27.2 C
Dar es Salaam
Wednesday, July 24, 2024

Contact us: [email protected]

Nani atategua fumbo la Edward Sokoine

pix coverNa Balinagwe Mwambungu

NI miaka 32 sasa tangu Tanzania impoteze Edward Moringe Sokoine. Ingefaa sasa wanaojua siri za kifo chake kutokana na ajali ya gari iliyotokea pale Dakawa, mkoani Dodoma, wakajitokeza na kueleza ukweli, ili kuiweka historia sawa. Tanzania inaweza kuingizwa katika kitabu cha kumbukumbu—Guiness  Book of Records—kwani si jambo la kawaida Waziri Mkuu kugongwa na gari akiwa kwenye msafara!

Hii inatokana na ukweli kwamba Wananchi wengi hawakuamini kwamba Sokoine alikufa kwa ajali ya gari kwa kuwa wanajua utaratibu wa msafara wa kiongozi kama Waziri Mkuu.

Kukawa na hoja nyingi tu ambazo badala ya kujibiwa, ikatolewa marufuku ya kuendelea kuhoji kifo cha Sokoine.

Kwa kipindi nilichokuwa nafanya kazi Daily/Sunday News, ziliwahi kutolewa marufuku nne kutoka Ikulu. Marufuku ya kwanza ilikuwa hii ya kifo cha Waziri Mkuu Edward Sokoine. Hii ilitokana na taarifa kuvuja kwamba Daily/Sunday News walikuwa wanajipanga kuzama kiundani zaidi na kujiridhisha kwamba kweli Sokoine alikufa kuokana na ajali?

Kwa nini waandishi walikuwa na shaka kuhusu kifo cha Sokoine? Ilitokana na ukweli kwamba akiwa Waziri Mkuu, alisimamia utekelezaji wa amri yaRais Mwalimu Julius Nyerere ya kupambana na wahujumu uchumi. Sokoine kama Waziri Mkuu, ndiye alikuwa kinara wa kusimamia utekelezaji wa amri hiyo.

Watu wengi walikamatwa kwa makosa ya kuhodhi au kulangua bidhaa mbali mbali. Kampeni hiyo ilichagizwa zaidi na Radio Tanzania Dar es Salaam (RTD) kupitia kipindi cha Mazungumzo Baada ya Habari,  na ‘Tuambie wako wapi, ni akina nani na wanafanya nini’—vipindi hivyo viliwatia hamasa wananchi kutoa taarifa kwenye mamlaka husika.

Lakini taarifa nyingine hazikuwa sahihi na zilisababisha watu wengine wasio na hatia kuswekwa rumande na kuachiliwa baada ya uchambuzi wa kina. Ukweli ni kwamba watu waliumia, hasa wafanyabiashara. Kwa hiyo baada ya kikundi cha watu wenye ushawishi waliojenga chuki dhidi ya Edward Sokoine.

Pia baadhi ya wanasiasa na viongozi wa Serikali walitikiswa na operesheni hiyo kwa sababu ya kutoa vibali vya kununua bidhaa kutoka maduka ya umma (RTCs) na  National Milling Corporation (NMC) na Shirika la Ugawaji—National Distributers (NDL). Mmoja wapo alikuwa Edward Barongo (RIP), ambaye wakati huo alikuwa Mkuu wa Mkoa wa Kilimanjaro. Barongo aliachiwa baadaye kwa amri ya Ikulu.

Lakini pia kulikuwa na kikundi kidogo cha wateule wa Mwalimu ambao walikuwa wanashukiwa kwamba walikuwa ‘majipu’ na  Sokoine alitaka lakini Mwalimu Nyerere akaweka ‘Stop’.

Jambo hili lilimwudhi Sokoine kwa vile aliona kwamba kumbe ‘operesheni wahujumu uchumi’

Ilikuwa ya kibaguzi. Kwa hasira akapanda ndege kuelekea Arusha na alipofika kule taarifa zinasema akawaambia walinzi na wasaidizi wake kwamba warudi Dar es Salaam na ndege hiyo ya Serikali na kwamba atawapa taarifa pindi atakapowahitaji.

Edward Lowassa, ambaye alikuwa mgombea wa urais katika Uchaguzi Mkuu wa Oktoba mwaka jana, bila kujua alirudia maneno ya mtangulizi wake Edward Sokoine aliposema: ‘Nitakwenda kuchunga ng’ombe Monduli.’

Kwa hiyo, Sokoine baada ya oparesheni wahujumu uchumi, alikwena kuchunga ng’ombe Monduli na kususa cheo cha Waziri Mkuu. Nchi ilibaki bila Waziri Mkuu kwa kipindi. Taarifa zilieleza kwamba Mwalimu alimtumia ujumbe mara kadhaa kwamba arudi Dar es Salaam, lakini alikataa hadi alipotumwa Makamu wa Rais Aboud Jumbe na kumshawishi kuendelea na kazi.

