23.8 C
Dar es Salaam
Sunday, October 13, 2024

Contact us: [email protected]

NAPE ALIAMSHA DUDE

*Serikali yamjibu hoja ya Stigler’s Gorge, ilani ya CCM

*Yagongelea msumari marufuku maandamano, Msajili apewa meno


Na FREDY AZZAH-DODOMA

DUDE limemshwa. Ndivyo unavyoweza kusema baada ya Serikali kumjibu Mbunge wa Mtama, Nape Nnauye (CCM), aliyedai kwa sasa inaelekeza nguvu nyingi kwenye mradi wa uzalishaji umeme wa maji wa Stigler’s Gorge, wakati haupo kwenye Ilani ya CCM ya mwaka 2015.

Nape alisema Serikali imeacha mradi wa gesi ambao ndio ulinadiwa wakati wa kampeni kwenye Uchaguzi Mkuu 2015.

Juzi akichangia hotuba ya makadirio na matumizi ya ofisi ya Waziri Mkuu kwa mwaka 2018/19, Nape alisema: “Bahati mbaya sana humu ndani (Hotuba ya Waziri Mkuu) hakuna kabisa kabisa (hoja ya gesi), maana yake ni kwamba hili jambo pengine limenza kuachwa sasa tuende kwenye Stigler’s, lakini je, hatusaliti Ilani ya Uchaguzi ya CCM?”

 

MAJIBU YA SERIKALI

Akichangia wakati wa kuhitimisha hoja hiyo jana bungeni mjini hapa, Waziri wa Nishati, Dk. Medard Kalemani, alisema mradi wa Stigler’s Gorge upo kwenye Ilani ya CCM na ndiyo maana unatekelezwa na Serikali.

Alisema Ilani ya Uchaguzi, haikuainisha mradi mmoja mmoja, bali imezungumzia vyanzo vya miradi ya umeme ambayo ni maji, gesi, upepo na makaa ya mawe.

“Haijataja mradi mmoja mmoja, imeeleza vyanzo vya umeme vitakavyoendelezwa ili tupate umeme wa uhakika mpaka tuweze kukaa hapa na kusema mwingine tuuzie majirani wetu,” alisema Dk. Kalemani.

Alisema katika kile kinachodhihirisha miradi ya gesi haijatelekezwa, hadi sasa megawati 787 za umeme unaotumika unatokana na nishati ya gesi.

“Na hii itaendelea kwa sababu mpaka 2020 pale Kinyerezi peke yake tutakuwa na megawati 1,560 zinazotokana na gesi pekee,” alisema.

Dk. Kalemani alisema mradi wa Stigler’s kwa sasa ni muhimu utekelezwe kwa kuwa utasaidia kuongeza kiwango cha umeme nchini na kuwa na uhakika na Tanzania ya viwanda.

Alisema pia mbali na ongezeko la umeme, jinsi mradi huo utakavyojengwa, utakuwa moja ya kivutio cha utalii na utasaidia miundombinu kama barabara za kwenda kwenye mradi huo kujengwa kwa kiwango cha lami.

Dk. Kalemani alisema pia kuhusu mradi wa kuchakata gesi asili (LNG), unaotarajiwa kujengwa kwenye mikoa ya Lindi na Mtwara, unaendelea na kwamba tayari eneo la mradi limeshapatikana na tathmini ya malipo kwa wananchi imekamilika.

“Kwahiyo namwomba ndugu yangu Nape aendelee kuhamasisha wananchi, miradi hii ya gesi haijatelekezwa, kinachofanyika ni kutafuta vyanzo mchanganyiko vya kuwa na umeme wa uhakika,” alisema Dk. Kalemani.

 

VYAMA VINAVYOVUNJA SHERIA

Naye Waziri wa Nchi Sera, Bunge, Kazi, Vijana, Ajira na Walemavu, Jenista Mhagama, akijibu hoja za wabunge waliochangia kwenye hotuba hiyo, pamoja na mambo mengine, alimtaka Msajili wa Vyama vya Siasa, kufuata ushauri aliopewa na Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Katiba na Sheria juu ya vyama vinavyovunja sheria.

Alisema mwaka 1992, wananchi walihojiwa juu ya wanaotaka vyama vingi ambapo asilimia 80 walikataa, lakini Serikali ikaamua kuruhusu mfumo huo jambo linaloonyesha CCM haiogopi ushindani.

“Demokrasia ya wachache waliotaka vyama vingi inaheshimiwa na wengi walioukataa, kwa haya niliyoyasema, inajidhihirisha nchi iliingia kwenye mfumo wa vyama vingi kwa ajili ya demokrasia, kwahiyo hakuna sheria inayomfanya Msajili wa Vyama kuvunja demokrasia na kufuta mfumo wa vyama vingi katika Tanzania.

“Ninamwomba Msajili wa Vyama aendelee kuchukua hatua stahiki kama Kamati ya Bunge ilivyoshauri kwa vyama vyote ambavyo havitaki kufanya shughuli zake kwa kufuata sheria na taratibu tulizoweka, ili kusaidia mfumo wa vyama vingi kwenye nchi yetu uwe halisia, ambao unaendana na matakwa ya kisheria.

“Kamati inashauri na kusisitiza kwamba ofisi ya Msajili wa Vyama vya Siasa ihakikishe kunakuwepo na usimamizi wa karibu kwa kufuatilia na kuchunguza mienendo inayoharibu sifa na vigezo vya vyama vya siasa nchini na kwamba Msajili asisite kufuta usajili wa chama chochote cha siasa kitakachokiuka sheria, kanuni na taratibu za uendeshaji wa vyama vya siasa,” alisema Mhagama.

 

MAANDAMANO

Katika hatua nyingine, Mhagama alizungumzia suala la maandamano akisema wabunge wa upinzani wamelalamika wakisema ni suala la kikatiba na kwamba wanafikiri kuna msingi wa kuwaachia waendelee kuandamana bila kufuata sheria.

Alisema maandamano yanaratibiwa kwa sheria ya usalama chini ya polisi, na Katiba haiwezi kuchukuliwa tu kuruhusu maandamano bila sheria kufuatwa.

“Naomba Watanzania wahakikishe wanafuata sheria, Katiba imeruhusu maandmano lakini yanaratibiwa kisheria. Niulize tu, tukiamka hapa siku moja asubuhi kila mtu aamue kuandamana kwa sababu Katiba imesema, nadhani haitakuwa sawa. Naomba vyama viheshimu Katiba na sheria,” alisema.

 

 Kwa habari zaidi jipatie nakala ya gazeti la MTANZANIA.

 

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
590,000SubscribersSubscribe

Latest Articles