30 C
Dar es Salaam
Saturday, December 4, 2021

CAG eleza sababu deni la taifa kupaa

RAMADHAN HASSAN-DODOMA

RIPOTI ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) kwa mwaka ulioishia Juni 2019, inaonesha wizi katika walmashauri, deni la taifa kuzidi kupaa, pamoja na malipo ya mishahara kwa watumishi ambao wamefariki.

Akizungumza na waandishi wa habari muda mfupi baada ya kuwasilisha ripoti ya ukaguzi ya mwaka wa fedha 2018/19 bugeni Dodoma jana, CAG Charles Kichere alisema kuwa alifanya ukaguzi huo kwa taasisi za Serikali Kuu, mamlaka ya Serikali za mitaa, mashirika ya umma, miradi ya maendeleo na vyama vya siasa kwa mwaka wa fedha ulioishia Juni 30 mwaka jana.

Alisema alitoa jumla ya hati 1,082 za ukaguzi ambapo kati ya hizo, zinazoridhisha ni 1,017 (sawa na asilimia 94), zenye shaka ni 46 sawa na asilimia 4.25, zisizoridhisha ni saba sawa na asilimia 0.64) na mbaya ni 12 sawa na asilimia 1.11.

MAKUSANYO

CAG alisema katika mwaka wa fedha ulioishia Juni 30 mwaka jana, Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA)  ilikusanya kiasi cha Sh trilioni 15.74 kati ya makisio ya Sh trilioni 18.29, hivyo kutofikia malengo kwa kiasi cha Sh trilioni 2.55 sawa na asilimia 14.

Alisema jumla hii ya makusanyo haihusishi Sh bilioni 20.05 za vocha za misamaha ya kodi na fedha za marejesho ya kodi kutoka Hazina.

Mapato halisi ya mwaka wa fedha 2018/19 (yakijumuisha vocha za misamaha na marejesho ya kodi) ni Sh trilioni 15.76.

“Ukilinganisha na makusanyo halisi ya mwaka uliopita (2017/18) ambayo ni Sh trilioni 15.40, kuna ongezeko la Sh bilioni 360 sawa na asilimia mbili,” alisema CAG.

DENI LA SERIKALI LAZIDI KUPAA

Alisema kufikia Juni mwaka jana deni la Serikali lilikuwa Sh trilioni 53.11 ambapo deni la ndani lilikuwa Sh trilioni 14.86 na deni la nje Sh trilioni 38.24 ikiwa ni ongezeko la Sh trilioni 2.18 sawa na asilimia nne ikilinganishwa na deni la Sh trilioni 50.93 lililoripotiwa tarehe 30 Juni, 2018.

“Ongezeko la deni limesababishwa na riba ya mikopo, mikopo halisi na kushuka kwa thamani ya shilingi,” alisema CAG.

UDHAIFU UOKOAJI WA MALIPO

Alisema katika ukaguzi wake alibaini majalada 338 kati ya 3,448  yaliyokuwa yamekokotolewa kimakosa, kati ya hayo, 170 yalikuwa na zaidi ya kiwango stahiki kwa Sh milioni 316.12  na 168 yalikuwa na kiwango pungufu kwa Sh milioni 433.57.

“Kutokana na udhaifu huo, Serikali ingepata hasara ya Sh milioni 316.12 kutokana na kuzidishwa kwa mafao, pia wastaafu wangelipwa kiasi pungufu cha shilingi milioni 433.57,” alisema CAG.

MALIPO KWA WATUMISHI WAFU

Alisema ukaguzi wa malipo ya mishahara alioufanya katika Jeshi la Polisi ulibaini kiasi cha Sh milioni 196.13 kilicholipwa kwa watumishi 11 ambao walikwishafariki, kufukuzwa kazi au kustaafu kinyume na matakwa ya kanuni ya 113 (3) ya Kanuni ya Fedha za Umma ya mwaka 2001.

MANUNUZI BILA MIKATABA

Pia alisema katika mwaka wa fedha 2018/19 alibaini kuwa taasisi tano za Serikali Kuu zilifanya manunuzi yenye thamani ya Sh bilioni 5.46 pasipokuwa na mikataba.

