27.5 C
Dar es Salaam
Tuesday, February 7, 2023

Contact us: [email protected]

MAYANGA UMETUDANGANYA KWA KESSY TAIFA STARS

WIKI iliyopita kocha mkuu wa timu ya soka ya Tanzania Bara ‘Taifa Stars’, alitangaza kikosi cha wacheza 26 kwa maandalizi ya michezo ya kufuzu michuano ya ubingwa wa Mataifa ya Afrika (CHAN) na Kombe la Mataifa ya Afrika (Afcon). 

Stars itaanza na Rwanda katika kuwania tiketi ya Chan mwakani nchini Kenya na mechi ya kwanza itachezwa Uwanja wa Taifa mjini Dar es Salaam kati ya Julai 14 na 16 kabla ya timu hizo kurudiana Uwanja wa Amahoro, Kigali kati ya Julai 21 na 23, iwapo kama itafanikiwa kuitoa Rwanda itakwenda kumenyana na mshindi kati ya Uganda, Sudan Kusini au Somalia katika raundi ya tatu ya mchujo, mchezo utakaochezwa kati ya Agosti 11 hadi 13, huku marudiano yakiwa Agosti kati ya 18 hadi 20 mwaka huu.

Pongezi kwa Mayanga kwa kufanya uteuzi ulioonekana angalau kukidhi kiu ya Watanzania wengi, baada ya kuwapa nafasi chipukizi Yussuf na Abdulrahman Juma waliotoka nje ya Simba, Yanga na Azam kutokana na siku za hivi karibuni Stars kuonekana ni ya Dar es Salaam pekee.

Wakati zikitolewa pongezi hizo, Kiroho safi ina shaka juu ya uteuzi wa nafasi ya beki wa kulia ambao umewapa Shomari Kapombe na Hassan Ramadhan ‘Kessy’.

Sipingani na uteuzi wako kwa kuwa wewe ndiye kocha, lakini nina mashaka na wale uliowapa dhamana katika nafasi hiyo hasa ukizingatia Tanzania tunahitaji ushindi katika michezo yetu na si watu wanaokwenda kupiga ‘selfie’ nje ya mipaka na kushindwa kutimiza majukumu yao.

Huenda Kapombe umempa nafasi kutokana na ukongwe wake wa mashindano ya kimataifa, lakini kwa upande wa Kessy je?

Kessy ambaye hivi karibuni ndio amepata nafasi ya kucheza ndani ya timu yake ya Yanga, baada ya Juma Abdul kuwa na jeraha la goti, ameichezea michezo mitatu pekee dhidi ya Mtibwa Sugar, nyingine ni ile ya Kombe la FA dhidi ya Kiluvya United na mwisho ikiwa ni ya klabu bingwa dhidi ya Zanaco.

Katika michezo hiyo tukitoa unafiki ni kweli Kessy alionekana kucheza katika kiwango cha juu, kiasi cha kuamini huenda hivi karibuni atarejea katika kile kiwango alichoonekana nacho kipindi akiwa Simba, lakini ukweli lazima usemwe kuwa hakuwa na kiwango kama cha Juma Abdul aliyeonekana moja wa mabeki wa kulia bora Tanzania kutokana na uwezo wake wa kuzuia mawinga wasumbufu, kukokota mpira kwa spidi na kusaidia mashambulizi kwenye lango la adui, kizuri zaidi ni uwezo wa kupiga krosi zenye macho.

Kumtaja Abdul sina maana kuwa Mayanga angempa nafasi, la hasha kwa kuwa inaeleweka wazi beki huyo anasumbuliwa na matatizo ya goti, lakini mbona hakumtaja Salum Kimenya na Michael Aidan.

Hivi unataka kutuambia kuwa Kimenya na Aidan waliocheza kwa ubora zaidi ya mechi tatu alizocheza Kessy, hawakuwa na viwango vya kuitwa Stars? Je, ni kwa kuwa hawachezi timu za Simba, Yanga na Azam?

Kessy ana kipi kikubwa mno kilichowazidi wengine ambacho kimesababisha kupewa nafasi, ni wazi  kwa hili Mayanga umetudanganya, kwani mechi tatu haziwezi kumbeba Kessy Stars na kuwaacha wengine walioonyesha uwezo mkubwa zaidi yake, labda kama kuna kitu nyuma ya pazia ambacho Watanzania hatukijui kuhusu uteuzi wake.

Acha tuone katika uteuzi huu, ukizingatia  mpira ni mchezo wa hadharani ila Mayanga kumbuka Watanzania tunahitaji ushindi pekee na si ushiriki kimataifa. 

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
208,885FollowersFollow
561,000SubscribersSubscribe

Latest Articles