23.3 C
Dar es Salaam
Friday, April 26, 2024

Contact us: [email protected]

Ndalichako atangaza kiama vyuo ambavyo havijalipa wanafunzi fedha za kujikimu

CHRISTINA GAULUHANGA Na TUNU NASSOR-DAR ES SALAAM

WAZIRI wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Profesa Joyce Ndalichako, ametoa siku tatu kwa vyuo nchini kuhakikisha wanawalipa fedha za kujikimu wanafunzi wote wanaostahili.

Akizungumza wakati akikabidhi magari manne kwa Chuo cha Taifa cha Usafirishaji (NIT), Ndalichako alisema baadhi ya vyuo hadi leo havijatoa fedha hizo kwa wanafunzi licha ya Rais John Magufuli kuagiza kuwa wanafunzi wakifika vyuoni wakute fedha zao.

Profesa Ndalichako alisema ni muhimu fedha hizo zitolewe kwa wanafunzi ili waendelee na masomo bila kupata usumbufu wowote.

Alisema wizara yake haitaweza kukivumilia chuo kitakachokiuka agizo hilo kwa sababu hakuna sababu ya kuchelewesha kufanya malipo hayo kwa kuwa fedha tayari zipo vyuoni.

“Kabla hata vyuo havijafunguliwa, tayari Serikali ilikuwa imetoa Sh bilioni 122 zikiwemo fedha za posho ya chakula na malazi kwa wanafunzi, pamoja na ada kwa ajili ya vyuo.

“Napongeza vyuo vilivyoweka utaratibu wa wanafunzi kulipwa hata kabla ya hawajaripoti vyuoni ili kuhakikisha tunaendana na maelekezo ya Rais kwamba wanaunzi wanavyofika shuleni wakute fedha zao.

“Nitoe wito kwa vyuo ambavyo hadi leo hii bado havijamaliza kuwalipa wanafunzi fedha za kujikimu, ikifika Ijumaa wanafunzi wote wawe wamekwishapata fedha zao, kwa sababu hakuna sababu yoyote ya kuchelewesha kufanya malipo kwa wanafunzi kwa sababu fedha tayari zipo chuoni.

“Rais wakati anatangaza kufunguliwa vyuo, alitoa maelekezo kwamba ni lazima wanafunzi wanapofika vyuoni wapate fedha, sasa maelekezo ya mkuu wa nchi ni lazima tuhakikishe tunayasimamia ipasavyo.

“Sisi wizara ambayo ndiyo tuna dhamana ya kusimamia vyuo, hatutakuwa na msalie mtume na chuo ambacho kitakaa na fedha za wanafunzi badala ya kuwapa wakati fedha zile zipo, na wanafunzi wameshafungua vyuo wapo vyuoni, hili suala la kusema wanafunzi wanachelewa kusaini si kweli, mtu ana njaa atakataaje kusaini?

“Na kama ameshasaini kwanini usubiri huyo mwingine ambaye ameshiba hana njaa? Kwa hiyo suala la kupewa fedha kwa wanafunzi naomba vyuo hadi ijumaa wanafunzi wawe wameshapata fedha zao, nawapongeza walioweka utaratibu wa kuwalipa wanafunzi kabla hata hawajaripoti vyuoni,” alisema Profesa Ndalichako.

Katika hatua nyingine, alisema Benki ya Dunia imetoa mkopo wa  Sh bilioni 175 sawa na Dola za Marekani Milioni 75 kwa Serikali ya Tanzania kwa lengo la kuleta mapinduzi katika vyuo  vinne vinavyotoa elimu ya ufundi  hapa nchini.

Alisema NIT ni miongoni mwa vyuo hivyo vitakavyonufaika na mkopo huo kupitia mradi wao wa kuleta mapinduzi kwenye elimu ya ufundi Afrika Mashariki (EASTRIP) ambacho kitapata Sh bilioni 49.

Profesa Ndalichako alisema mradi wa EASTRIP unatekelezwa katika nchi tatu za Afrika Mashariki ambazo ni Kenya, Ethiopia na Tanzania.

Akitaja vyuo vingine vitakavyonufaika na mkopo huo ni Taasisi ya Teknolojia ya Dar es Salaam  Campus (DIT DSM), DIT Campus ya Mwanza na Chuo cha Ufundi Arusha (ATC). 

Alisema malengo ya mradi huo ni kuvijengea vyuo hivyo uwezo ili viweze kutoa mafunzo bora na kuwapata wanafunzi wenye sifa stahiki ambazo zitawawezesha kujiajiri au kuajiriwa.

“Pia fedha hizo za  mradi zitatumika katika kujenga miundombinu ikiwemo madarasa, mabweni, karakana, ofisi za wahadhiri pamoja na watumishi wengine,” alisema Profesa Ndalichako. 

Alisema pia magari ambayo wamepatiwa NIT ni sehemu ya mradi huo, hivyo wanauomba uongozi wa chuo hicho yatumike vizuri na kwa malengo yaliyokusudiwa na si vinginevyo.

Kwa upande wake, Mkuu wa Chuo cha NIT, Profesa Zacharia Mganilwa alisema mradi wa EASTRIP ni wa miaka mitano, wenye lengo la kuongeza uwezo wa vyuo vya elimu ya ufundi na mafunzo  kutoa taaluma inayokidhi matakwa ya soko, kuongeza uwezo wa walimu pamoja na kuboresha miundombinu.

Alisema kiasi cha fedha cha Sh bilioni 49 ambacho NIT kitazipata, kitatumika katika kuboresha utawala na kutoa mafunzo kama kituo cha umahiri, kuimarisha mahusiano kati ya chuo na wadau mbalimbali wa sekta ya anga na operesheni za usafirishaji pamoja na kutoa udhamini kwa wanafunzi wasichana.

Naye, Mwenyekiti wa Baraza la Uongozi wa chuo, Profesa Bavo Nyichomba alisema hatua ya chuo kununua magari hayo ni dhahiri kuwa kimepata vitendea kazi madhubuti na ni matokeo ya juhudi za Serikali kupitia Wizara ya Elimu, Benki ya Dunia pamoja na Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles