23.6 C
Dar es Salaam
Wednesday, September 27, 2023

Contact us: [email protected]

Ndoa zinavyoharibiwa na ngono holela

MAJUZI niliwaambia wanafunzi wangu wakitaka kuwa na ndoa bora hapo baadaye lazima wajifunze kuacha ngono kabla ya ndoa. 

Kusikia hivyo walicheka mithili ya watu waliosikia kichekesho kipya cha mwaka, sikushangaa. Kwa mujibu wa takwimu zisizo rasmi wastani wa umri wa kijana kuanza ngono ni miaka kati ya 14 na 15. Wanafunzi wangu walikuwa na kati ya umri wa miaka 21 na 23.

Wangali wakicheka niliwakaribisha kutazama video ya utafiti wa Profesa Walter Mischel wa Chuo Kikuu cha Stanford uliopima subira ya watoto wa miaka minne. Video hiyo iliwaonyesha watoto waliogawiwa vitu vitamu viitwavyo marshmallow ili kuona kama wangeweza kujizuia kula hata katika mazingira ambayo walikuwa na uhuru wa kufanya hivyo. 

Mtafiti aliwaambia watoto wangeweza kula pipi hizo kama wangetaka lakini kama wangesubiri mpaka atakaporudi wangepata ‘marshmallow’ zaidi kama takrima ya kujinyima. Mwisho wa video hiyo, watoto wachache tu ndio walioweza kujizuia wakati zaidi ya nusu ya watoto walishindwa kujizuia.  

Video hiyo ilizima ghafla kicheko cha wanafunzi wangu. Nilichukua kipaza sauti na kuwakaribisha kutafakari kile walichojifunza kwenye utafiti huo. Baada ya kusikiliza maoni yao mengi, niliamua kuhitimisha; “Hawa watoto tunaowaona hapa walifuatiliwa na Mischel kwa miaka mingi baadaye. Mischel aligundua jambo la ajabu kidogo. Wale walioweza kungoja walikuwa na mafanikio makubwa shuleni na hata katika maisha kwa ujumla. Walioshindwa waliishia kuwa watu wasio na mbele wa nyuma.” 

Ukumbi wote wa mhadhara ulikuwa kimya, wanafunzi walikuwa wakifuatilia niliyokuwa nikiwaeleza. Niliendelea kuwaeleza uwezo wa kujizuia ni tabia inayohitajika sana kwenye maisha. Kuanzia kwenye taaluma, biashara, kazi, imani na hata kwenye ndoa. Bila kujifunza kujizuia huwezi kupata mafanikio yoyote. 

Kuna mambo unaweza kuyafanya kama kijana usione matokeo yake lakini yakakujengea mustakabali mbovu kwenye maisha ya baadaye ya ndoa. 

Mfano kufanya ngono holela kabla ya ndoa. Ngono ikiwa tabia hutaiacha ukiwa kwenye ndoa, usipoweza kujifunza kujizuia sasa ukiwa kijana na kufanya maamuzi magumu ya kusema sitafanya ngono kabla ya ndoa, itakuwa vigumu kwako kuwa mume au mke mwaminifu ikiwa utafanikiwa kuingia kwenye ndoa. 

Wanaume wengi huchanganya kumpenda mwanamke na kumtamani. Ingawa upendo unazo chembechembe fulani za tamaa ndani yake, kwa kiasi kikubwa upendo una uwezo mkubwa wa kujizuia kuliko tamaa. Mwanamume mwenye upendo wa dhati hatangulizi hisia bali maamuzi. Upendo humfanya awe na uwezo wa kutokufanya mapenzi na mtu ampendaye. 

Kwa upande mwingine mwanamume mwenye tamaa hufikiri akimpenda mwanamke lazima afanye naye ngono. Mtu huyu anayeongozwa na hisia kuliko maamuzi, anapofanikiwa kufanya ngono na mwanamke huyo msisimko huo wa kimapenzi aliokuwa nao awali huzimika. Hali hii inapotokea hujikuta akipunguza mawasiliano na hatimaye uhusiano wake na mwanamke huzorota.  

Pamoja na starehe yake, ngono inapofanywa holela na mtu msiye na makubaliano naye inapunguza kujiamini kwako.  Fikiria msichana anayetoa mwili wake kwa mwanamume kama ishara ya kumpenda. Kinyume na matarajio yake, mwanamume hupoteza msisimuko naye hasa anaposhiriki ngono wakati hana mpango naye. Katika mazingira hayo ni rahisi uhusiano huo kufifia na hatimaye kumfanya msichana aliyeamini anapendwa kuanza kujisikia kukataliwa.

Mazingira kama haya huwakuta wasichana wengi wanaojikuta wameachwa na rafiki zao bila kutarajia. Kuachwa huwafanya wawe na wasiwasi na uzuri na sifa nyingine walizonazo. Wengine huanza kujichukia na kuamua kujirahisisha kwa wanaume wengine kama njia ya kujiaminisha kuwa bado wanapendwa. Hali kama hii hupunguza sana kujiamini kwa mwanamke.

Mnapokubaliana kufanya ngono na mtu mtakayefunga naye ndoa, kwa haraka haraka inaweza kuonekana ni ishara ya kuaminiana. Kwamba ameweza kuutoa mwili wake kwa ajili yako, inaweza kutafsirika kama kiwango cha juu cha mapenzi.

Hata hivyo, kisaikolojia hali ya kutokuaminiana katika ndoa ina uwezekano mkubwa wa kuanzia hapa. Mwenzako huanza kuwa na wasiwasi na uaminifu wako unapokuwa na watu wengine. Ikiwa uko kwenye ndoa na unajiuliza kwa nini mwenzako hakuamini, upo uwezekano mkubwa mlifanya kosa la kukutana kingono kabla ya ndoa. 

Mbali na ngono kuongeza uwezekano wa kuambukizwa magonjwa ya zinaa, mimba zisizotarajiwa na kukuvurugia mipango ya maisha, ukiweza kujifunza kusema hapana kwa ngono kabla ya ndoa, utapunguza uwezekano wa kuingia kwenye ndoa na watu wasiokufaa. Hata kama ulishaanza bado una nafasi ya kusema hapana tangu leo.

Na CHRISTIAN BWAYA, Mhadhiri wa Saikolojia Chuo Kikuu cha Kikatoliki Mwenge (MWECAU). Twitter: @bwaya Simu: 0754870815

Heri ya mwaka mpya 2020.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,729FollowersFollow
574,000SubscribersSubscribe

Latest Articles