23.3 C
Dar es Salaam
Friday, April 26, 2024

Contact us: [email protected]

NECTA RICHARD: Nataka kuwa mhandisi kuisaidia nchi yangu

Necta Richard
Necta Richard

Na Veronica Romwald, Dar es Salaam

WASICHANA wengi nchini wamekuwa wakiyaona masomo ya Sayansi kwamba ni magumu na mzigo mkubwa kwao hali inayotoa nafasi kwa wavulana kuyachangamkia.

Necta Richard ambaye ni mwanafunzi wa kidato cha pili katika Shule ya Sekondari Jangwani, ni miongoni mwa wasichana walioamua kuitikia wito wa kusoma masomo hayo.

Anasema amejipanga kuhakikisha anafikia ndoto yake ya kuwa mhandisi mkubwa wa baadae nchini pindi Mungu atakapomwezesha kuhitimu masomo yake.

MTANZANIA lilipata fursa ya kuzungumza na Necta punde baada ya kumaliza kuwasilisha hotuba mbele ya Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Ummy Mwalimu, wakati wa maadhimisho ya Siku ya Idadi ya Watu Duniani Julai 11, mwaka huu kwa niaba ya wanafunzi wenzake 150.

Necta anasema tangu akiwa mdogo amekuwa akitamani kuja kuwa mhandisi na alipoanza kusoma aliweka juhudi katika kujifunza masomo hayo ili kufikia ndoto yake.

Anasema kila siku amekuwa akijifunza kwa bidii na kuwasikiliza kwa makini walimu wake ili aweze kuwa na uelewa mpana zaidi.

“Nataka kuwa mhandisi mkubwa ili kuisaidia nchi yangu, nimepanga kusoma fani ya ‘Mechatronics’. Hii ni fani inayojumuisha mambo mawili kwa pamoja yaani ‘Mechanical na ‘Enginearing’ ambapo nitaweza kupata ujuzi wa vitu vingi kwa wakati mmoja kupitia fani hiyo nitaweza kujua namna ya kutengeneza magari, masuala ya umeme, kutengeneza vyuma na vitu mbalimbali vya aina hizo,” anasema.

Necta anasema wasichana wanapaswa kuachana na woga wa kusoma masomo ya sayansi kwa sababu kuna fursa nyingi za kujikomboa kichumi katika maisha yao ya baadae.

“Sijui kwanini wanaogopa na kuyakimbia masomo ya Sayansi, lakini hakuna jambo gumu, kikubwa ni kuwekeza katika kujifunza ili kujijengea msingi mzuri wa baadae kwa sababu masomo haya usipoweka msingi hapa awali huko mbele lazima utayaona magumu kwako.

“Nimeambiwa wasichana wengi wanaikimbia fani hii ya ‘Mechatronics’, ndio maana wanaofanikiwa kumaliza ni wanaume peke yao, mimi nataka nivunje rekodi hiyo ya kuwa msichana wa kwanza kusoma fani hiyo,” anasema kwa kujiamini.

Anasema anataka kuvunja rekodi hiyo na kuwa msichana wa kwanza kusoma fani hiyo kwani licha ya wavulana kuisoma hata hivyo bado kuna wataalamu wachache nchini.

“Kwa msingi huo utaona namna ambavyo fani hii ina fursa nyingi za ajira. Nawashauri wasichana wenzangu wasiyakimbie masomo ya sayansi bali wayapende na kutia juhudi ya kujifunza ili waje kujikomboa kiuchumi hapo baadae,” anasema.

Pamoja na hayo, Necta anasema wazazi wana jukumu kubwa la kuhakikisha wanawasaidia watoto wao hasa wa kike katika kukabiliana na changamoto mbalimabali wanazokumbana nazo kila siku.

“Mtoto wa kike anakabiliwa na changamoto nyingi kuliko mtoto wa kiume na hili lipo wazi, kwa mfano kuna suala la unyanyasaji wa kijinsia, ukeketaji, ndoa na mimba za utotoni ambazo kiukweli imekuwa ikiwafanya wengi washindwe kutimiza ndoto zao.

“Hivyo wazazi wana jukumu kubwa la kuhakikisha wanawalinda watoto wa kike dhidi ya unyanyasaji wa kila aina ili wafikie malengo yao kama ilivyo kwa watoto wa kiume, serikali nayo inapaswa iweke mazingira rafiki kwa watoto wa kike na kuweka sheria za kuwalinda,” anasema.

Anasema serikali inapaswa kukomesha na kuziondoa kabisa mila potofu dhidi ya mtoto wa kike ambazo zimekuwa zikikandamiza haki zao za msingi.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles