23.4 C
Dar es Salaam
Saturday, April 27, 2024

Contact us: [email protected]

NGOMA KAFANYA YAKE MASHABIKI FANYENI YENU

Na ADAM MKWEPU-DAR ES SALAAM


SUBIRA ipo kwa wanaoamini tu. Subira na uvumilivu ni vitu ambavyo hata katika vitabu vya dini vimetajwa kwa wale wenye imani na hofu ya Mungu.

Kuna wakati mashabiki wa soka hawana tofauti na wagonjwa wa akili pindi linapokuja suala la timu au mchezaji kufanya vibaya ndani ya uwanja.

Kutokana na tabia hiyo, mashabiki wa timu ya Yanga hawaoni tatizo hata kama  mshambuliaji wao, Donald Ngoma, akifukuzwa kwa sababu tu hakuwapo katika michezo mikubwa ambayo wamepoteza huku pengo lake likionekana wazi.

Yanga imemkosa Ngoma katika michezo kadhaa ya Ligi Kuu Tanzania Bara ukiwamo wa Simba ambao walifungwa mabao 2-1 huku Ngoma akiwa jukwaani kutokana na maumivu ya goti aliyopata katika mchezo wa JKT Ruvu.

Ngoma amekuwa akilalamika kusumbuliwa na maumivu makali ya goti kwa muda mrefu, lakini ripoti ya madaktari wa klabu hiyo mara kadhaa imeonekana kukanganya mashabiki.

Ipo ripoti iliyodai kuwa mchezaji huyo alikuwa mzima kabla ya mchezo dhidi ya Simba licha ya mwenyewe kudai kuwa bado hali yake ilikuwa mbaya kucheza mchezo huo.

Lakini kwa kile kilichoonekana katika mchezo wa Ligi ya Mabingwa Afrika dhidi ya Zanaco, ni dhahiri kwamba Ngoma bado ni mgonjwa wa goti.

Kwa inavyoonekana tatizo hilo lilifahamika hata kwa wapinzani ndio maana katika mchezo dhidi ya Zanaco walikuwa wakimwandama sana mshambuliaji huyo ambaye baadaye hali ilikuwa mbaya na kutolewa.

Kwani hata alipotolewa nje hali yake iliendelea kuwa mbaya zaidi na kulazimika kupelekwa ndani kwa matibabu ya dharura, huku akisaidiwa kutembea na madaktari wa timu hiyo.

Yupo daktari mmoja aliwahi kusema kuwa wachezaji wengi wa timu kubwa za Simba, Yanga na Azam FC wanasumbuliwa na ugonjwa wa muda mrefu wa goti.

Daktari huyo alienda mbali na kudai kuwa ugonjwa huo unachukua muda mrefu kupona, hivyo wachezaji wengi huogopa kupoteza nafasi zao uwanjani ndio sababu ya kuwa tayari kucheza hata kama wakiwa wagonjwa.

Wapo wanaochomwa sindano ilmradi wasiache kucheza, lakini jambo hilo lipo tofauti kabisa katika kichwa cha Ngoma ambaye hakuwa tayari kufanya kitendo hicho ili acheze mchezo dhidi ya Simba.

Hakuna ubishi kwamba ukimtaja Ngoma utakuwa ukimtaja mshambuliaji hatari wa timu ya Yanga kwa kipindi hiki ambacho Obrey Chirwa amebeba majukumu mazito ya kuiweka safu hiyo kwenye mabega yake.

Ngoma ndiye mshambuliaji aliyewapa Yanga jeuri ya kunyakuwa ubingwa wa ligi hiyo misimu miwili mfululizo, huku akiwanyamazisha wapinzani wao wa jadi Simba kwa kuwafunga mara zote katika michezo ya Ligi Kuu misimu hiyo.

Ngoma kafanya aliyotakiwa kufanya akiwa katika afya njema na kiwango bora ndani ya kikosi cha Yanga, hivyo ni wakati wa mashabiki wa timu hiyo kumsikiliza.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles