24.6 C
Dar es Salaam
Monday, October 14, 2024

Contact us: [email protected]

MTU NA MKEWE WAKUTANA KWA MAKONDA

JOHANES RESPICHIUS Na TUNU NASSOR-DAR ES SALAAM


NI zamu ya wanaume sasa. Ndivyo hali inavyoonekana baada ya wanaume zaidi ya 10 kuibukia katika Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda kufikisha kilio chao cha kupokwa watoto.

Hali hiyo imetokea huku mamia ya wanawake wanaodai kutelekezewa watoto wakiendelea kumiminika kwenye ofisi hizo.

Wanaume hao walifika jana katika ofisi hizo na kudai hawashindwi kulea watoto, isipokuwa wazazi wenzao wamewapoka kwa madai ya umasikini.

Walisema kama Makonda ameamua kuwasaidia wanawake, basi ajue wapo wanaume wanaolia kunyanyaswa na wenza wao.

“Mimi mke wangu alinikimbia nilipougua miguu kiasi cha kushindwa kutembea, aliondoka na watoto wangu wote watatu, nimekuwa mtu wa mawazo kiasi cha kupata vidonda vya tumbo, naomba awarudishe,” alisema Tito Chemba.

Chemba (35), ambaye ni mkazi wa Kijichi, Dar es Salaam,  alisema ujio wake kwa Makonda ni kutaka kurejeshewa wanawe wanaoishi Bukoba kwa ndugu wa mkewe.

Naye Edmond Mbisho, alisema mkewe aliondoka na mtoto wake tangu akiwa na miaka mitatu na sasa ana miaka sita.

“Sina la zaidi hapa, ninachotaka kujua ni namna gani nitampata mwanangu, si kingine. Kwa sasa mwanamke anaishi na mtu mwingine. Lengo lake anataka nionekane nimeshindwa kulea mwanangu, kwa hili hapana, sikubali hata kidogo,” alisema.

Naye Vedasto Mdesa mkazi wa mkoani Iringa, alisema watoto wake watatu waliozaliwa kwa pamoja walichukuliwa na ndugu wa mkewe na kupelekwa nchini Urusi.

“Nilinyang’anywa watoto wangu kisa mimi ni masikini, hivi sasa naishi kwa tabu na sababu kubwa ni umasikini na wanasema sijasoma. Mwanamke niliyezaa naye ana shahada na mimi ni mpigapicha nisiye na elimu,” alisema.

 

WENZA WAKUTANA

Hata hivyo, wakati usajili ukiendelea kwa watu wenye matatizo mbalimbali, katika hali isiyokuwa ya kawaida, wazazi wawili walikutana ana kwa ana.

Katika tukio hilo, mwanamke Sylvia Felisiano alifika katika viwanja vya ofisi ya Makonda, baada ya kusikia mume wake, Chemba, amekwenda kulalamika amemkimbia na watoto wao watatu.

Mwanamke huyo alidai alipata taarifa hizo kupitia mitandao ya kijamii na kuamua kufika katika ofisi hizo ili kujua hoja ya mzazi mwenzake huyo.

“Nimekuja hapa kusikiliza, anasema nimemkimbia, sasa nimekuja kumsikiliza hapahapa nini hoja yake,” alisema Sylvia.

Baada ya kufika eneo hilo, alipelekwa moja kwa moja kwa maofisa wa ustawi wa jamii na wanasheria waliopiga kambi kusikiliza kero hizo za kifamilia.

Akizungumza baada ya kusikilizwa kwa shauri lao, Chemba, alisema walipoitwa alisema mzazi mwenzake alikuwa anataka kuuzwa kwa mali.

“Wakati ninamuoa alinikuta nikiwa tayari nimeandaa mazingira ya kuishi watoto wangu, ambayo ni nyumba na shamba, hivyo ni mali ya wanangu,” alisema Chemba.

Aliongeza iwapo Sylvia atahitaji kurudi nyumbani kulea watoto, arudi lakini hatakuwa kama mkewe na asimbughudhi mkewe aliyenaye sasa.

 

LOWASSA AZULIWA JAMBO

Mkazi wa Kigamboni aliyejitambulisha kwa jina la Fatuma Lowassa (31), alimwaga machozi mbele ya Makonda akidai kutelekezwa na baba yake, Waziri Mkuu wa zamani, Edward Lowassa.

Alisema yupo tayari kupima kipimo cha DNA na Lowassa kuthibitisha hilo.

“Nimejaribu sana kutafuta ufumbuzi wa suala hili kwa miaka mingi, nilipeleka barua Ikulu kuomba kuonana na baba kipindi akiwa Waziri Mkuu, lakini niliitwa na mama katika Klabu ya Momba iliyopo Kinondoni.

“Alikuja mwanaume akiwa kwenye gari lenye ‘tinted’ akatuhoji mimi na mama akaondoka, hakutupa majibu yeyote,” alisema Fatuma.

Alidai kuwa aliwahi kukutana na Fredy Lowassa na akamuahidi kumsaidia, lakini hadi sasa hakuna mrejesho.

Kwa upande wake, Makonda alimtaka Fatuma kwenda na mama katika ofisi hiyo ili wapate msaada.

MTANZANIA ilimtafuta Fredy, ambaye alijibu kwa kifupi: “Paul Makonda nimemlea, nasikitia sana anapozidi kumkashifu na kumsumbua mzee (Lowassa).

“Nasikitika sana, huyo ni kijana wangu, anajua, lakini hata mimi angenipa heshima tu. Kama ana shida anisumbue mimi, lakini si mzee. Huu ndio ujumbe wangu kwa Makonda.”

 Kwa habari zaidi jipatie nakala ya gazeti la MTANZANIA.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
590,000SubscribersSubscribe

Latest Articles