24.4 C
Dar es Salaam
Sunday, October 13, 2024

Contact us: [email protected]

BOMBARDIER YAACHIWA

Na MWANDISHI WETU – DAR ES SALAAM


HATIMAYE ndege mpya ya Shirika la Ndege Tanzania (ATCL) iliyokuwa inashikiliwa nchini Canada imeachiwa.

Kwa mujibu wa taarifa ambayo Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais-Ikulu, Gerson Msigwa, aliandika jana katika akaunti yake ya mtandao wa kijamii wa Twitter, ilifafanua kwamba ndege hiyo aina ya Bombardier Q400 imeshaachiwa na tayari imeondoka nchini humo.

Pasipo kutaja siku iliyoachiwa na kuondoka nchini humo, Msigwa, alifafanua katika taarifa yake kwamba ndege hiyo iko njiani kuja nchini.

Pia alisema kwamba ndege nyingine tatu, Bomberdier CS 300, mbili kutoka Canada pamoja na Boeing 787-8 Dreamliner kutoka Marekani zitawasili hapa nchini baadaye mwaka huu na alimalizia ujumbe wake kwa kuwatakia Watanzania Ijumaa Kuu njema.

Taarifa za kushikiliwa kwa ndege hiyo kwa mara ya kwanza zilitolewa na Mwanasheria Mkuu wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Tundu Lissu, katika mkutano wake na waandishi wa habari uliofanyika Agosti 18, mwaka jana Dar es Salaam na alisema moja kati ya ndege aina ya Bombadier Dash Q400 imeshikiliwa Canada na kampuni moja ya ujenzi ya Stirling Civil Engineering Ltd.

Lissu alidai kwamba, sababu za kushikiliwa kwa ndege hiyo ni kutokana na Serikali kudaiwa Dola milioni 38 za Marekani (Sh bilioni 87) na kwamba kampuni hiyo ilitishia kuipiga ‘mnada’ ndege hiyo ili kufidia deni hilo ikiwa Serikali haitalipa.

Alisema ndege hiyo ni ile ambayo kwa mujibu wa Serikali ilitakiwa kuwasili hapa nchini Julai, mwaka jana.

Lissu ambaye pia ni Mbunge wa Singida Mashariki, alisema mwaka 2009 kampuni hiyo ilipewa kandarasi ya kutengeneza Barabara ya Wazo Hill–Bagamoyo.

Alisema kabla ya kukamilisha ujenzi huo, Serikali ilivunja mkataba bila kuzingatia makubaliano na kuinyang’anya kampuni hiyo zabuni na kuagiza kutimuliwa nchini.

Pia alisema kampuni hiyo ilifungua kesi katika Mahakama ya Kimataifa ya Usuluhishi jijini Paris na kuishinda Serikali ya Tanzania.

Kwa mujibu wa Lissu, uamuzi wa mahakama uliitaka Serikali kuilipa takribani Dola milioni 25 za Marekani (Sh bilioni 40 kwa wakati huo).

Lissu alisema deni hilo halikulipwa kwa wakati na Juni, mwaka jana lilifikia Dola milioni 38 za Marekani.

Alisema baada ya kampuni hiyo kuona hailipwi fedha zake iliomba kibali cha mahakama kukamata mali za Tanzania.

Siku mbili baada ya Lissu kutoa taarifa hiyo, Serikali kupitia kwa Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa Idara ya Habari (Maelezo) na Msemaji Mkuu wa Serikali, Zamaradi Kawawa, ilithibitisha kushikiliwa kwa ndege hiyo.

Pamoja na Serikali kukiri kudaiwa lakini iliwatuhumu wanasiasa kutengeneza mgogoro.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
590,000SubscribersSubscribe

Latest Articles