22.2 C
Dar es Salaam
Saturday, August 20, 2022

Ndayiragije ataja vigezo mchezaji kuitwa Stars

NA ASHA KIGUNDULA

KOCHA Mkuu wa timu ya Tanzania, Taifa Stars, Etienne Ndayiragije, amesema nidhamu ya mchezaji na kujituma kwake uwanjani, ndivyo vigezo vya msingi vinavyomfanya aitwe katika kikosi chake.

Akizungumza Dar es Salaam jana alipotembelea ofisi za Kampuni ya New Habari (2006) Ltd, wazalishaji wa magazeti ya MTANZANIA, BINGWA, DIMBA na RAI zilizopo Sinza Kijiweni, Ndayiragije alisema anaamini nidhamu kwa mchezaji ndani ya uwanja, ni muhimu mno.

Alisema anashukuru katika kipindi chake, wachezaji wanaoitwa Taifa Stars wamekuwa wakizingatia nidhamu, kitendo kinachompa faraja.

“Wakati mwingine utovu wa nidhamu kwa mchezaji, hutegemea na jinsi kocha anavyoishi nao, kwa upande wangu, huwa kila mchezaji ninamfanya kuiona timu ya taifa kama yake, sina ubaguzi, kila mmoja aone ufahari kuichezea timu yake ya Taifa,” alisema.

Alisema kwa jinsi anavyoishi na vijana wake pamoja na kuzungumza nao mara kwa mara, kuna wakati aliwahi kuulizwa imekuwaje hadi mmoja wa wachezaji wa timu hiyo anayesifika kwa utovu wa nidhamu katika klabu yake, lakini akiwa Stars anakuwa ‘mtoto mzuri’.

“Kuna wachezaji ambao wanasifika kwa utovu wa nidhamu katika klabu yao, lakini wakiwa timu ya Taifa, wao ndio huwa mstari wa mbele kuwakumbusha wenzao kufuata taratibu za kambi. Utovu wa nidhamu wa mchezaji unategemea na uhusiano baina yake na kocha wake,” alisema.

Wakati huo huo, Ndayiragije amelifagilia Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) chini ya Rais Wallace Karia kwa kutomwingilia katika majukumu yake, hasa katika suala zima la kuteua wachezaji na kupanga kikosi.

“Uongozi wa Karia huwa hautuingilii katika majukumu yetu, mimi na wenzangu (makocha wasaidizi, Juma Mgunda na Seleman Matola pamoja na meneja Nadir Haroub ‘Cannavaro’), katika kuteua wachezaji, huwa tunashirikishana na kila mmoja kutoa maoni yake, hakuna kiongozi yeyote wa TFF anayetuingilia,” alisema.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
199,057FollowersFollow
551,000SubscribersSubscribe

Latest Articles