Matukio muhimu yakukumbukwa Yanga Vs Polisi Tanzania

0
841

NA WINFRIDA MTOI

KATIKATI ya wiki lilishuhudiwa pambano la kukata na shoka la Ligi Kuu Tanzania Bara  kati ya Yanga dhidi ya Polisi Tanzania.

Mchezo huo ulimalizika kwa sare ya mabao 3-3.

Mchezo huo uliochezwa Uwanja wa Uhuru jijini Dar es Salaam, ulishudiwa na mashabiki wa wastani.

Matokeo hayo yalizidi kuiweka kwenye wakati mgumu Yanga.

Ilikuwa mechi ya pili ya Ligi Kuu msimu huu kwa Wanajangwani hao, waliokuwa wanashiriki Ligi ya Mabingwa Afrika kabla ya kutupwa nje wakiwa raundi ya kwanza.

Mchezo wa kwanza,  Yanga iliumana na Ruvu Shooting na kufungwa bao 1-0, mchezo ambao pia ulichezwa Uwanja wa Uhuru.

Matokeo hayo yanaifanya Yanga kuendelea kusalia  katika nafasi za chini kwenye msimamo wa ligi hiyo, kutokana na kuambulia pointi moja pekee huku watani zao Simba wakiwa kileleni na pointi 12, baada ya kucheza mechi nne, wakishinda zote.

Mechi hiyo ambayo ilikua ya pili kwa Yanga kukutana na Polisi Tanzania katika kipindi cha mwezi mmoja, baada ya ile ya kirafiki ya kujiandaa na msimu mpya iliyochezwa Uwanja wa Ushirika mjini Moshi mkoani Kilimanjaro, ambapo miamba hiyo ya Jangwani ilichapwa mabao 2-0.

MTANZANIA linakuletea baadhi ya matukio muhimu yaliyojili katika mchezo huo, ambao Kocha Mkuu wa Yanga, Mwinyi Zahera, aliushuhudia akiwa jukwaani kutokana na kutumia adhabu ya kufungiwa mechi tatu na Shirikisho la Soka Tanzania (TFF).

Mfungaji wa ‘hat trick’ akosa mpira

Katika mchezo huo,  mshambuliaji Ditram Nchimbi alitakata vilivyo, baada ya kuifungia Polisi mabao matatu ‘hat trick’.

Hat hivyo aliishia kupiga picha na mpira kisha ukarudishwa kwa wahusika kwa madai kwamba TFF atapatiwa mwingine.

Nchimbi alifunga mabao hayo, dakika za 34, 55, 58  na kuiwezesha timu yake kuondoka na pointi moja muhimu ugenini.

 Kitendo hicho cha kutopewa mipira baada ya mechi  kwa wachezaji  wanapofunga  hat trick, kimejirudia kwani msimu uliopita Alex Kitenge wa Stand United, alifunga  mabao kama hayo dhidi ya Yanga, Uwanja wa Taifa, lakini hakupewa mpira.

Molinga athibitisha ubora wake

Mshambuliaji wa Yanga, raia wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo(DRC), David Molinga, alidhihirisha ubora wake, baada ya kuiokoa timu yake na aibu ya kufungwa nyumbani.

Katika mchezo huo mshambuliaji huyo alifunga  mabao mawili kipindi cha pili.

Molinga ambaye bado hajaaminiwa na wapenzi wa timu hiyo, alionyesha ubora wake akianza kufunga kwa kichwa bao pili dakika ya 65, wakati  Polisi tayari walikuwa mbele  kwa mabao matatu, lakini hakushangilia.

Straika huyo aliendelea kupambana na dakika ya 68, akapiga mpira wa adhabu uliokwenda moja kwa moja nyavuni, ndipo alishangilia akielea kwa mashabiki wa Yanga huku akijipiga kifuani.

Zahera akiona cha moto

Kitendo cha kusuasua kwa timu hiyo kikosi chake kuonekana kucheza chini ya kiwango hasa washambualiaji wakigeni, Juma Balinya na Sadney Urikhob, kiliwafanya mashabiki wa Yanga kuanza  kumpigia kelele kocha wao Mwinyi Zahera aliyekuwa jukwaani  wakimtaka awatoe wachezaji hao.

Hali hiyo ilimfanya Zahera asijue cha kufanya na baada ya timu kwenda mapumziko, hakurejea tena sehemu aliyokuwa amekaa kuepuka kelele za mashabiki, hata mwisho wa mchezo hakutaka kuongelea chochote.

Juma Abdul avunja ukimya

Beki Juma Abdul ambaye alikosekana katika michezo mingi iliyopita kutokana na kusumbuliwa na majeraha huku nafasi yake kwa muda mrefu ikichezwa na Paul Godfrey, alionekana kurejea kwa kasi akichangia kupatikana kwa mabao mawili.

Licha ya kikosi hicho kuonekana kutocheza soka la kuvutia, lakini kwa mchezaji mmoja mmoja Juma Abdul alifanya kazi kubwa iliyowavutia wapenzi wengi wa Yanga ambao walikuwa wamemkosa kwa muda mrefu.

Mashabiki wakinukisha  

Kama ilivyo kawaida ya mashabiki wa Yanga na Simba kukosa uvumilivu, katika mchezo huo iliibuka taflani ya mashabikikupigana wenyewe kwa wenyewe.

Mtafaruku huo ulitokana na pande mbili kutofautiana kimtizamo, wale wanaomkubali
Zahera na wenzao wanaompinga.

Mashabiki wachache walishuhudia mchezo huo, lakini timbwili lake lilikuwa kubwa, kwani walikwenda uwanjani wakiwa na  matarajio ya kuondoka na pointi tatu, kutokana na timu yao kuonekana kuimarika katika mechi za Ligi ya Mabingwa walizocheza ikiwemo dhidi ya  Zesco United ya Zambia.

Mashabiki hao waliondoka na hasira, huku wakimtupia lawamaZahera kwa kushindwa kupanga vizuri kikosi chake.

Walisikika wakisema wamechoka kunyanyaswa na Selemani Matola tangu akiwa Lipuli na sasa Polisi Tanzania.

Ulinzi kila kona

Kutokana na uwepo wa Mkuu wa Jeshi la Polisi Tanzania (IGP), Simon Sirro, aliyefika kuisapoti timu yake, ulinzi ulikuwa mkali uwanjani hapo tofauti na mechi nyingine.

 Polisi walionekana kuimarisha ulinzi.

Hali hiyo ilichangia kuwatuliza mashabiki wa Yanga, waliokuwa wakilalamikia matokeo waliyopata na hata wachezaji walipotoka kwenda kupanda basi lao, hakuna shabiki aliyejaribu kuwasogelea na kuwasumbua.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here