Alisema alibaini Mahakama ya Tanzania ilifanya malipo ya awali kwa mkandarasi ya kiasi cha Sh bilioni 4.83 kwa ujenzi wa mahakama 16, lakini mkandarasi alilipwa malipo ya ziada ya kiasi cha Sh bilioni 1.54 kwa vifaa kinyume na makubaliano ya mkataba.

“Pia, nilibaini kuwa ujenzi wa mahakama nne zinazojengwa Bunda, Kilindi, Katavi na Lindi ambazo zililipiwa malipo ya awali ya Sh bilioni 1.47 ulikuwa umesimama toka mwezi Septemba 2017,” alisema CAG.

Alisema alibaini dosari kwenye malipo yaliyofanywa na Jeshi la Polisi katika ujenzi wa majengo Sh milioni 806.69 katika kupitia malipo yaliyofanyika kwa ujenzi wa nyumba 400, mabweni na vyumba vya madarasa.

VIFAA AMBAVYO HAVIKUPOKEWA

Alisema taasisi saba za Serikali Kuu zilifanya ununuzi wa vifaa na huduma vyenye thamani ya Sh milioni 587.65 vilivyoagizwa na kulipiwa ambavyo havikupokewa kinyume na makubaliano ya mkataba.

CUF NA UTOAJI WA FEDHA

Aidha CAG alisema Chama cha Wananchi (CUF) kilipokea ruzuku kutoka serikalini kiasi cha Sh milioni 369.38 mnamo Januari 5 mwaka  2017.

“Nilibaini kuwa katika fedha hizo, chama kilihamisha Sh milioni 300 kutoka kwenye akaunti ya chama kwenda akaunti binafsi ya mwanachama mnamo tarehe 6 Januari, 2017 na kiasi cha Sh milioni 69 kilitolewa kama fedha taslimu. Hata hivyo, nyaraka za matumizi ya fedha hizo hazikuwasilishwa kwa ajili ya ukaguzi.

“Bodi ya Wadhamini ya CUF ilitoa mkopo wa Sh milioni 45 mnamo tarehe 3 Januari 2017 kwa kituo kimojawapo cha redio cha Mkoa wa Tanga kwa makubaliano ya kurejesha kwa kipindi cha miaka mitatu mpaka tarehe 03 Januari 2020.

“Aidha pia chama hicho kiliidhinisha na kutoa mkopo mwingine wa Sh milioni 35, Februari 16, 2018 kwa kituo hicho hicho cha redio kwa makubaliano ya kulipa kwa kipindi cha miaka miwili mpaka Februari 16, 2020,” alisema CAG.

SERIKALI ZA MITAA

Alisema katika mwaka wa fedha 2018/19, mamlaka 126 za Serikali za Mitaa zilipanga kukusanya mapato ya jumla ya Sh bilioni 463.95 kutokana na vyanzo vya ndani, mamlaka hizo zilifanikiwa kukusanya Sh bilioni 342.49 hivyo kuwa na upungufu wa Sh bilioni 121.46 sawa na asilimia 26 ya bajeti yote.

CAG alisema katika mwaka wa fedha 2018/19, mamlaka 182 za Serikali ya mitaa zilipokea jumla ya ruzuku ya maendeleo Sh bilioni 913.69.

WADAIWA SUGU

Aidha, alisema alibaini kwamba baadhi ya mashirika ya umma yana fedha nyingi ambazo zinashikiliwa na wadaiwa sugu.

Alisema kati ya mashirika 148 ambayo ameyakagua, amebaini 34 yenye wadaiwa sugu ambayo madeni yanafikia kiasi cha Sh bilioni 224.69.

Aliyataja mashirika ambayo ni wadaiwa sugu kuwa ni Mfuko wa Bima ya Afya, Mfuko wa Fidia kwa Wafanyakazi, Mamlaka ya Udhibiti wa Mawasiliano Tanzania, Shirika la Nyumba la Taifa na Kampuni ya Ubungo Plaza

- Advertisement -
bestbettingafrica

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

66,457FansLike
167,968FollowersFollow
526,000SubscribersSubscribe
- Advertisement -
10Bet

Latest Articles