Nguli wa soka Marekani jela kwa kubaka wanawake 16

Darren Sharper
Darren Sharper
Darren Sharper

NEW YORK, Marekani

NYOTA wa soka wa zamani wa nchini Marekani, Darren Sharper, amehukumiwa kifungo cha miaka 18 jela kwa kukutwa na hatia ya kubaka  wanawake 16 tofauti katika majimbo mbalimbali nchini humo.

Sharper ambaye aliwahi kucheza katika timu ya New Orleans Saints, alihukumiwa mara mbili baada ya kutuhumiwa kufanya vitendo hivyo na waendesha mashtaka hayo kupendekeza kupewa adhabu hiyo.

“Napenda kuomba radhi zaidi kwa maelfu kutokana na kitendo nilichofanya,” alisema Sharper baada ya kupokea hukumu hiyo na kuongeza kwamba bado anafikiria ni kwa namna gani alifanya makosa hayo.

Lakini mmoja wa walioathirika na kitendo hicho, alisikika akisema kwamba mwanasoka huyo hastahili kusamehewa kutokana na wingi wa wanawake aliowatendea kitendo hicho ambacho hakifai kutokea katika jamii.

Jaji Jane Triche Milazzo akitoa adhabu kwa Sharper alisema: “Hatuwezi kupuuza uharibifu uliofanywa kwa wanawake na jamii kwa ujumla.”

Hata hivyo, Sharper alikiri mbele ya Mahakama ya Shirikisho ya jiji la New Orleans kwamba aliwalaghai wanawake watatu ili aweze kuwabaka.

Pia alikiri kufanya vitendo hivyo wakati akisomewa mashtaka katika Mahakama za Serikali za jiji la Louisiana, Arizona, California na Nevada.

Nguli huyo aliyecheza soka kwa miaka 14 na kumaliza soka lake mwaka 2011, pia aliwahi kucheza katika timu ya Bay Packers na Minnesota Vikings ya nchini humo.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here