30 C
Dar es Salaam
Saturday, December 4, 2021

Nape: JPM anastahili tena kupeperusha bendera CCM

MWANDISHI WETU-DODOMA

MBUNGE wa Mtama, Nape Nnauye amesema Rais Dk. John Magufuli ametekeleza vizuri Ilani ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) na kwamba anastahili kupewa miaka mingine mitano.

Nape aliyepata kuwa Katibu wa Itikadi na Uenezi wa CCM, alitoa kauli hiyo bungeni jana wakati akichangia bajeti ya Ofisi ya Waziri Mkuu kwa mwaka 2020-21.

“Mheshimiwa Spika, mwaka 2015 CCM tulitengeneza ilani ya uchaguzi kwa kazi zitakazofanywa na Serikali ya awamu ya tano, tulipoikamilisha tukamtafuta mtu atakayefanya kazi tuliyoiweka kwenye ilani, wakati ule waliojitokeza ni watu wengi walioomba kazi hiyo.

“Lakini CCM tukamteua John Magufuli kuifanya kazi ya kuitekeleza ilani na hakuteuliwa kwa bahati mbaya, tuliona ana uwezo wa kufanya kazi tunayompa kwa sababu ni mtu mwenye uwezo, jasiri na mzalendo.

“Sina mashaka chama hiki kikifanya tathimini leo, ni wazi Magufuli ameifanya kazi vizuri na hivyo anastahili kupewa miaka mingine mitano ya kukamilisha kazi tuliyompa, lakini pia tumpe kazi nyingine kwa sababu amefanya kazi vizuri,” alisema Nape.

Alisema ilani hiyo ya mwaka 2015 ilimtaka atakayepewa kazi na Serikali yake afanye kazi ya kutafsiri ukuaji wowote wa uchumi autafsiri kwenye maisha ya kawaida ya Watanzania jambo ambalo nalo limefanyika vizuri.

“Kwa upande wa afya, tulitaka tusogeze hizi huduma za afya na kuziboresha. Katika kipindi cha miaka mitano vimejengwa vituo vya afya 352, kama uchumi usingekuwa una-perform isingewezekana kufanya kazi hii.

“Zimejengwa hospitali 67 za wilaya, tuna mikoa mipya ambayo ilikuwa haina hospitali za rufaa na  zimejengwa hospitali tatu za kanda.

“Kwa kazi hii sina mashaka chama changu tutampa fursa tena ya kuipeperusha bendera na sina mashaka Watanzania wameona tafsiri ya kukua uchumi kwenye huduma za afya.

“Kwa upande wa elimu zinatolewa Sh bilioni 24 kila mwezi kwa ajili ya elimu bure, kwenye umeme napo hali ni nzuri sana, zaidi ya vijiji 9,000 vimepata umeme, kama uchumi usingekuwa unaenda vizuri isingewezekana.

“Mimi kama mwenezi mstaafu wa CCM ambaye nilisimamia utekelezaji wa ilani ya uchaguzi, nasema kazi ilifanyika vizuri na tuna sababu ya kumpa tena fursa John Magufuli,” alisema Nape.

Vilevile alisema kwenye ilani hiyo walimpa Rais Magufuli kazi ya kubadilisha utamaduni wa mambo yanavyofanyika hapa nchini.

“Mfano mtu unaweza kupata kipato kikubwa, lakini hakilingani na kazi anayofanya, wakati mwingine kuna biashara hewa, kazi hewa, kwenye uchumi vyuma vinakaza, lakini kwa sababu wakati mwingine tulizoea dili, dili zikifungwa kwa vyovyote vile vyuma vitakaza tu, ndio maana itabidi tumpe tena fursa,” alisema Nape.

Alisema Rais Magufuli pia ameweza kubadili mwenendo wa siasa za hapa nchini na kwamba vyama kama Chadema na ACT Wazalendo walifanya uchaguzi wao wa ndani kwa umakini mkubwa.

“Tukienda kwenye siasa kuna kelele ndio, lakini ukienda Chadema, ACT namna walivyofanya uchaguzi wao wa ndani utaona kuna ‘serious’, utaona kuna mabadiliko ya namna tunavyoendesha siasa zetu.      

“Hata mitaani hali imebadilika kidogo watu wako ‘serious’, inawezakana kuna mapungufu, Mwalimu Nyerere alituambia kwamba ukiwa unasafisha nyumba unaweza ukafagia shilingi, sasa kufagia shilingi haifanyi nyumba isisafishwe… mapungufu ya hapa na pale katika kutengeneza mambo haya tunakanyagana vidole yatumike vizuri turekebishe mambo huko mbele,” alisema Nape.

Pia alilipongeza Bunge la 11 chini ya Spika Job Ndugai akisema yamefanyika mabadiliko ya namna ya uendeshaji, hasa pale ulipofanyika uamuzi wa kijasiri wa kuanzisha studio ya Bunge.

“Ushauri wangu ni kwamba nadhani ni vizuri tukaitengea fedha ya kutosha studio hii na isiwe nyuma kwenye mabadiliko ya teknolojia, vifaa vya kisasa vitolewe ili iweze kufanya kazi vizuri na si vibaya pia ikawa sehemu ya kanuni za kudumu za Bunge,” alisema Nape.

- Advertisement -
bestbettingafrica

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

66,457FansLike
167,968FollowersFollow
526,000SubscribersSubscribe
- Advertisement -
10Bet

Latest Articles