23.3 C
Dar es Salaam
Saturday, April 20, 2024

Contact us: [email protected]

Kinyongo kinasababisha kansa

dk-michael-barry-akizungumzia-utafiti-wake-ambao-umebaini-kuwapo-uhusiano-kati-ya-magonjwa-ya-kansa-na-tabia-ya-baadhi-ya-watu-kushindwa-kusamehe*Daktari wa Marekani asema asilimia 61 ya magonja ya kansa ni matokeo ya kushindwa kusamehe

 VERONICA ROMWALD Na HERIETH MANDARI – DAR ES SALAAM

UTAFITI uliofanywa nchini Marekani umebaini kuwa asilimia 61 ya magonjwa ya saratani yanasababishwa na tabia ya watu kushindwa kusamehe wenzao waliowakosea.

Daktari Michael Barry ndiye aliyefanya utafiti huo nchini humo, ambapo sasa ameanzisha kliniki ya matibabu ya kusamehe ‘Forgiveness Therapy’.

Anasema watu wengi hushindwa kuwasamehe wenzao, hali ambayo huwasababishia msongo wa mawazo.

“Wanakuwa hawana amani moyoni, muda mrefu wanakuwa na msongo wa mawazo dhidi ya wale waliowakosea, mwisho hujikuta wakiugua maradhi haya ya saratani,” anasema.

Daktari bingwa wa kutibu magonjwa ya akili na mihemko, Steven Standiford wa Marekani, anasema suala hilo lina ukweli ndani yake.

“Wengi hushindwa kuhimili hali ya kutokusamehe lakini pasipo kujua kwamba hali hiyo huchangia kujiua wenyewe, kwani huwasababishia kupatwa na maradhi mbalimbali,” anasema.

Akizungumza na MTANZANIA Jumamosi, Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Saratani, Ocean Road, Dk. Julius Mwaiselage, alisema anakubaliana na utafiti huo kwa kiasi fulani.

“Nimeona ni moja ya form za ‘spiritual medicine… alternative medicine’, lakini kikubwa imelenga ku-control mwenendo wa afya ya mgonjwa ili asiwe na msongo wa mawazo.

“Matibabu hayo huenda yatasaidia kufanya utendaji kazi wa chembechembe ambazo zinataka kubadilika kuwa saratani zirudi katika hali yake ya kawaida,” alisema.

Alisema hata hivyo, pamoja na hayo, bado tafiti zaidi zinatakiwa kufanyika ili kujua hasa ni saratani ya aina gani ambazo zinaweza kuzuilika kwa njia hiyo.

“Na tafiti hizi ziwe hasa katika nchi zinazoendelea ambapo chanzo kikuu cha saratani zinazoongoza zinatokana na maambukizi kama virusi,” alisema.

Katika utafiti wake, Daktari huyo wa Marekani, Barry, anaamini kupitia msamaha lolote linawezekana.

Katika kitabu chake kipya kiitwacho ‘The Forgiveness Project’ (Mpango wa kusamehe) kinachoelezea uvumbuzi wa ajabu wa jinsi ya kupambana na ugonjwa wa saratani, kuwa na afya njema na kuwa na amani,  Dk. Barry anaelezea uchunguzi alioufanya juu ya umuhimu wa msamaha katika afya na unavyoweza kuleta tiba ya ugonjwa mkubwa kama saratani.

Dk. Barry katika kuonyesha kwamba msamaha una nafasi kubwa katika afya ya binadamu, anasema hata dini zinaamini katika kusamehe.

“Hali ya kuweka kinyongo ama hasira moyoni ni hatari kwa afya zetu na pia ni hatari katika ustawi kiroho ambapo inaweza kuharibu familia, ndoa na hata makanisa. Lakini ni vipi kwa upande wa afya ya kimwili? Je, kuna uhusiano wowote kati ya hali ya  kutokusamehe na saratani? Kati ya hali ya kusamehe na kuponya? Ni kwa jinsi gani unaweza kusamehe kwa dhati?

“Baada ya kufanya utafiti wa kisayansi, kitheolojia na kijamii kwa kushirikiana na uzoefu kutoka kliniki ya saratani ya nchini Marekani, nimegundua mambo makubwa katika kuoanisha kinga ya mwili na msamaha na kwamba vina uhusiano mkubwa sana katika afya ya mwili wa binadamu,” anasema.

