23.4 C
Dar es Salaam
Saturday, April 27, 2024

Contact us: [email protected]

Ndugai azindua Bunge ‘Live’ Kenya

MWANDISHI WETU-DAR ES SALAAM

SPIKA wa Bunge, Job Ndugai amewataka Wakenya kujifunza na kutumia lugha ya Kiswahili kwa kuwa kwa sasa ni miongoni mwa lugha rasmi katika Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC).

Pamoja na hili, pia amewapongeza Wakenya kwa kuonyesha mubashara vikao vya Kamati vya Bunge.

Hayo aliyasema jana jijini Nairobi nchini Kenya, wakati akizindua Kanuni za Kudumu za Bunge kwa lugha ya Kiswahili, tukio ambalo lilirushwa mubashara na runinga ya Citizen ya nchini humo.

“Nchi zetu kwa muda mrefu zimekuwa na kasumba kuhusu lugha zetu wenyewe ni dhaifu, duni, lakini lugha za watawala wetu ni bora na za juu. Nawapongeza kwa uzinduzi, kwamba sasa vikao vya kamati mbalimbali vitarushwa mubashara (Live).

 “Ukitaka kujifunza lugha fulani ni lazima utumie kamusi ya lugha yenyewe, kwa hiyo ninawatia moyo muendelee kujifunza Kiswahili kwa sababu sasa hivi kinatumika kama lugha mojawapo muhimu na rasmi katika Jumuiya ya SADC, Umoja wa Afrika, Bunge la Afrika, lakini pia kwenye Jumuiya yetu ya Afrika Mashariki Kiswahili ni moja ya lugha rasmi inayotumika,” alisema Ndugai.

Katika msafara huo, Ndugai aliambatana na Mbunge wa Same Mashariki, Naghejwa Kaboyoka (Chadema) ambaye pia ni Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge ya Hesabu za Serikali (PAC).

“Ili uweze kupata mafanikio, ni vizuri ukajua lugha ya Kiswahili hata kama ni kile cha kuombea maji, sio vibaya kuzungumza Kiingereza, lakini ili uweze kufanikiwa katika mambo yako unayoyafanya, ni vyema ukajifunza Kiswahili pia.

“Huwa tunafuatilia wakati wa Uchaguzi Mkuu wa Kenya, asilimia 60 ya wanasiasa wengi kwenye kampeni wanatumia Kiswahili, sasa itakuwa jambo la ajabu unaomba kura kwa wanannchi kwa Kiswahili halafu ukifika bungeni unatumia lugha nyingine.

“Nawatia moyo sana, si lugha ngumu hata kidogo, Kiswahili hakikwepeki kwa sasa katika eneo letu la Afrika Mashariki,” alisema Ndugai.

Pia aliupongeza uongozi wa Bunge la Kenya kwa kuandaa taarifa za kamati walizoziandaa na kwa hatua waliyoifikia ya kurusha mubashara matangazo ya kamati za Bunge ili wananchi wa Kenya kuona kinachoendelea.

BUNGE ‘LIVE’ TANZANIA

Aprili 25, 2016 jijini Dodoma, aliyekuwa Waziri wa Habari, Nape Nnauye alijikuka katika wakati mgumu baada ya kuzomewa na wabunge wa Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni wakati akitetea hoja ya Serikali ya kutokurusha matangazo hayo moja kwa moja.

Hata mara kadhaa baada ya kuondolewa kwenye uwaziri, alinukuliwa akisema kuwa si yeye aliyeanzisha ajenda ya kuua matangazo hayo bali ilikuwapo tangu Bunge la 10.

Septemba 2017, majadala wa kuzuiwa kwa matangazo ya moja kwa moja kutoka bungeni uliibuka upya bungeni huku baadhi ya wabunge wa upinzani wakilalamikia hali hiyo, akiwamo Mbunge wa Viti Maalumu, Aida Khenani (Chadema) aliyehoji sababu za kuzuia shughuli za Bunge kuonekana moja kwa moja.

Akichangia mjadala wa bajeti ya Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Khenani alisema Shirika la Utangazaji Tanzania (TBC) linatumia kodi za wananchi, lakini vikao vya wabunge waliowachagua havionyeshwi moja kwa moja kuwawezesha kufuatilia wanachozungumza wawakilishi wao.

“Hapo kuna tatizo,” alisema Khemani ambaye aliungwa mkono na mbunge mwenzake wa Viti Maalumu, Mariam Msabaha (Chadema), aliyehoji sababu za Bunge kuwa na hofu ya vikao vyake kuonekana moja kwa moja.

Hata hivyo, Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Dk. Harrison Mwakyembe, alijibu hoja hizo akisema hoja ya Bunge Live amekuwa akiijibu na anachoweza kusema ni kuwa Mamlaka ya Udhibiti wa Huduma za Mawasiliano Tanzania (TCRA), imelikabidhi Bunge leseni na litaweza kuamua lolote.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles