24.4 C
Dar es Salaam
Sunday, October 13, 2024

Contact us: [email protected]

NGORONGORO HEROES CHAPA HAO DR CONGO

Na MOHAMED KASSARA -DAR ES SALAAM


TIMU ya  Taifa ya vijana walio na  umri wa miaka 20 ‘Ngorongoro Heroes’, leo itashuka dimbani kuumana na Jamhuri ya Kidemokrasia ya  Kongo (DRC) katika mchezo wa kuwania kufuzu fainali za mataifa Afrika za  vijana utakaochezwa Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.

Fainali za Mataifa ya Afrika za vijana zitafanyika Novemba mwaka huu nchini Niger.

Ngorongoro Heroes itaingia kwenye mchezo huo ikiwa inajiamini baada ya kuvuna ushindi katika michezo yake miwili ya kimataifa ya kirafiki ya hivi kaibuni.

Ngorongoro ilicheza pambano lake la kwanza la kujipima nguvu dhidi ya timu ya taifa ya vijana ya Morocco na kushinda bao 1-0     kabla ya kuichapa Msumbiji mabao 2-1, michezo yote ikipigwa Uwanja wa Uhuru, Dar es Salaam.

Lakini ili kuipiga DRC leo,    Ngorongoro ambayo inaundwa na wachezaji wengi waliong’ara  katika fainali za mataifa ya Afrika za vijana walio na umri chini ya miaka 17         wakiwa na kikosi cha Serengeti Boys, italazimika kupambana kufa au kupona ili kuibuka na ushindi.

Wachezaji hao wamekuwa pamoja kwa kipindi cha mwaka mmoja ambapo hadi sasa wameshacheza jumla ya mechi 30 za kimashindano na kirafiki.

Kikosi cha DRC kitakachoivaa Ngorongoro kimetoka kushiriki michuano ya Baraza la Soka Ukanda wa Kusini mwa Afrika (Cosafa) na kumaliza katika  nafasi ya tatu,    hii ina maana kwamba wachezaji wake bado wako vizuri kisaikolojia.

Pia kikosi cha DRC kinaundwa na baadhi ya wachezaji wanaocheza soka la kulipwa nje ya Bara la Afrika, wakiongozwa na nahodha Ismael Lukokingedi anayekipiga katika timu ya vijana ya KRC Genk ya Ubelgiji.

Mazingira  haya yanaufanya mchezo wa leo kutotabirika matokeo yake kirahisi zaidi ya ukweli kwamba, unatarajiwa kuwa na ushindani wa hali ya juu.

Akizungumza katika mkutano na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam jana, kocha mkuu wa Ngorongoro Heroes, Ammy Ninje, alisema kikosi chake kipo tayari kwa mapambano na kuibuka na ushindi ili kuwapa raha maelfu ya Watanzania ambao wamekuwa wakiwaunga mkono.

“Morali ya wachezaji iko juu, vijana wana njaa ya kutaka kufanikiwa,  nimekuwa nao kwa kipindi kifupi lakini wamenionyesha kuwa kuna jambo wanalitaka.

“Hatuna hofu na ukubwa wa miili ya wachezaji wao, nimewaambia vijana wangu namna ya kucheza nao, tunataka kuhakikisha tunaimaliza mechi hii hapa hapa nyumbani kabla ya kwenda ugenini, tutatumia mbinu kama zilizotumiwa kaka zao     (Stars) kuimaliza DRC wiki iliyopita,”     alisema Ninje.

“Jambo la msingi na muhimu,    nawaomba Watanzania wajitokeze kwa wingi uwanjani kesho     (leo)   kuwasapoti wachezaji naamini hatutawaangusha.”

Kwa upande wake, nahodha wa DRC,  Ismael Lukokingedi, alisema wataingia uwanjani kwa tahadhari wakilenga kuepuka kupoteza mchezo kama ilivyotokea kwa kaka zao walipokumbana cha mabao 2-0 kutoka kwa Stars.

“Tunajua hautakuwa mchezo mwepesi, Tanzania ina wachezaji wengi wenye vipaji, tuna heshimu hilo,    tumejiandaa vema kwa ajili ya kuhakikisha tunapata matokeo mazuri hapa kabla ya kwenda kumaliza kazi nyumbani,” alisema Ismael.

Viingilio vya mchezo huo ni Sh1000 kwa mzunguko na  Sh 3,000 kwa jukwaa maalum(VIP ), utachezeshwa na mwamuzi Willam Uloyo kutoka Uganda).

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
590,000SubscribersSubscribe

Latest Articles