Aliyechapisha maudhui Bongo times TV atiwa hatiani

0
614

KULWA MZEE, DAR ES SALAAM

Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu imemtia hatiani mfanyabiashara Obadia Kwitega kwa kosa la kuchapisha maudhui kwenye mtandao wa Bongo Times TV bila leseni ya Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA).

Mshtakiwa huyo alitiwa hatiani jana mbele ya Hakimu Mkazi Mwandamizi, Janeth Mtega baada ya kukiri kosa kwa kuandika barua kwa Mkurugenzi wa Mashtaka nchini (DPP) na kukubaliana kuwa mshtakiwa anatakiwa kulipa fidia ya Sh milioni mbili. 

Mshtakiwa alisomewa shtaka moja ambapo anadaiwa kwamba kati ya Januari 29 mwaka 2017 na Machi 29 mwaka 2019 katika maneo mbalimbali jijini  Dar es Salaam, kupitia televisheni ya mtandao ya Bongo Times TV alichapisha maudhui bila kuwa na leseni ya TCRA wakati akijua ni kinyume cha sheria.

Mshtakiwa alitiwa hatiani na kabla ya kupewa adhabu aliomba mahakama impunguzie adhabu kwa sababu ana familia inayomtegemea kwani anasomesha wadogo zake na ana mchumba anayetarajia kufunga naye ndoa muda si mrefu.

Wakili wa Serikali Faraji Nguka aliomba mahakama hiyo kumpa adhabu kali ili iwe fundisho kwa wengine.

Akitoa adhabu Hakimu Mtega alisema mahakama inampa adhabu mshtakiwa ya kulipa fidia Sh milioni mbili, faini milioni tano na endapo atashindwa ataenda jela mwaka mmoja.

Mshtakiwa amefanikiwa kulipa faini na ameachiwa huru.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here