BABA KORTINI KWA TUHUMA ZA KUWABAKA WATOTO WAKE

0
667

Na JANETH MUSHI-ARUSHA

JAPHET Legimani (37), mkazi wa Daraja Mbili, jijini Arusha, amepandishwa katika Mahakama ya Wilaya ya Arumeru mkoani Arusha kwa makosa ya kufanya mapenzi na watoto wake wa kuwazaa.

Mmoja wa watoto hao, ana umri wa miaka 14 na anasoma kidato cha kwanza na mwingine ana miaka 12 anasoma darasa la sita katika moja ya shule za msingi mkoani Arusha.

Mbele ya Hakimu Mkazi wa Mahakama hiyo, Patricia Kisinda, Wakili wa Serikali, Riziki Maayu, alidai mahakamani hapo kuwa mtuhumiwa huyo alitenda makosa hayo kati ya mwaka 2016 na 2017 kwa watoto wake hao.

Katika kesi ya kwanza, Legimani anadaiwa kufanya mapenzi na ndugu wa damu, kinyume na kifungu cha 158 (1) cha sheria ya kanuni ya adhabu ambapo katika tarehe tofauti mwaka 2016, katika maeneo ya Daraja Mbili, alifanya mapenzi na mtoto wake (jina linahifadhiwa), mwenye umri wa miaka 14 anayesoma kidato cha kwanza.

Katika kesi ya pili, Wakili Riziki alidai mahakamani hapo, kuwa Legimani anadaiwa kufanya mapenzi na ndugu yake wa damu ambapo katika tarehe tofauti, kati ya Januari hadi Mei mwaka huu, alifanya mapenzi na mtoto wake (jina linahifadhiwa) mwenye umri wa miaka 12 ambaye anasoma darasa la sita katika moja ya shule za msingi jijini hapa.

Mshitakiwa huyo, alikana kutenda makosa hayo na wakili huyo wa Serikali aliieleza mahakama hiyo, kuwa upelelezi bado haujakamilika na kuiomba mahakama ipange tarehe nyingine ya kutaja kesi hizo.

Hakimu Patricia alimweleza mshitakiwa huyo kuwa dhamana iko wazi ambapo alitakiwa kudhaminiwa na wadhamini wawili ambao ni waajiriwa wa taasisi inayotambulika na mahakama, ambapo kila mdhamini anapaswa kusaini dhamana ya Sh milioni 5.

Pamoja na hayo, alidai kwamba, kama mshtakiwa atafanikiwa kupata dhamana, hataruhusiwa kusafiri nje ya Arusha bila kibali cha mahakama hiyo.

Mashauri hayo yaliahirishwa hadi Juni 28 mwaka huu, yatakapotajwa tena huku mshitakiwa akirudishwa mahabusu baada ya kukosa wadhamini.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here