyingi, huku mitetemo ikitamalaki watu tukiwa vitini kwa utulivu huku kila mmoja amefunga mkanda.

Ndege ukajisogeza taratibu kwenye njia yake na kuanza kupaa angani, huku nikiwa kitini na kazi ya kusima ramani kupitia ‘tv ndogo ya kwenye kiti’ na kuona tunamaliza anga ya Tanzania kuingia Kenya na kisha Somalia, baada ya muda usingizi ukanipitia na ilipofika saa 7:30 usiku tulitua Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Hamadi mjini Doha nchini Qatar.

Tukashuka na kuanza kutafuta ndege nyingine ya kuelekea Bangkok nchini Thailand, ukubwa wa unjwa wa Kimataifa wa Hamadi Doha, ulinishangaza na kuona alaa kumbe dunia ina mambo mazuri na kila mtu yupo mbio na baada ya kutembea kwa umbali mrefu hatimaye tulilifikia geti namba nane, tulilotakiwa kupita ili kuanza safari yetu ya pili.

Mungu alitusaidia na tulitimiza wajibu wetu ikiwamo ukaguzi na kukaa mapumziko kidogo na ilipofika saa 8 usiku tulitangaziwa na abiria kuanza ukaguzi wa tiketi zetu kwa ‘zone’ ambayo nami ilinifikia tena zone namba tatu huku nikiwa na tikiti yangu.

Tulikamilisha taratibu na kuingia ndani ya ndege tukafunga mikanda na ilipofika saa 8:30 usiku safari ikaanza ya kukata anga na na tukafanikiwa kufika saa 7 mchana ya siku ya pili na kutua katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Suvarnabhumi ambao ni mkubwa huku ukiwa unapokea idadi kubwa ya ndege za kimataifa na wageni kutoka mataifa mbalimbali.

Tuliposhuka tu, wahudumu tuliowakutana nao walianza na salama Sawadikrapu, wote wakiinamisha mikono yao kwenye kifua na kuinama name nikajibu Sadika, kwa kuwa alikuwa ni mwanamama.

Lakini cha kuashangaza kila tulipokuwa tunapita pale uwanjani, raia wa Thailand nyuso zao zilijawa na tabasamu kiasi kwamba hata mgeni kujihisi nipo eneo salama na kila nikiulizwa swali na maofisa wa uhamiaji pale uwanjani nalijihisi kwamba sina tatizo kwa kuwa hawakuwa ni wenye kukunja uso kama tulivyozoea kwa askari wengine wawapo katika majukumu yao.

Wananchi jijini Bangkok wakiweka maua kwenye eneo maalumu la ibada

Tulikamilisha taratibu na kuanza kutoka pale uwanjani, kwa kweli ilikuwa ni safari nzuri huku wenyeji wetu wakiwa ni wenye furaha mno kwetu wakati wote.

Tulifika hadi Hoteli ya Grande Centre Point na kupokewa na wahudumu wenye tabasabu wakati wote huku nikiwa na shauku kubwa ya kujua kwa undani kwa nini watu wake ni wakarimu wakati wote.

Mwenyeji wetu Dararat Weerapong, akatuchukua hadi katika moja ya mgahawa na kupata mlo wa mchana, lakini wale wahudumu muda wote wakizunguka kuhakikisha natimiziwa mahitaji yangu.

Siku zangu zote nilizokuwa Thailand nilipata maelezo kadhaa kutoka kwa mmoja wa marafiki zangu Pratch Rujivanarom, akaniambia kwamba moja ya utamaduni kwa watu wa Taifa la Thailand ni tabasamu wakati wote, kwani hata historia inaonesha kwamba Thailand ni nchi ya ‘tabasamu’.

Pia alikwenda mbali zaidi na kunieleza kwamba wananchi wa taifa hilo wengi wao ni watu wachakarikaji si wa kukaa na kuletewa na hata pindi wanapokuwa katika biashara zao, muda mwingi huongozwa na ukarimu unaombatana na tamasabu kiasi cha kujenga imani kwa wateja wao wakati wote.

“Tabasamu ni sifa kubwa kwetu kwani Thailand ni ‘Business Hub’ kwa nchi zote za Asia ya Kusini. Ndio maana hii Bangkok ina watu asilimia 30 ya watu wote wa Thailand ambao kwa sasa wanakadiriwa kufikia zaidi ya milioni 67.

“Lakini hata hivyo, hapa tumeweza kuendelea, tuna treni ya umeme ambayo inachukua watu wengi mno, pia tuna barabara nyingi zikiwamo za juu lakini zipo pia njia ya kulipia ‘By pass’, ambazo zimekuwa ni msaada mkubwa mno,” anasema Rujivanarom.

Kidogo akanipeleka kwenye historia ya taifa hilo na kusema kuwa  nchi hiyo ilijulikana kama Uthai (Siam) ni nchi ya kifalme katika Asia ya Kusini – Mashariki.

Imepakana na Laos, Kambodia, Malaysia na Myanmar. Ina pwani kwenye Ghuba ya Uthai ya Bahari ya Kusini ya China, upande wa Kusini na Bahari Hindi upande wa Magharibi. Nchi hiyo ina wakazi zaidi ya milioni 67 hivyo, inashika nafasi ya 20 duniani.

Mji Mkuu na mkubwa ni Bangkok, ukiwa na wakazi zaidi ya milioni nane. Nchi iliitwa rasmi Siam hadi mwaka 1939, tena kati ya 1945 na 1949.

Neno Thai  linamaanisha ‘uhuru’ kwa Kithai, pia ni jina la kundi kubwa la watu nchini ambao ni Wathai asilimia 75 – 85, mbali na Wathai-Wachina asilimia 12.

Tangu Septemba 19, 2006 nchi imekuwa ikitawaliwa na kamati ya jeshi. Jeshi ilipindua Serikali ya Waziri Mkuu Thaksin Shinawatra, bila kumwaga damu. Viongozi wa kijeshi walipatana na mfalme kwamba wataandaa uchaguzi mpya.

Nchini Uthai kuna lugha za asili 73 kati yake, Kithai ndiyo lugha rasmi. Wathai walio wengi, asilimia 94.6 hufuata dini ya Ubuddha katika madhehebu ya Theravada. Kusini, mpakani kwa Malaysia, kuna Waislamu asilimia 4.6 na Wakristo ni asilimia 0.7.

Kwa hakika nimefika Thailand na kushuhudia kuwa ni nchi ya tabasamu wakati wote huku maendeleo yakishika kasi.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
580,000SubscribersSubscribe

Latest Articles