26.2 C
Dar es Salaam
Sunday, January 29, 2023

Contact us: [email protected]

NEC yarejesha wagombea ubunge 15

 MWANDISHI WETU -DAR ES SALAAM

TUME ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) imetoa uamuzi wa rufaa 55 za wagombea ubunge, huku ikiwarudisha wagombea 15 kuendelea na mchakato wa uchaguzi.

Wakati ikiwarejesha hao, tume hiyo imekataa rufaa 15 za wagombea wengine ambao hawakuteuliwa, huku ikigomea rufaa 25 za kupinga walioteuliwa.

Taarifa iliyotolewa kwa vyombo vya habari jana na kusainiwa na Mkurugenzi wa Uchaguzi NEC, Dk. Wilson Mahera, ilisema tume imechambua vielelezo, nyaraka na maelezo ya warufani na warufaniwa vilivyowasilishwa ili kuhakikisha haki inatendeka kwa mujibu wa sheria na kanuni za uchaguzi. 

“Tume ya Taifa ya Uchaguzi inaendelea kupitia, kuchambua na kuzifanyia uamuzi rufaa za wagombea ubunge zilizowasilishwa na wagombea kupitia kwa wasimamizi mbalimbali wa uchaguzi nchi nzima.

“Kifungu cha 40(6) cha Sheria ya Taifa ya Uchaguzi, sura ya 343, kinatoa fursa kwa wagombea wa ubunge kukata rufaa wanapokuwa hawajaridhika na uamuzi wa wasimamizi wa uchaguzi kutokana na pingamizi zilizowasilishwa.

“Uamuzi uliofanywa na tume katika rufaa hizi, umewarejesha baadhi ya warufani kwenye orodha ya wagombea. 

“Tume itaendelea kutoa matokeo baada ya usajili na uchambuzi wa rufaa hizo kuanzia leo (jana), kesho (leo) na kuendelea,” ilisema sehemu ya taarifa hiyo. 

Taarifa hiyo pia ilieleza kuwa wahusika wa rufaa hizo wameanza kujulishwa kwa barua kuhusu uamuzi wa tume kuanzia jana. 

“Zoezi la kuzijadili na kuzitolea uamuzi rufaa hizo linaendelea na kuanzia leo (jana), tume itakuwa inatoa uamuzi na kuwajulisha wahusika kwa kadiri rufaa hizo zitakavyokuwa zinamalizika kushughulikiwa. 

“Leo (jana) tume imetoa uamuzi wa rufaa 55 za wagombea ubunge ambapo imekubali rufaa 15 na kuwarejesha wagombea katika orodha ya wagombea. Imekataa rufaa 15 za wagombea ambao hawakuteuliwa, imekataa rufaa 25 za kupinga walioteuliwa. 

“Tume imechambua vielelezo, nyaraka na maelezo ya warufani na warufaniwa vilivyowasilishwa ili kuhakikisha kwamba haki inatendeka kwa mujibu wa sheria na kanuni za uchaguzi,” ilisema taarifa hiyo. 

Hadi sasa Chama Cha Mapinduzi (CCM) kimeshajikusanyia wabunge 20 waliotangazwa kukosa washindani kwenye majimbo yao, hivyo wanahesabika tayari ni washindi hata kabla ya kupigiwa kura na wananchi.

Wasimamizi wa uchaguzi kwenye maeneo hayo, walieleza sababu za wagombea hao wa vyama vya upinzani kuenguliwa ni kutokana na kutokukidhi matakwa ya kisheria na hivyo kuwaacha wa CCM wakiwa na sifa halali za kuwa wagombea.

Miongoni mwa wanasiasa mashuhuri waliopitishwa kwa mtindo huo, ni Waziri Mkuu Kassim Majaliwa wa Jimbo la Ruangwa, Nape Nnauye (Mtama), Spika wa Bunge, Job Ndugai (Kongwa) na Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Palamagamba Kabudi (Kilosa).

Kwenye orodha hiyo, wamo pia wafanyabiashara maarufu kama Ahmed Shabiby ambaye alitangazwa mshindi katika Jimbo la Gairo kwa kile ambacho msimamizi alisema ni “wagombea wengine kurudisha fomu saa 11 jioni badala ya saa 10 jioni”.

Mwingine ni Abdulaziz Aboud (Morogoro Mjini) kwa kile ambacho msimamizi alisema ni makosa kwenye fomu za wagombea wengine. 

Yumo pia meneja wa msanii Naseeb Abdul (Diamond Platnumz), Hamis Taletale ambaye naye alipita ubunge wa Jimbo la Morogoro Kusini Mashariki. 

Kutokana na hilo, mara kadhaa viongozi wakuu wa vyama vya upinzani wamekuwa wakieleza bayana kuwa wagombea wao wamechezewa rafu, huku wakitoa matamko ya kulaani.

Vyama ambavyo wagombea wake wa ubunge walienguliwa kutokana na sababu mbalimbali ni Chadema na ACT Wazalendo.

Kwa upande wa Chadema, wagombea wake wa ubunge pamoja na madiwani ni zaidi ya 1,000 ambao walikata rufaa kwenye tume hiyo.

CHADEMA

Akzungumzia hatua hiyo ya NEC, Meneja Habari na Mawasiliano wa Chadema, Tumaini Makene alisema tume ilitakiwa kueleza kwa uwazi kwa umma kuhusu majina ya wabunge ambao imetoa uamuzi wa rufaa zao badala ya kufanya kwa kificho kama ilivyofanyika. 

“Hawa tume wametoa uamuzi, haijulikani ni nani na nani ambao rufaa zao zimetolewa. Ni vema wangetaja hadharani kwa majina na majimbo ya wahusika ili iwe wazi kwa umma kuliko namna hii waliyofanya, wanasema tu idadi ya rufaa bila kutaja wahusika na vyama vyao.

“Sisi pia hadi muda huu tunaona tu kwenye mitandao ya kijamii kuhusu taarifa ya hatua hiyo ya tume ilipofikia, lakini hatujajua ni kina nani ambao rufaa zao zimeshapitiwa na kama wanatoka kwetu au vyama vingine. Tume iache kufanya mambo haya kwa kificho kificho namna hii, iwe wazi kwa umma,” alisema Makene.

Alisema kwa namna mambo yanavyoendeshwa na tume, inaweza kuonekana kama kuna mambo yaliyojificha.

“Tume inatakiwa kuwa wazi kuhusu utaratibu mzima uliotumika kufikia maamuzi kuhusu rufaa hizo, na kutaja wale ambao rufaa zao zimeshapitishwa, majina yao na vyama vyao hadharani,” alisisitiza Makene.

ACT WAZALENDO

Akizungumza na MTANZANIA Dar es Salaam jana kuhusu uamuzi huo wa NEC, Katibu Mkuu wa Chama cha ACT Wazalendo, Ado Shaibu, alisema utaratibu uliotumika una upungufu kwa sababu tume ingeweka kila kitu hadharani kwa sababu hilo ni suala la masilahi makubwa kwa umma.

Kuhusu idadi ya wagombea wao walioshinda rufaa hizo, alisema: “Tume inawasiliana moja kwa moja na wagombea. Hadi sasa hatujapata mawasiliano na mgombea hata mmoja aliyerejeshwa, tunaendelea kufuatilia,” alisema Shaibu.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
208,063FollowersFollow
561,000SubscribersSubscribe

Latest Articles