27.5 C
Dar es Salaam
Friday, March 29, 2024

Contact us: [email protected]

Kuna haja kurudiwa Tume ya Warioba kupambana na rushwa

Judge-Joseph-Sinde-WariobaMIAKA michache nyuma, ingawa sasa inaonekana kama zamani za kale, palitokea kuwapo kwa Tume ya Warioba ya Kupambana na Rushwa. Tume hiyo iliundwa na Rais Benjamin Mkapa na iliongozwa na Jaji Joseph Sinde Warioba mmoja wa Watanzania waliojijengea sifa kubwa ya uaminifu, uadilifu na uzalendo.

Tume hiyo ilikuja na mapendekezo kadhaa siyo tu yaliyoonekana mazuri bali pia muhimu katika vita hivyo na kwa hakika watu wengi waliingia matumaini kuwa huo labda ungekuwa kama mwarobaini wa kupambana na adui mkubwa wa taifa lolote, rushwa.

Hatua kadhaa zilichukuliwa hapa na pale, sheria mbili tatu zikabadilishwa, lakini pia kukawepo kazi pana ya kikademia ambapo wataalamu wa siasa, sheria, saikolojia na sayansi ya jamii wakafanya uchambuzi na kuandika makala kadhaa wa kadhaa.

Tena wakati huo Tume ya Warioba iliundwa huku rushwa ikiwa bado ni tatizo dogo na ilikuwa kama vile ni “rushwa ya chai na andazi” na ilionekana kwa mwelekeo wa tume hiyo inaweza kuizuia rushwa kubwa ambayo bichwa lake lilikuwa ndio kwanza linajitokeza.

Ila inaonekana kuwa baada ya muda mdogo tume hiyo ikakunjwa kunjwa na kutiwa kabatini na ndio ikawa mwanzo wa rushwa kubwa kushamiri kwa sababu sio tu hakuna hofu ya Mungu lakini pia hofu ya sheria na Serikali ikaanza kumomonyoka pia.

Tamaa, hasadi, kukosa uzalendo vikawa vitu vya kawaida kabisa na jamii ikawa inashangilia kabisa na kumuenzi na kumtukuza mtu ambaye anaiibia Serikali au yule ambayo anapata ujasiri wa kupata utajiri kwa haraka. Kuiba na kufisidi bila kimeme au kiwewe ikawa ni jambo lililoanza kuota mizizi haraka na Tanzania ikaanza kuingia katika rubaa mbovu kimataifa.

Na kwa kweli tokea muda huo Tanzania imebaki  kutajwa katika jina baya la nchi zilizooza kwa rushwa na kuharibu sifa ya kisiasa, kiuchumi, kimkakati na hata ya kiwekezaji.  Rushwa imezama katika jamii hadi sasa imekuwa ni kama utamaduni na maisha ya kawaida ya Mtanzania.

Mtu kunyoya Serikali bilioni 6  hadi kumi, mtu kudanganya na kufilisi mali za umma kwa kiwango cha kutisha si tatizo, kusikia magari 500 yamepita bila ushuru si jambo la kushangaza, kuambiwa kuwa makontena 3,000 yametoka bandarini bila ya mapato yoyote au kusikia meli 65 zimepakua mizigo lakini hata moja haijalipa ushuru halimshangazi tena Mtanzania.

Wala Mtanzania wa leo kukamatwa na rushwa au kushtakiwa hakumshitui, ila huwa kama shujaa mbele ya jamii. Kutjirika ndio suala kuu bila  kujali utajiri huo unapatikanya vipi, hata iwe ni kwa kuwakosesha watu dawa, elimu au huduma yoyote ya lazima.

Serikali ya Jakaya Kikwete hadi sasa tumeingia ya John Pomb5e Magufuli zimejaribu kuziba mianya ya njia zote, lakini bado mchwa wanapenya nya kuharibu mali ya umma. Ubaya zaidi ni kuwa hakuna woga hata wa senti tano.

Hali sasa imekuwa ya kutisha kiasi ambacho huwezi kuamini kuwa hakuna chochoro ya wizara, taasisi hata moja ambayo haibomolewi na rushwa kiasi ambacho mwaka jana baadhi ya wafadhili walitishia kukata misaada yao ikiwa hatua madhubuti ya kupambana na rushwa hiyo hazitachukuliwa.

Ndio maana ikanijia fikra Je, kuna haja ya kuipitia upya ripoti ya Tume ya Warioba ya Kupamban na Rushwa au kuna haja ya kuunda Wariobta ll maana kwa hali inavyokwenda inaelekea jahazi linakwenda mrama kama hata nahodha hajui cha kufanya bali anapambana huku na kule.

Hadi sasa hakuna mwelekeo kuwa nchi ndio inayoshinda katika vita hii, ila ukweli ni kuwa kuna dalili nyingi kuwa rushwa na ufisadi ndio unaoshinda. Hatua za karibuni za kufikisha vigogo mahakamani zinatia moyo kidogo lakini wengi hawaamini kuwa mashtaka hayo yatakwenda hadi mwisho kuwatia hatiani waliotuhumiwa.

Rushwa lazima ipambanwe kwa imani kubwa. Mwananchi anatakiwa aamini kuwa kila mtu yuko chini ya sheria. Anataka aone mifano, hatua na uamuzi imara wa kumpa moyo maana kwa sasa imani ni ndogo sana kiasi ambacho watu wamediriki kusema kuwa hata hao wadogo na kidogo basi  hukumu zao ziwe za vifo.

Hilo halitawezekana kwa sasa kwa sababu sheria zetu hazina hukumu za vifo kwa makosa ya ufisadi kwa sasa lakini sheria inaweza kufanyiwa marekebisho au basi hata hizo adhabu ndogo zilizopo sasa ziwe zinaheshimwa na kupewa kila aliyetiwa hatiani bla kujali hadhi yake katika jamii au kifedha.

Vinginevyo  basi tuikumtie vumbi  ripoti ya Tume ya Warioba ya Kupambana na Rushwa walau tupate fikra mpya maana hatuwezi kwenda kama tunavyokwenda kwa kudhani kuwa hatuna hata mwongozo katika suala hili.

Lazima tujipange kama nchi wakati tukisema tunaelekea katika uchumi wa viwanda na kipato cha kati la sivyo safari itatushinda njiani na kwa kujidhuru wenyewe.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
585,000SubscribersSubscribe

Latest Articles