29.7 C
Dar es Salaam
Wednesday, August 17, 2022

Mnyika ataka kura nne uchaguzi mkuu 2020

BENJAMIN MASESE-MWANZA

KATIBU Mkuu wa Chama Cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), John Mnyika amemuomba Rais Dk. John Magufuli  kuandaa utaratibu utakaowezesha Watanzania kupiga kura  za aina nne, wakati wa uchaguzi  mkuu mwaka 2020.

Alisema utaratibu huo, utamwezesha mwananchi kupiga kura ya kumchagua rais, mbunge, diwani na kura ya maoni juu Katiba mpya ambayo itaweka uhalisia Watanzania wanahitaji Katiba mpya au la.

Kauli hiyo, aliitoa jana katika ofisi za Chadema Kanda ya Viktoria jijini Mwanza, baada ya kusimikwa na wazee wa jadi ya kabila la Wasukuma na kupewa  jina la Chifu la Malonga, likiwa na maana ya  mrekebishaji yaani kutengeneza mambo yaliyoharibika na kuwa mazuri.

Aisema kama utaratibu huo, utashindikana ni vema Serikali kwa kushirikiana na Bunge kufanya  marekebisho ya mpito kwenye Katiba iliyopo sasa kabla ya uchaguzi mkuu wa 2020  ili kuwa na tume huru ya uchaguzi.

Alisema  muda uliobaki kabla ya uchaguzi huo,  haiwezekani kukamilika kwa mchakato mzima wa katiba mpya,inawezekana kufanyika marekebisho ya muda ili kukidhi matakwa ya wananchi yakiwamo kupinga matokeo ya rais mahakamani na kuwa na tume huru.

“Nilipochaguliwa katibu mkuu  kuna vipaumbele karibu vitano nilijiwekea kikiwamo cha kudai tume huru ya uchaguzi, mpya kwa bahati nzuri watanzania wanayo rasimu ya Katiba mpya ya Jaji Joseph Warioba ambayo kwa namna moja au nyingine iliharibiwa na watu wachache.

“Mara kadhaa Rais Dk. Magufuli amenukuliwa akisema Katiba mpya siyo kipaumbele chake, wakati kwenye ilani ya chama chake ni miongoni mwa mambo ambayo waliahidi kuyatekeleza, alipokuja kuzindua Bunge mjini Dodoma alihiadi, tunashangaa anabadilika,tunapaswa kuchukua tahadhari kwa kumtaka  aruhusu mchakato uendelee.

“Kwa kuwa muda uliobaki kwenda kwenye mchakato wa uchaguzi mkuu ni mchache, tunamshauri rais aandae utaratibu utakaowezesha mwananchi kupiga kura ya kumchagua diwani, mbunge, rais na kupira kura ya maoni juu ya katiba mpya, hapo tutaona uhalisia kama Watanzania wanahitaji jambo hilo au la.

“Sote tunajua Katiba mpya ni ya miaka kuanzia 50 na kuendelea,kama  mchakato huio utakuwa mgumu, basi kabla ya uchaguzi lazima tufanye marekebisho ya mpito kwenye katiba yetu ili tupate tume huru ya uchaguzi  na matokeo ya rais kupingwa mahakamani vingine nguvu ya umma itatumika ili kupata ushindi,”alisema.

Akizungumza na viongozi wa kanda hiyo,  Mnyika alisema hakuna budi viongozi wa vyama vya upinzani kuungana pamoja kupeleka muswada bungeni kwa ajili ya kufanya marekebisho hayo

Alisema yapo madai Katiba mpya, ni gharama kubwa, lakini Rais Dk. Magufuli akikubali kupeleka muswada wa dharura bungeni ili kufanya marekebisho ya mpito kwenye katiba  iliyopo  bila kusubiria mchakato mzima wa katiba mpya.

Mnyika  ambaye alikuwa akishangiliwa kila mara , alisema katiba iliyopo inaweza kuongezwa vipengele vitatu ambavyo ni  tume huru ya uchaguzi, ibara inayotaka matokeo ya uchaguzi wa rais yapingwe mahakamani na kifungu kinachosema ili mtu atangazwe kuwa mshindi wa urais lazima awe amezidi asilimia 50 ya kura zote.

Alisema wakati wa uchaguzi mkuu kiwepo pia kipengele cha kupiga kura ya maoni kuhusu aina gani ya katiba inayotakiwa ili wananchi waipigie kura wakati wakichagua wabunge, madiwani na rais.

Kwa upande wa wazee  waliomsimika  Mnyika  na kumkabidhi mkuki, ngoma ya asili, kigoda na kibuyu, walisema kumsimika a na kumpa jina la kichifu  ni ishara ushindi wa chama hicho na kushika dola baada ya uchaguzi Mkuu mwaka 2020.

Wazee hao, ni Jakton Katinde, Buluno Zacharia  na Mzee Mtani  walisema yapo mambo yaliyoharibika katika uongozi uliopita hivyo wameamua kumpa jina la Malonja lenye maana ya mrekebishaji ambapo wana imani atarekebisha  baadhi ya masuala amabyo hayakwenda vizuri.

“Hata Nyerere alipokuwa akipigania uhuru wa taifa hili alikalia kigoda hiki akasema tunataka uhuru wetu, wazungu wote waliogopa na kutawanyika na wewe kukalia kigoda hiki umepewa nguvu ya kupambana na kushika dola,” alisema Katinde.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
198,905FollowersFollow
550,000SubscribersSubscribe

Latest Articles