31.2 C
Dar es Salaam
Tuesday, November 28, 2023

Contact us: [email protected]

Kanzidata ya DNA kurahisisha utambuzi miili, wahalifu

Na AVELINE KITOMARY-DAR ES SALAAM

MAABARA ya Mkemia Mkuu wa Serikali imekuwa na nafasi kubwa kusaidia utambuzi na udhibiti wa kemikali.

Wakati wa kuanzishwa kwake lengo kuu lilikuwa ni kufanya utafiti wa magonjwa ya ukanda wa joto (Tropical Disease) mwaka 1895 na magonjwa yaliyolengwa kwa wakati huo yalikuwa ni malaria na kifua kikuu.

Baada ya uhuru maabara hiyo ilikuwa ni idara ndani ya Wizara ya Afya lakini kwa sasa ni mamlaka inayojitegemea kutokana kuundwa rasmi kisheria kupitia sheria ya Mamlaka ya Maabara ya Mkemia Mkuu wa Serikali Na.8 ya mwaka 2016.

Jukumu la maabara hiyo ni pamoja na kufanya uchunguzi wa kitaalamu au kisayansi wa sampuli  mbalimbali zinazotokana na makosa ya jinai, usalama na ubora wa bidhaa, masuala ya kijamii na usalama wa afya kazini.

Licha ya majukumu hayo pia maabara hiyo inasimamia utekelezaji wa sheria za udhibiti wa kemikali viwandani na majumbani na kudhibiti matumizi ya vinasaba vya binadamu. Pia kutoa ushahidi wa kitaalamu mahakamani kwenye mashauri yote yanayohusisha uchunguzi wa kimaabara.

MAFANIKIO

MKEMIA Mkuu wa Serikali, Dk. Fidelice Mafumiko

Mkemia Mkuu wa Serikali, Dk. Fidelice Mafumiko, anasema mafanikio yaliyopatikana ni pamoja na ununuzi wa mitambo, ujenzi wa miundombinu na ukuzaji wa Tehama.

Mafanikio mengine ni katika uchunguzi wa maabara hasa katika matukio makubwa, udhibiti wa kemikali na taka kemikali.

“Tumenunua mitambo yenye uwezo wa kufanya kazi ya uchunguzi wa sampuli za dawa za kulevya, vyakula, dawa za binadamu, mifugo, viambata vya sumu, viuatilifu na bidhaa za viwandani yote ina thamani ya Sh bilioni 6.5.

“Mitambo hiyo inasaidia kubaini viwango vya madini kwenye udongo, uchunguzi wa vinasaba na mafuta ya kula,” anasema. 

Dk. Mafumiko anasema pia wameweza kuimarisha usimamizi na udhibiti wa kemikali kwa lengo la kulinda afya za wananchi na mazingira dhidi ya matumizi yasiyo salama ya kemikali.

“Kuongezwa kwa rasilimali watu na kufanya ukaguzi kwa saa 24 katika mipaka 45 nchini, ongezeko hilo ni kutokana na usimamizi thabiti wa sheria ya usimamizi na udhibiti wa kemikali za viwandani na majumbani,” anasema.

Dk. Mafumiko anasema maabara hiyo pia imekuwa mstari wa mbele kushiriki katika majanga makubwa ya kitaifa hasa katika utambuzi wa miili iliyoharibika.

“Matukio tuliyoshiriki ni kama kuzama kwa kivuko cha MV Nyerere Ukerewe, miili 10 ilitambuliwa baada ya ulinganifu wa ndugu 12 katika sampuli 39 zilizochukuliwa. Katika ajili ya lori iliyotokea Tarime mwaka 2018 miili 14 ilitambuliwa baada ya ndugu 25 kufanyiwa upimaji wa vinasaba.

“Katika Ajali ya roli la mafuta lililotokea Msamvu Morogoro  miili 61 ilitambuliwa kulingana na sampuli za ndugu waliojitokeza na kuna lori lililopata ajali na kuwaka moto eneo la kibiti mkoani Pwani watu watatu walitambulika baada ya ndugu kujitokeza.

“Naweza kusema kuwa tumeendelea kuimarika katika kutoa msaada wa aina hii kwa jamii hasa majanga yanavyotokea kwani tulivyo sasa si sawa na mwanzo,”anasema.

