NCCR-MAGEUZI YAJITOSA SAKATA LA MCHANGA

0
600

Na MWANDISHI WETU-DAR ES SALAAM

BAADA ya Rais, Dk. John Magufuli kukabidhiwa ripoti ya mchanga wa dhahabu, Chama cha NCCR-Mageuzi kimekitaka Chama Cha Mapinduzi (CCM), kuwaomba radhi Watanzania.

Katibu Mkuu wa NCCR-Mageuzi, Juju Danda, alisema katika taarifa yake kwa vyombo vya habari jana, kwamba ripoti hiyo ya mchanga imeanika uozo uliosababishwa na CCM kwa kipindi kirefu ilichokaa madarakani.

“Kwa maana hiyo, ni vema CCM wakakaa, wajiulize na kujipima kwa kuwaomba radhi Watanzania ambao wamekuwa wakiishi maisha magumu yaliyosababishwa na CCM.

“Kamati mbili zilizoundwa na Rais Dk. John Magufuli, zimethibitisha pasipo shaka, kuwa Watanzania wameibiwa tena kwa kiwango kikubwa ingawa mwaka 2007, Kamati ya Bomani ilitoa maoni na mapendekezo kadhaa yaliyohusu sekta ya madini ingawa maoni hayo hayakufanyiwa kazi,”alisema.

Kwa mujibu wa taarifa hiyo, kukiri kosa ni uungwana na kwamba CCM wanatakiwa kujitokeza hadharani na kuwaomba radhi Watanzania, kuwa hawakuwatendea haki kutokana wizi uliokuwa ukifanyika katika sekta ya madini.

Pamoja na hayo, Danda aliiomba Serikali kuhakikisha inachukua hatua za kisheria kwa yeyote aliyeshiriki katika kuangamiza uchumi wa Taifa kwa kusaini mikataba mibovu katika sekta ya madini.

 NCCR-Mageuzi, tunafarijika kuona tuliyokuwa tukiyapigania kwa miaka mingi, yanaendelea kufichuliwa waziwazi  na ukweli unazidi kubainika kupitia kamati zilizoundwa na Rais.

“Pia ni muda muafaka wa kupitia upya sheria zote zinazohusu masuala ya madini na ni wakati muafaka wa wataalamu wazalendo kuipitia tena Katiba iliyopendekezwa kwa kuwa inatoa mwelekeo wa kuwadhibiti wabadhirifu,” alisema.

 

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here