NGORONGORO HEROES MFALME CECAFA

0
659

NA MOHAMED KASSARA-DAR ES SALAAM

TIMU ya Taifa ya vijana walio na umri chini ya miaka 20 ‘Ngorongoro Heroes’,  imetwaa ubingwa wa michuano ya Chalenji ya  Baraza la Vyama vya Soka kwa Nchi za Afrika Mashariki na Kati (Cecafa), baada ya jana kuichapa Kenya bao 1-0,  katika mchezo wa fainali uliochezwa Uwanja Njelu, Jinja nchini Uganda.

Bao la kujifunga la beki wa Kenya, Onyango Otieno dakika ya 45,  lilitosha kuipa Ngorongoro ufalme wa soka wa Cecafa kwa vijana.

Ilikotokea

Ngorongoro ilipangwa kundi moja la B katika michuano hiyo, ikiwa pamoja na Kenya.

Katika mchezo wa hatua ya makundi, timu hizo zilifungana mabao 2-2.

Ngorongoro inayonolewa na kocha Zuberi Katwila ilimaliza nafasi ya pili  kwenye kundi lake, nyuma ya vinara  Kenya waliokamata usukani kutokana na kuwa na wastani mzuri wa mabao ya kufunga na kufungwa.

Robo fainali, Ngorongoro iliivaana na wenyeji Uganda na kuibuka na ushindi wa mabao 4-2 kabla ya kutinga nusu fainali ambko huko ilikutana na Sudan na kuilaza mabao 2-0.

Mbali ya kutwaa ubingwa, Ngorongoro imeweka  rekodi ya kumaliza michuano hiyo bila kupoteza mchezo, ikianza kuichapa  Ethiopia mabao 4-0, ikalazimishwa sare ya mabao 2-2 na Kenya, kabla ya kufunga hatua ya makundi kwa kuishushia kipigo cha mabao 5-0, ndugu zao wa Zanzibar ‘Karume Boys’.

Kenya kwa upande wake Kenya, ilizindua kampeni zake kwa kuidungua Zanzibar mabao 5-0, ikatoka sare ya mabao 2-2 na Ngorongoro, kabla ya kufunga hatua ya makundi kwa  kuichakaza Ethiopia mabao 5-0.

Nusu fainali, Kenya  iliumana na Eritrea na kuibuka na ushindi wa bao 1-0 ulioipeleka fainali.

Akizungumza mchezo wa jana, Katwila alisema kikosi chake kilistahili  kutwaa ubingwa huo kutokana na kusheheni wachezaji wenye vipaji vya juu na wapambanaji.

“Tangu mwanzo tulikuwa na malengo letu  na si mengine zaidi ya kupambana ili tuweze kutwaa ubingwa wa mashindano hayo, namshukuru Mungu tumetimiza,”alisema Katwila.

Kikosi cha Ngorongoro kinatarajia kurejea nchini kuanzia leo.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here