Baba afungwa maisha kwa kumpa mimba mtoto wake

0
681

Walter Mguluchuma-Katavi

MAHAKAMA ya Wilaya ya Mpanda mkoani Katavi, jana imemuhukumu mkazi wa Mtaa wa Mjimwema, Lazaro Charles (35) kutumikia  kifungo cha maisha jela, baada ya kupatikana na hatia ya kumbaka na kumpa mimba mtoto wake wa kumzaa.

Mtoto huyo mwenye umri wa miaka 14, ni mwanafunzi wa darasa la saba Shule ya Msingi Majengo, Manispaa ya Mpanda.

Hukumu hiyo iliyovutia hisia za wakazi wengi wa  Manispaa ya Mpanda, ilitolewa jana na Hakimu   Mkazi Mfawidhi wa Mahakama ya Wilaya ya  Mpanda, Gosper Luoga baada ya mahakama kuridhika na ushahidi uliotolewa mahakamani na upande wa mashtaka.

Katika  kesi hiyo, upande wa mashtaka ambao uliongozwa na mwanasheria wa Serikali,     Gregory Muhangwa, ulikuwa na mashahidi watano na upande wa utetezi, mshtakiwa alikuwa na shahidi mmoja ambaye ni mke wake.

Awali Muhangwa alidai mahakamani hapo kuwa mshtakiwa alitenda kosa hilo kwa nyakati tofauti Januari mosi, 2017 na Aprili 29, mwaka huu.

Alidai kuwa mshtakiwa alikuwa akitenda kosa hilo nyumbani kwake, wakati mama wa mtoto alipokuwa akisafiri.

Kwamba alikuwa akiingia kwenye chumba alichokuwa akilala mtoto na kumbaka kwa nguvu.

Muhangwa alidai kuwa baada ya kumbaka, alikuwa akimwekea majani sehemu za siri kama dawa ya kienyeji ili kumwondolea maumivu.

 Alisema hali ya mtoto ilianza kubadilika na kuwafanya walimu wake waamue kumpeleka hospitali kufanya vipimo ambavyo vilionyesha ni mjamzito.

Alipoulizwa nani kampa ujauzito, alimtaja baba yake mzazi Lazaro Charles.

 Hakimu Mkazi Mfawidhi Luoga baada ya kusikiliza ushahidi wa kesi hiyo uliotolewa na upande wa mashtaka, alisema mahakama imeridhika nao.

Alisema mahakama inamtia hatiani mshtakiwa kwa kosa la kifungu cha sheria namba 158 (1)     (a) sura ya 16 ya marekebisho ya sheria ya mwaka 2002.

Alimtaka mshtakiwa kama atakuwa na sababu yoyote ile ya msingi ambayo inaweza kuishawishi mahakama ili kumpunguzia adhabu ajitetee.

Charles aliiomba impatie nakala ya hukumu ya mwenendo wa kesi tu, kwani hana utetezi wowote.

 Baada ya ombi hilo, Muhangwa aliiomba mahakama itoe adhabu kali kwa mshtakiwa ili iwe fundisho kwa wazazi wengine wenye tabia kama hiyo.

 Hakimu Luoga baada ya kusikiliza pande zote, alisoma hukumu na kuiambia mahakama mshtakiwa amepatikana na kosa, hivyo mahakama inamhukumu kutumikia kifungo cha maisha jela.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here