Rais Mwalimu Nyerere alisoma ‘mood’ ya wananchi, Sokoine alikuwa amejijengea uhalali wa kuwa sauti ya wanyonge, alisimama kidete kupinga dhuluma na alikuwa mzalendo kweli. Anapenda kufuatilia malalamiko ya wanancchi yeye binafsi kama afanyavyo Waziri Mkuu wa sasa.

Sokoine hakuwa rafiki wa wazembe na maofisa wasiotimiza wajibu wao. Ofisini kwake pale Magogoni pembezoni mwa Ikulu walimpa jina la ‘Bwana Siku Saba’. Akimpa kazi ofisa, alikuwa anampa siku saba kuleta mrejesho ndani ya siku saba. Kama ametumwa kutatua tatizo mkoani, ni lazima apeleke majibu ndani ya siku saba.

Sokoine alikuwa mtu mpole ingawaje umbo lake liliwatisha watu wengine. Alizungumza kwa upole, lakini alikuwa anamaanisha kile alichokuwa anakisema.

Siku moja Mwandishi wa Shirika la Habari Tanzania (SHIHATA) mkoani Iringa, aliripoti kwamba pembejeo za kilimo kwa ajili ya ‘the big four’ mikoa ya Ruvuma, Iringa, Mbeya na Rukwa, zilikuwa hazijasambazwa na msimu wa kilimo ulikuwa umekwishaanza. Pembejeo zilikuwa zimefungiwa kwenye maghala pale Makambako. Wakuu wa mikoa ya Ruvuma Lawrence Gama na Athuman Kabongo, wakamlaani Mwandishi na kwamba aliandika habari za uongo. Habari hiyo ilichapishwa na Daily News.

Zamani watumishi wa Serikali walikuwa wanafanya kazi hadi Jumamosi saa sita na nusu. Habari za ndani ya Ofisi ya Waziri Mkuu zikatufikia kwamba mchana ule Sokoine ataondoka kwenda Iringa, lakini isitangazwe hadi saa saba siku ya Jumapili.

Waziri Mkuu alifika Makambako bila hata Mkuu wa Mkoa, Mkuu wa Polisi wala Afisa Usalama wa Mkoa hawakupewa taarifa hadi msafara ulipopita Ipogolo, Iringa kwamba Waziri Mkuu anaelekea Makambako. Watu wanafikiri ziara za kustukiza amegundua Rais John Magufuli, ndio zilikuwa zake Edward Sokoine.

Maofisa wa Serikali walifika mahali kwa sababu zao wenyewe, walikuwa wanatoa taarifa za uongo (yamemkuta Anne Kilango Malecela). Sokoine alipenda kuthibitisha mwenyewe. Siku moja Waziri Mkuu alimwita Waziri wa Kilimo, Profesa John Machunda, ampelekee taarifa ya hali ya chakula nchini. Waandishi wa habari tukaitwa kwa Waziri Mkuu.

Waziri Machunda akaanza kusoma taarifa yake. Alipoanza kutaja mikoa kwa mkoa, Waziri Mkuu akamwambia ‘Stop’ na kumweleza kwamba taarifa yake haikuwa linganifu na taarifa aliyokuwa nayo, kama vile Waziri Mkuu Kassim Majaliwa alivyomuumbua aliyekuwa Kamishina Mkuu wa TRA. Sokoine akamwamuru Prof .Machunda akalete taarifa sahihi ndani ya siku saba.

Umewahi kumwona Waziri aliyechanganyikiwa? Machunda aliondoka huku amelowa shati. Akasahau kuwa alikwenda kwa Waziri Mkuu kwa Shangingi, akaanza kurudi Pamba House kwa miguu. Dereva wake akawa anamfuata kwa gari huku akimpigia honi bosi wake, lakini akawa hasikii.

Kutokana na habari ya pembejeo Makambako, ambapo alishuhudia mwenyewe kwamba ikikuwa imerundikwa pale, Sokoinie akaanza kuviamini vyombo vya habari. Lakini wakubwa, hasa wakuu wa mikoa na mawaziri, walikuwa wanapenda kumpelekea taarifa nzuri nzuri tu. Sokoine akaihamishia Idara ya Habari (Maelezo) kuwa chini ya Ofisi ya Waziri Mkuu.

Ni Waziri Mkuu pekee ambaye amewahi kufanya sherehe ya kuaga mwaka na wahariri na waandishi wa habari pale Ikulu mwanzoni mwa mwaka 1984.  Naikumbuka sana sherehe ile, kumbe alikuwa anatuaga!  Aprili 12, 1984, Edward Moringe Sokoine alituacha.

Je, ile ilikuwa ajali au ilikuwa ajali ya ‘kutunga’? Dumisani Dube alitaka kuja kusafisha jina lake, lakini akarudishiwa Uwanja wa Ndege wa Dar es Salaam. Kwa nini?

Ni miaka 32 imepita,Watanzania bado hawana majibu ya kifo cha Edward Moringe Sokoine.

 

 

 

 

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
589,000SubscribersSubscribe

Latest Articles