22.2 C
Dar es Salaam
Monday, October 14, 2024

Contact us: [email protected]

AZAM VS MTIBWA KAZI IPO LEO, STAND UNITED YATANGULIA NUSU FAINALI

Na MOHAMED KASSARA -DAR ES SALAAM


AZAM FC itakuwa mwenyeji wa  Mtibwa Sugar leo kwa kuumana katika mchezo wa robo fainali ya michuano ya Kombe la Shirikisho la Azam, utakaochezwa Uwanja wa Azam Complex, Dar es Salaam.

Azam ilitinga hatua hiyo baada ya kuiondoa mashindanoni  KMC mabao 3-1, katika mchezo wa hatua ya 16 bora uliochezwa Uwanja wa Azam Complex, Dar es Salaam.

Wapinzani wao Mtibwa    imefika  hatua hiyo baada ya kuing’oa timu ya     Buseresere ya Geita kwa kuichapa mabao 3-0, katika mchezo wa hatua ya 16 bora uliochezwa Uwanja wa Nyamagana, Mwanza.

Mara ya mwisho timu hizo zilikutana Novemba 27, mwaka jana katika mchezo wa Ligi Kuu Tanzania Bara uliochezwa kwenye uwanja huo   ambapo matokeo yalikuwa sare ya bao 1-1.

Azam itajitupa dimbani pasipo wakali wake watatu kutokana na kuwa majeruhi,  mabeki Mohamed Yakubu na Daniel Amoah pamoja na mshambuliaji Wazir Junior.

Kwa upande wa Mtibwa,  itawakosa mabeki wao Issa Rashid ‘Baba Ubaya’ na Salum Kanoni wanaosumbuliwa na majeraha ya goti.

Akizungumza na MTANZANIA jana, Kocha Mkuu wa Mtibwa, Zuber Katwila, alisema kuelekea pambano hilo amekiandaa kikosi chake kucheza mchezo wa kushambulia zaidi akiamini itamsaidia kuvuna ushindi.

“Ni mchezo wa matokeo lazima tujitahidi kutumia nafasi, nimejipanga kwa lolote kuhakikisha tunapata ushindi na kusonga mbele, wachezaji wangu wana uzoefu wa kutosha, sina haja ya kuhofia kucheza usiku,”   alisema Katwila.

Kocha msaidizi wa Azam, Iddi Nassoro ‘Cheche’, akizungumzia maandalizi ya mchezo huo, alisema wamejiandaa kuhakikisha wanatumia vizuri faida ya kucheza nyumbani.

“Hii ni michuano migumu zaidi  na kwa    vile hakuna nafasi ya kujirekebisha unapokosea, lazima uwe na mpango sahihi wa kuhakikisha unapata ushindi ili kuvuka kwenda hatua nyingine,” alisema Cheche.

Katika mchezo mwingine, Tanzania Prisons itaikaribisha JKT Tanzania kwa kuumana nayo kwenye Uwanja wa Sokoine, Mbeya.

Prisons ilichumpa hatua hiyo baada ya kuiondosha mashindanoni Kiluvya United kwa kuichapa penalti 5-4 katika mchezo wa hatua ya 16 bora uliochezwa Uwanja wa Sokoine, Mbeya.

JKT Tanzania ilifuzu robo fainali baada ya kuifurusha Ndanda FC kwa kuichapa bao 1-0 kwenye Uwanja wa Meja Jenerali Isamuhyo, Dar es Salaam.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
590,000SubscribersSubscribe

Latest Articles