Kupitia shuhuda mbalimbali za wagonjwa wapatao watano wa saratani, Dk. Barry ameweza kusaidia wasomaji wake kutofautisha na kupambana na vikwazo vyote vinavyokwamisha tiba na amani.

“Saratani ni ugonjwa mbaya sana na ambao tiba yake pia ni ngumu, lakini sisi wenyewe tunao uwezo wa kujitibu, kwa kutibu kwanza mawazo yetu, na mioyo yetu kupitia msamaha ambapo kwa msamaha huo miili yetu itatii,” anasema.

Katika kitabu hicho cha ‘The Forgiveness Project’, kinaelezea shuhuda mbalimbali, ikiwemo ya Jayne, mmoja wa wahanga wa ugonjwa huo ambaye alikuwa na saratani ya matiti na akaweza kupata uponyaji kwa kusamehe.

Shuhuda nyingine ni Cathy, ambaye anaeleza jinsi msamaha ulivyoleta mabadiliko chanya katika mahusiano.

Naye Sharon anasema kupitia hali ya kusamehe ameweza kupata uponyaji au tiba wakati akiendelea na tiba ya saratani.

Dk. Barry, ambaye pia ni mchungaji, anasema vitabu vingi vimekuwa vikielezea kuhusu suala la msamaha, lakini ni wachache wamekuwa wakihusisha msamaha na ustawi wa afya.

Kitabu cha ‘The Forgiveness Project’ kimeelezea tafiti za kisayansi ambazo ni rahisi kuzielewa kwa lugha nyepesi na inayoeleweka na kimetoa njia itakayosaidia watu kusahau matendo mabaya yaliyopita na kupata amani.

Dk. Barry ni mkurugenzi wa huduma ya utoaji tiba, amekuwa akitoa huduma katika makanisa kwa miaka zaidi ya 20 na amekuwa akitoa elimu katika vipindi vya luninga na redio nchini Marekani.

Ni mwandishi wa vitabu vingine mbalimbali, vikiwemo ‘A Reason for Hope, ‘A Season for Hope’ na ‘The Art of Care giving’.

Mwandishi huyo wa vitabu alijitoa kwa miaka kadhaa katika kufanya utafiti kuhusu mahusiano kati ya msongo wa mawazo, kutokusamehe na ugonjwa wa saratani.

Inakadiriwa kwamba, jumla ya taarifa za wagonjwa wapya wa saratani wapatao milioni 1.5 zimeripotiwa katika kipindi cha mwaka 2010 zikiwa na makadirio ya vifo vya watu 570,000 kwa mwaka huo peke yake.

 

Kusamehe kuna nguvu:

Iwapo utasamehe au ukijisamehe mwenyewe nafsi yako, kwa kufanya hivyo kutakuweka huru kuondokana na mambo yaliyokuwa yanakusumbua na hivyo kukufanya kutekeleza masuala yako mengine muhimu.

Vile vile kunakuweka huru kiakili na kihisia na hivyo kukuwezesha kutumia akili yako kuanza upya maisha bora.

Msamaha unakusaidia kufikia malengo yako uliyojiwekea, labda unataka kazi nzuri zaidi, unataka kupata pesa nyingi, mahusiano mazuri au hata mahali pazuri pa kuishi. Msamaha unakusaidia kuyapata yote hayo.

Iwapo hutasamehe utajikuta ndani ya nafsi yako unajifunga katika mambo kama hasira, majuto, maumivu na kupata taabu mbalimbali na kwa hali hiyo ni kama mtu anayeendesha baiskeli ambayo imefungwa breki wakati wote na hivyo kupunguza mwendo, kukuchanganya kiakili na hivyo kushindwa kuendelea mbele.

Iwapo hutajifunza kusamehe ili kujinufaisha, basi jifunze kusamehe wengine. Jinsi utakavyozidi kujifunza kusamehe wengine ndivyo ambavyo utanufaika na wale wote uliowasamehe.

Fikra zako zitakuwa sahihi na zenye mtizamo chanya kuliko ilivyokuwa awali. Utajikuta unajitoa kwa wengine na pia kuwa na utayari kuchangia ulichonacho.

Utajikuta pia unakuwa mpole, mkarimu, na mwenye kujali wengine bila kujiuliza au kutumia muda kufanya maamuzi, utakuwa na furaha na mambo mengine mazuri zaidi na pia utaishi vizuri na wenzako na wao pia watakuwa na mapokeo mazuri kwako.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles