22.6 C
Dar es Salaam
Saturday, May 21, 2022

Balozi wa Ushelisheli aipongeza Osha kwa usimamizi mzuri wa sheria

Faraja Masinde -Dar es salaam

BALOZI wa Heshima wa Visiwa vya Ushelisheli nchini, Maryvonne Pool, ameipongeza Tanzania kwa hatua kubwa iliyofikiwa katika usimamizi wa sheria ya Afya na Usalama Mahali pa Kazi yenye lengo la kulinda nguvu kazi ya taifa.

Balozi Marvonne alitoa pongezi hizo jana jijini Dar es Salaam alipotembelea ofisi za Wakala wa Usalama na Afya Mahali pa Kazi kwa lengo kufanya usajili wa moja ya miradi ambayo ofisi yake ni mbia pamoja na kujifunza namna ambavyo taasisi ya OSHA inatekeleza majukumu yake.

Maryvonne alisema anatambua kazi nzuri  inayofanywa na OSHA katika kusimamia utekelezaji wa Sheria ya Afya na Usalama Mahali pa Kazi ya mwaka 2003 ambapo kupitia sheria hiyo maeneo mengi ya kazi yanatambulika na kuzingatia viwango vya usalama na afya kazini.

“Naipongeza Tanzania chini ya uongozi wa Rais Dk. John Magufili kwa kuwa na taasisi muhimu kama hii ambayo inasaidia kulinda nguvu kazi ya nchi na kimsingi nimekuwa nikiwasikia sana siku hizi na nafahamu jinsi mlivyojipanga katika kutekeleza majukumu yenu ya msingi,” alisema Balozi  Maryvonne.

Aidha, Balozi huyo aliahidi kushirikiana na OSHA katika kuviwezesha vikundi vya wakulima wadogo wanaofanya shughuli zao katika wilaya za pembezoni mwa mikoa ya Dar es Salaam na Pwani hususan kuhakikisha kwamba vikundi hivyo vinasajiliwa na OSHA kwa ajili ya kuendelea kupatiwa miongozo ya namna ya kujikinga na madhara yatokanayo na shughuli za kilimo.

“Sisi tunafanya miradi mbali mbali ya kuwawezesha wakulima kuboresha uzalishaji na kupata masoko ya mazao ya kilimo na japokuwa tumekuwa tukiwawezesha wakulima kupata vifaa muhimu vya kujikinga kama vile viatu vya shambani (Gunboots) lakini tunaona ipo haja ya kuwahamasisha wakulima kuwa katika vikundi vya uzalishaji na kuwawezesha kupata usajili wa OSHA ili muendelee kuwaongoza kufanya kazi zao kwa usalama zaidi,” alisema Maryvonne.

Kwa upande wake, Kaimu Mtendaji Mkuu wa OSHA, Khadija Mwenda, alisema Taasisi yake imefarijika kutambua kwamba juhudi za serikali za kulinda nguvukazi ya Taifa zinaonekana.

“Tumefurahi sana leo kutembelewa na Balozi wa Heshima wa Ushelisheli hapa nchini kwetu ambaye amekuja kusajili eneo lake la kazi, tumepata fursa ya kushirikishina mambo mengi na kubadilishana uzoefu jinsi ambavyo nchi zetu zinasimamia masuala ya afya na usalama ambapo amefurahi sana kuona kwamba nchi yetu ina mfumo madhubuti wa kusimamia usalama na afya ili kulinda nguvu kazi ya Taifa,” alisema Mwenda.  

Katika ziara yake Balozi huyo alifanikiwa kusajili mradi ambao ofisi yake ni mbia na kupatiwa cheti cha usajili papo hapo, aidha, alipata fursa ya kubadilishana uzoefu na Mtendaji Mkuu wa OSHA kuhusu mifumo ya usimamizi wa masuala ya Usalama na Afya baina ya Tanzania na Visiwa vya Ushelisheli ambapo alieleza kuwa nchi yake ina sheria kali zinazohusu masuala ya usalama na afya mahali pa kazi.

Miongoni mwa majukumu ya OSHA ni kusajili sehemu za kazi na kisha kuendelea kuzitembelea sehemu hizo kwa ajili ya kufanya ukaguzi na kutoa ushauri wa viwango stahiki vya Usalama na afya vinavyopaswa kuzingatiwa.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
191,647FollowersFollow
541,000SubscribersSubscribe

Latest Articles