27.2 C
Dar es Salaam
Wednesday, February 8, 2023

Contact us: [email protected]

TMA yatoa tahadhari mvua za vuli

 ANDREW MSECHU –DAR ES SALAAM 

MAMLAKA ya Hali ya Hewa (TMA) imetoa tahadhari kuhusu mvua za msimu wa vuli za mwaka huu, ikieleza kwamba huenda zikawa za chini ya wastani hadi wastani katika maeneo yote ya nchi, hivyo tahadhari inahitajika. 

Akizungumza na wanahabari wakati akitoa mwelekeo wa mvua za vuli zinazotarajiwa kuanza Oktoba hadi Desemba, Mkurugenzi Mkuu wa TMA, Dk. Agnes Kijazi alisema kutokana na mifumo ya hali ya hewa ilivyo kwa sasa na inayotarajiwa kuwa kwa Oktoba hadi Desemba, inatarajiwa kuwa na mvua za chini ya wastani hadi wastani. 

“Mvua za chini ya wastani hadi wastani zinatarajiwa katika maeneo ya ukanda wa Ziwa Viktoria, Nyanda za Juu Kaskazini Mashariki, Pwani ya Kaskazini pamoja na maeneo ya kaskazini mwa Mkoa wa Kigoma. 

“Kwa hiyo kwa taarifa hii, tunatoa ushauri na tahadhari kwa wadau wa kisekta, wakiwemo wa sekta ya kilimo na usalama wa chakula, mifugo na uvuvi, maliasili, wanyamapori na utalii, nishati na maji, usafirishaji, mamlaka za miji, afya pamoja na menejimenti za maafa,” alisema Dk. Kijazi. 

Alisema kwa utabiri huo, ushauri na tahadhari unatolewa mahususi kwa maeneo yanayopata mvua ya misimu miwili kwa mwaka, ambayo ni Nyanda za Juu Kaskazini Mashariki, Pwani ya Kaskazini, Ukanda wa Ziwa Viktoria na kaskasini mwa Mkoa wa Kigoma. 

 Dk. Kijazi alisema athari zinazotarajiwa kutokana na mvua hizo za chini ya wastani hadi wastani ni upungufu wa unyevunyevu katika udongo unaotarajiwa kujitokeza katika maeneo mengi, magonjwa ya mlipuko kutokana na upungufu wa maji safi na salama, upungufu wa malisho na maji unaoweza kusababisha migogoro ya wakulima na wafugaji na uwezekano wa matukio ya moto katika misitu na mapori. 

Alieleza kuwa sababu ya mvua hizo za chini ya kiwango hadi wastani ni mifumo ya hali ya hewa, ambapo hali ya joto la bahari katika eneo la kati la kitropiki ya Bahari ya Pasifiki liko chini ya wastani na inatarajiwa kuendelea kuwa hivyo katika kipindi chote cha msimu wa Oktoba hadi Desemba. 

Alisema hali hii inatarajiwa kupunguza nguvu ya mifumo inayosababisha mvua katika maeneo mengi yapatayo misimu miwili kwa mwaka na kwamba joto la bahari la wastani linatarajiwa katika maeneo ya upande wa magharibi mwa Bahari ya Hindi. 

“Upande wa mashariki mwa Bahari ya Hindi unatarajiwa kuwa na joto la bahari la juu ya wastani hali inayosababisha msukumo wa unyevunyevu kutoka baharini kuelekea pwani ya maeneo ya Nyanda za Juu Kaskazini Mashariki mwa nchi,” alisema Dk. Kijazi. 

Alisema kutokana na hali hiyo, kwa upande wa sekta ya kilimo, kutokana na kupungua kwa unyevunyevu ardhini kunaweza kusababisha kujitokeza kwa visumbufu vya mazao na magonjwa. 

“Hivyo wakulima wanatakiwa kupanda mbegu na mazao yanayoweza kustahimili ukame na kukomaa ndani ya muda mfupi, pia kuendelea kupata ushauri kwa maofisa ugani kuhusu namna bora ya kuendesha kilimo kwa usalama wa chakula na lishe,” alisema Dk. Kijazi. 

Alisema kuwa kwa upande wa mifugo na uvuvi, magonjwa ya mifugo na mazao ya uvuvi yatapungua, lakini mtiririko hafifu wa maji unatarajiwa kusababisha uzalishaji mdogo wa mazao ya samaki na mifugo, na pia kunaweza kuwa na upungufu wa malisho na maji unaoweza kusababisha migogoro ya wakulima na wafugaji, hivyo wakulima na wafugaji wanatakiwa kufuata ushauri kwa maofisa ugani. 

Dk. Kijazi alisema sekta ya watalii na wanyamapori inatakiwa kuendelea kutoa elimu kwa wahusika kuhusu uwezekano wa kupungua kwa maji na malisho katika mbuga na hifadhi, sekta ya usafirishaji kutumia vyema muda huo kuharakisha ujenzi wa miundombinu, sekta ya nishati, maji na madini kujipanga kukabiliana na upungufu wa maji katika mabwawa kwa kuwa na njia za nishati mbadala, matumizi sahihi ya maji katika uchakataji madini, umwagiliaji na matumizi ya majumbani. 

“Lakini pia kwa mamlaka za miji zinashauriwa kutumia fursa hiyo kuboresha mfumo wa usambazaji wa maji safi na taka, sekta ya afya kuchukua hatua kupunguza athari za mlipuko wa magonjwa ya kuambukiza, zinazoweza kujitokeza na kuhimiza usafi wa mazingira, kwa menejimenti ya maafa inatakiwa kupanga mikakati stahiki ya kukabiliana na matuko ya moto katika mapori na misitu,” alisema Dk. Kijazi. 

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
208,871FollowersFollow
561,000SubscribersSubscribe

Latest Articles