24.8 C
Dar es Salaam
Thursday, September 21, 2023

Contact us: [email protected]

Tembo wavamia makazi ya watu, wala chakula cha akiba

Derick Milton, Simiyu

Jumla ya kaya 11 katika kijiji cha Halawa Wilaya ya Bariadi mkoani Simiyu, hazina chakula wala mahali pa kuishi baada ya nyumba zao kuvamiwa na tembo na kuharibiwa vibaya.

Licha ya nyumba hizo kuharibiwa, tembo hao pia wamekula chakula chote kilichohifadhiwa ndani ya nyumba hizo.

Tembo hao zaidi ya 10 waliotoka katika pori la akiba Maswa, wanadaiwa kuvamia kijiji hicho usiku wa kuamkia jana Septemba Mosi,  saa saba usiku, ambapo waliezua nyumba 11 za familia saba zenye watu zaidi ya 50.

Mmoja wa wananchi walionusurika na kadhia hiyo, Mwalu Nsulwa amesema tembo hao walivamia kwenye nyumba yake na kula mahindi yote gunia tano na viazi vilivyokuwa vimehifadhiwa ndani.

“Baada ya tembo kuvamia walianza kula mahindi na viazi vyote wakamaliza na wameezua hadi nyumba na sasa sina sehemu ya kuishi.

“Wakati wanaingia mimi na watoto wangu wawili tulijificha uvunguni mwa kitanda ili kunusuru maisha yetu,” amesema Nsulwa.

Aidha, Mtendaji wa kijiji hicho Mayenga Matongo amesema tembo hao walivamia kaya saba na kuezua nyumba zote 11 na kula mahindi magunia 42, viazi magunia sita huku akibainisha kuwa hakuna vifo vilivyotokea.

“Familia hizi hazina sehemu ya kulala tena maana nyumba zao zimeharibiwa vibaya, hawana hata chakula kutokana na kuliwa na tembo na kilikuwa kimehifadhiwa ndani ya nyumba zao,” amesema Matongo.

Mkuu wa Wilaya Bariadi, Festo Kiswaga na baadhi ya viongozi wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), wilayani humo, wakikabidhia msaada wa chakula kwa wananchi ambao nyumba zao ziliharibiwa na tembo hao.
Picha na Derick Milton

Naye Mkuu wa Wilaya hiyo, Festo Kiswaga akiwa na viongozi wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Wilaya, walifika eneo la tukio na kutoa pole kwa wananchi hao ikiwa pamoja na kutoa msaada wa chakula vikiwamo unga kilo 220, maharage kilo 50 na sukari kilo 20.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,690FollowersFollow
574,000SubscribersSubscribe

Latest Articles