25.2 C
Dar es Salaam
Friday, April 26, 2024

Contact us: [email protected]

Mazoezi ya kuogelea huchangamsha akili

Watoto wakiogelea.
Watoto wakiogelea.

Na Maneno Selanyika, Dar es Salaam

MCHEZO wa kuogelea una historia ndefu tangu enzi za mababu ingawa huko Ulaya unaaminika ulianza mwaka 1800.

Kanuni mojawapo ya kuogelea ni kwamba mwogeleaji anatakiwa kuogelea huku ukielekea kwenye maji.

Kwa kuwa uogeleaji ni mchezo kama ilivyo mingine, wataalamu wa afya wanasema faida yake ni kubwa kwani licha ya kusaidia kujikinga na maradhi pia humfanya mtu kuwa mchangamfu siku zote.

Upo ukweli kwamba mtu asiposhiriki mazoezi mara kwa mara anaweza kupatwa na magonjwa kutokana na mwili kuwa dhoofu mwishowe hushindwa kupambana na vijidudu vinavyoingia mwilini ambavyo ndio vinasababisha ugonjwa kutokea.

Mbali na kuogelea michezo mingine ambayo humfanya mtu kuwa na mwili imara ni kukimbia, kucheza mpira wa aina yoyote na mengineyo.

Mwanafunzi Fransisca Soka (12) kutoka shule ya Sekondari Chalote iliyopo mkoani Morogoro, ni miongoni mwa watu wanaoamini kwamba mazoezi ya kuogelea yana faida kubwa hasa kuchangamsha akili na kupata ajira.

Fransisca ambaye ni mwanafunzi wa kidato cha kwanza alikutana na MTANZANIA wiki iliyopita maeneo ya Sinza, ambapo alikuwa yupo likizo.

Anasema alianza mazoezi ya kuogelea tangu akiwa na umri wa miaka saba alipokuwa darasa la pili.

Anasema kuna aina mbalimbali za uogeleaji ambazo hutumika katika mashindano ya Kimataifa ambayo huwashindanisha waogeleaji kama vile Backstrocke, Butterfly pamoja na Freestyle ambayo ndio mitindo mepesi.

“Uogeleaji ni mchezo kama ilivyo mingine japo serikali yetu bado haijaipa kipaumbele kutokana na sababu mbalimbali zikiwemo za ukosefu wa miundombinu ya mabwawa na vinginevyo,” anasema mwanafunzi huyo.

Anasema ana uwezo wa kuogelea katika maji yenye chumvi kama baharini, katika maziwa na hata kwenye mabwawa ambapo ana uwezo wa kuzama ndani ya maji kwa muda wa zaidi ya dakika 10 kama akiwa na vifaa vya kuogelea.

Anaishauri Serikali kujenga mabwawa ya maji katika shule mbalimbali ili kuwajengea mazingira wanafunzi wenye uwezo wa kuogelea wasipoteze vipaji vyao ambavyo vinaweza kuwaongezea vipato na taifa zima kwa ujumla.

Matarajio yake anasema ni kufanya kazi katika vyombo vya usafiri baharini na kwenye maziwa ili inapotokea ajali aweze kuokoa maisha ya wasafiri.

“Nawashauri wanafunzi wenzangu wanaopenda kuogelea wajitokeze wasiogope kwani ni michezo kama ilivyo mingine ambayo inaweza kuwapatia ajira na ongezeko la uchumi wao na jamii inayowazunguka.

“Wazazi ndio wenye mwongozo na kutambua vipaji vya watoto wao hivyo ni wajibu wao kuwatia moyo na si kuwavunja moyo,” anasema.

Mbali na mchezo huo pia Fransisca aliliambia gazeti hili kuwa yeye ni mtaalamu wa masomo mbalimbali mojawapo ni la Hisabati ambapo anasema hajawahi kupata alama chini ya B tangu alipokuwa shule ya msingi.

Anawataka wanafunzi wenzake kuacha kuogopa somo hilo na badala yake wawe wanafanya mazoezi mara kwa mara kwani ndio njia pekee ya kufaulu.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles