29.2 C
Dar es Salaam
Wednesday, December 6, 2023

Contact us: [email protected]

Matatani kuuza ARVs kunenepesha ng’ombe

Mwandishi Wetu-Igunga

JESHI la Polisi wilayani Igunga mkoani Tabora, linamshikiria mfamasia wa hospitali ya wilaya hiyo, Francis Mlesa (33) kwa tuhumza wizi wa dawa za kufubaza virusi vya ugonjwa wa Ukimwi (ARVs) na nyinginezo.

Mfamasia huyo anadaiwa kuiba dawa hizo na kwenda kuwauzia wafanyabiashara kwa ajili ya kunenepesha ng’ombe.

Habari za ndani kutoka kwa baadhi ya watumishi wenzake, zinasema hii si mara ya kwanza mtuhumiwa kuhusishwa na tukio hilo.

Mlesa ambaye yuko kitengo cha ugawaji wa dawa hospitalini hapo, anadaiwa kutenda kosa hilo Desemba 24, mwaka huu.

Akizungumza na waandishi wa habari ofisini kwake juzi, Ofisa Tarafa ya Igunga, Shadrack Kalekayo alisema Mlesa alishitukiwa na mlinzi aliyekuwa zamu ya saa 1:30 usiku, baada ya kumuona akiwa amefunga maboksi mawili ya dawa kwenye baiskeli yake.

Alisema baada ya kumuona alimsimamisha na kuanza kumhoji, lakini mtuhumiwa alisema muda wa matumizi wa dawa hizo umepita.

Mlinzi huyo, Rushinangeme Paulo alisema baada kuangalia kwa makini dawa hizo muda wake wa matumizi ulikuwa haujapita.

“Baada ya kumuona anatoka na baiskeli, huku akiwa amefunga maboksi mawili, nilimtilia shaka, nikamsimamisha kumhoji.

“Akanijibu dawa hizi muda wake wa matumizi umekwisha, nilipoziona niliona mbona bado hata mwaka wa kuisha matumizi haujafika,”alisema.

Alisema baada ya kumbana sawa sawa, mtuhumiwa alikimbia na dawa hizo.

Alisema baada ya msako mkali, Desemba 26, mwaka huu walifanikiwa kumkamata mtuhumiwa na kumfikisha mbele ya uongozi wa hospitali na kukiri kuiba dawa hizo.

Alisema wakati anahojiwa, alisema alichukua dawa hizo kwa ajili ya kuziteketeza kwa moto kwa sababu zilikuwa hazifai kwa matumizi ya binadamu tena.

Alisema baada ya kikao hicho, uongozi wa hospitali ukiongozwa na Mganga Mkuu wa Wilaya Igunga, Deus Rutha walimpeleka mtuhumiwa kituo cha polisi Igunga.

Mmoja wa mashuhuda, Kasembe Nangale alisema siku tukio alikuwa anatoka kumwangalia dada yake, Chaula Nangale ambaye amelazwa wodi namba 3 akisumbuliwa na ugonjwa wa kifua, tumbo na mgongo.

Alisema alipofika geti kubwa la kutokea, alimuona Mlesa akiwa amefunga maboksi mawili kwenye baiskeli kabla hajatoka mlinzi alimuuliza dawa hizo anazipeleka wapi.

“Mimi nilishuhudia mlinzi akimhoji mtumishi huyu, alijibu dawa hizo anakwenda kuziteketeza kwa moto kwani muda wake wa matumizi umekwisha,”alisema.

Alisema baada ya mtuhumiwa kutoa jibu hilo, mlinzi alimwamuru afungue dawa ili wazione.

Alipofungua ndipo dawa hizo zikaonekana ni ARVs, huku mtumishi huyo akitoroka nazo, baada ya mlinzi kuzidiwa na watu wanaopita katika geti hilo.

Alisema baada ya kuona kukimbia alitoa taarifa ofisi ya  Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) Wilaya ya Igunga.

Alisema Mkuu wa TAKUKURU Igunga, Francis Nzuakuu alifika hospitali na kuanza kazi ya kumsaka mtumiwa bila mafanikio.

Mganga Mkuu wa Wilaya ya Igunga, Deus Rutha alisema hospitali yake iko salama wala hakuna mtumishi aliyepelekwa kituo cha polisi kwa wizi wa dawa.

Wakati akisema hivyo, Nzuakuu alisema yeye alipigiwa simu na raia mwema kuwa kuna mtumishi ameiba dawa hospitalini na ametoroka nazo ambapo alifika eneo la tukio na kuanza kumsaka mtumishi bila mafanikio.

Alisema baada ya kumkosa mtumishi huyo, alimwagiza Rutha kumsaka hadi kumpata mtuhumiwa ambapo Desemba 26, walifanikiwa kumkamata.

Mkuu wa Wilaya ya Igunga, John Mwaipopo alisema tukio hilo lipo na mtuhumiwa anashikiliwa polisi.

Kutokana na hali hiyo,alitoa wito kwa watumishi wa idara zote kufanya kazi kwa uadilifu na kujiepusha na vitendo hivyo kwa sababu Serikali haitamfumbia macho mtumishi yoyote kwa wizi wa dawa. Kamanda wa Polisi Mkoa wa Tabora, Barnabas Mwakalukwa alipoulizwa juu ya tukio hilo,alithibitisha Malesa kushikiliwa na kusema hawezi kuzungumzia kwa kina kwa sababu wanaendelea kumhoji ili kubaini idadi na thamani ya dawa alizoiba.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
580,000SubscribersSubscribe

Latest Articles