21.9 C
Dar es Salaam
Monday, August 15, 2022

NHIF: Gharama mpya za matibabu Desemba

nhif-bernard-kongaNa JONAS MUSHI – DAR ES SALAAM

MFUKO wa Taifa wa Bima ya Afya (NHIF) utatangaza gharama mpya za matibabu kwa wanachama wa mfuko huo wanaohudumiwa na hospitali zenye mkataba.

Gharama hizo zitatangazwa baada ya NHIF kuketi kwenye meza ya mazungumzo na hospitali zilizosaini kutoa huduma ya matibabu kwa wanachama wa mfuko huo ili kumaliza mvutano kuhusu mabadiliko ya utoaji huduma.

Mvutano baina ya NHIF na hospitali zinazotoa huduma kwa wanachama wa mfuko huo uliibuka baada ya baadhi ya hospitali binafsi kudai mabadiliko ya bei za huduma yaliyofanywa na NHIF yaliyoanza kutumika Julai mwaka huu hayana uhalisia.

Katika malalamiko hayo, wamiliki wa hospitali hizo walidai kuwa bei za utoaji huduma zimepunguzwa kiasi kwamba zinahatarisha uendeshaji wa taasisi zao.

Akizungumza na waandishi wa habari jana jijini Dar es Salaam, Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa NHIF, Bernard Konga, alisema bei hizo zitaendelea kutumika hadi Desemba mwaka huu watakapokutana na wadau hao kujadili hoja zao na kufikia mwafaka.

Hata hivyo, alisema suala la mabadiliko ya bei huwa linafanyika kila mara inapohitajika kwa kuzingatia ushauri wa kitaalamu wa tathmini ya uhai wa mfuko, matokeo ya tafiti mbalimbali, maelekezo yanayotolewa na wizara na bodi ya wakurugenzi na maoni, ushauri na malalamiko yanayotolewa na wadau wakiwemo watoa huduma, wanachama na vyama vinavyowakilisha watoa huduma.

Alisema bei mpya ni makubaliano ya pande zote na zinatekelezwa chini ya mkataba ambao husainiwa kati yao na watoa huduma na kwamba atakayekiuka masharti ya mkataba atachukuliwa hatua za kisheria.

Alisema hadi sasa baadhi ya watoa huduma wamekwishasaini mikataba hiyo na kukubaliana na bei hizo na wengine wanaendelea kusaini na kwamba kinachoonekana kuwa ni mvutano, ni maombi na maoni ya baadhi ya watoa huduma wakitaka kufanyike marekebisho katika baadhi ya mambo.

“Hili suala linahusu maisha ya watu hivyo tunapofanya mabadiliko ya bei lazima tukae tukubaliane na inapotokea kuna vitu ambavyo haviendi sawa lazima tukae meza moja na watoa huduma kujadili ili kufikia mwafaka.

“Ndiyo maana tumesema bei hizi tutaziangalia kwa miezi sita wakati tunaendelea kupokea maoni na malalamiko kutoka kwa watoa huduma na ikifika Desemba tutakutana na kujadili hoja zao na sisi tutatoa hoja zetu.

“Hatuwezi kusema bei tulizopanga ndiyo mwafaka kwa sababu tunapokutana na kukubaliana bei ni suala moja na utekelezaji ni suala jingine, hivyo lazima tuwape nafasi ya kutueleza hali iko vipi katika utekelezaji ili tujue pakurekebisha,” alisema Konga.

Alisema malalamiko waliyoyapata ni ya gharama za kumwona daktari, utoaji wa vipimo na dawa.

Konga alisema licha ya malalamiko hayo upo ukweli kuwa mabadiliko hayo (kupanda na kushuka kwa baadhi ya gharama), gharama zimeongezeka kwa wastani wa asilimia 13.

“Mabadiliko haya yamehusisha kushuka na kupanda kwa gharama kwa kuzingatia aina ya huduma/dawa na daraja la kituo kinachotoa huduma lakini kwa wastani gharama zimeongezeka kwa asilimia 13.

“Sasa hivi tofauti na awali, gharama ya kumwona daktari ni sawa kwa kuzingatia daraja la kituo na utaalamu wa daktari badala ya kuangalia daraja la kituo pekee.

“Awali ilikuwa ada ya kumwona daktari bingwa akiwa katika hospitali ya mkoa analipwa shilingi 2,000 lakini daktari wa hadhi hiyo hiyo akiwa hospitali ya kanda ni shilingi 20,000, akiwa Muhimbili ni shilingi 40,000.

“Kwa upande wa vituo binafsi unakuta daktari bingwa yupo kwenye hospitali yenye hadhi ya mkoa au kanda, kwa hiyo anajiuliza kwanini huyu mgonjwa nisimwambie jioni tukutane kwenye kliniki yangu akijua kule atapata fedha nyingi.

“Tulichofanya sasa ni kupandisha madaktari bingwa wote iwe ni shilingi 15,000 na hii itazuia mrundikano wa madaktari sehemu moja kwa sababu awali walikuwa wanakimbilia kwenye fedha nyingi kwa hiyo utaona tumepandisha kwa wale waliokuwa wanalipwa shilingi 2,000 watalipwa shilingi 15,000 na wale wa wilaya waliokuwa wanalipwa shilingi 1,000 watalipwa shilingi 10,000,” alisema.

Konga alisema gharama za vipimo na dawa zimewekwa kwa ulinganifu katika vituo vyote na gharama za upasuaji wa uzazi na kufunga mirija ya uzazi kutoka Sh 130,000 hadi Sh 300,000 na upasuaji wa kidole tumbo imetoka 130,000 hadi 300,000 ambalo ni ongezeko la asilimia 65.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
198,717FollowersFollow
550,000SubscribersSubscribe

Latest Articles