Akizungumzi mapato anasema katika kipindi cha miaka minne yameongezeka na kwa sasa yamefikia Sh bilioni 24.246 tofauti na Sh bilioni 9.342 za mwaka 2015/2016 na kufanya ongezeko la mapato kufikia asilimia 118.

Kwa mujibu wa  Dk. Mafumiko, mapato hayo yameongezeka kutokana na kuimarishwa kwa mifumo ya udhibiti na ukusanyaji wa mapato na kuimarika kwa mifumo ya ndani ya ukaguzi na udhibiti fedha na utunzaji wa hesabu.

“Fedha hizi zimesaidia katika ununuzi na ukarabati wa mitambo ya maabara, kuboresha miundombinu ya maabara, kununua vitendanishi na kuimarisha ukaguzi wa kemikali,” anasema.

HUDUMA ZA KITAALAMU 

Mamlaka ya maabara ya mkemia mkuu pia imekuwa mstari wa mbele katika kutoa ushauri wa kitaalamu na mchango katika tiba kwa kushirikiana na hospitali mbalimbali ndani ya nchi.

Dk. Mufumiko anasema huduma walizoshiriki ni pamoja na upandikizaji wa figo na utambuzi wa jinsia tawala kwa watoto waliozaliwa na jinsia mbili. 

“Katika hili tumekuwa tukishirikiana na Hospitali ya Taifa ya Muhimbili, KCMC na Bugando na tumeweza  kufanya uchunguzi wa kimaabara kwa kutumia teknolojia ya vinasaba vya binadamu, kwenye uchunguzi wa kutambua uhusiano wa mtoaji na mpokeaji wa figo ili kuwezesha upandikizaji kwa mtu mwingine kwa mafanikio. 

“Pia kufanya uchunguzi wa kuwezesha utambuzi wa jinsi tawala kwa watoto wanaozaliwa na jinsi mbili ili kuweza kupata matibabu stahiki.

“Katika kipindi cha miaka minne tumefanikiwa kufanya uchunguzi wa ulinganishi kwa ajili ya upandikizaji wa figo kwa watu 29 na utambuzi wa jinsi tawala 48,” anasema. 

DNA

Anasema wanatarajia kuanzisha mfumo wa kanzidata ya Taifa katika upimaji wa sampuli za vinasaba (DNA) utakaosaidia kurahisisha utambuzi wa miili iliyoharibika na watu wanaojihusisha na uhalifu kwa kurahisisha uchunguzi na kutokutumia ndugu.

Mfumo huo pia utatumiwa katika kurahisisha huduma za matibabu kwa kuangalia mfanano wa vinasaba unaolingana kwa ndugu wa karibu.

Dk. Mafumiko anasema kuwa mfumo huo pia utatumika kwa watoto wa mtaani ambao wametelekezwa na wazazi wao. 

“Tunataka tutumie kipindi cha miaka miwili hilo suala likamilike, linaenda hatua kwa hatua na inahitaji umakini mkubwa.

“Tuitashirikiana na taasisi zingine kama NIDA na RITA na mfumo huo utasaidia utambuzi katika miili iliyoharibika lakini hii ni tofauti.

“Ukiwa na database (kanzidata) badala ya kutafuta ndugu tunawapata kupitia mfumo huo, pia itasaidia kwenye uhalifu mfano ubakaji, mauaji ya kutumia silaha sasa tunapoanza kutumia mfumo wa database tutaweza kuwatambua. 

“Pia itatumika katika matibabu tutashirikiana na madaktari kuwasaidia kugundua DNA ambazo zinafanana mfano, mtu akitaka kumtolea ndugu yake figo mfumo utaonesha nani ana uhusiano na anastahili ampatie mgonjwa figo kati ya ndugu,”anasema. 

Faida nyingine ya mfumo huo ni kuhusika katika suala zima la mirathi na uhalifu wa makosa ya jinai kama wizi, ubakaji, mauaji na majanga.

“Pia mfumo huu utatumika kwa watoto wa mitaani ambao wametelekezwa na wazazi wao, tutapima sampuli zao na kupitia kanzidata wazazi wao wanaweza kupatikana.

“Hivyo itarahisisha mambo mengi sana hata katika masuala ya mirathi tutashirikiana na mahakama,”anasema Dk. Mafumiko. 

Anasema kuwa mfumo huo utaanza kwa watoto ambao wanazaliwa, katika mifumo ya matibabu na mahakamani.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
579,000SubscribersSubscribe

Latest Articles