27.9 C
Dar es Salaam
Monday, June 24, 2024

Contact us: [email protected]

Naftal: Bado naamini nilishinda Jimbo la Kwela 2015

pix pg 14JOHANES RESPICHIUS

JINA la Daniel Naftal huenda ni geni masikioni mwa wengi. Huyu ndiye aliyekuwa mgombea ubunge katika Jimbo la Kwela (Chadema), Sumbawanga  mkoani Rukwa katika Uchaguzi Mkuu wa mwaka jana.

MTANZANIA limefanya mahojiano ya ana kwa ana na Naftal ambapo pamoja na mambo mengine anasema alishinda ubunge katika Jimbo la Kwela lakini alinyang’anywa haki yake.

SWALI: Hebu tueleze historia yako ya kisiasa  kwa ufup

JIBU: Kwanza nilianza kupenda siasa nikiwa katika masomo yangu pale Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), baada ya kumaliza masomo yangu nilijiunga na Chadema.

Baada ya hapo nilifanikiwa kufanya kazi katika ofisi ya vijana Chadema Makao Makuu kama Afisa Fedha na Utawala kuanzia mwaka 2010 hadi 2014.

Baadaye nilitamani zaidi kuwatumikia wananchi na hapo ndipo nilipoamua kushiriki mchakato wa kutafuta wagombea ndani  ya chama na baada ya kuchaguliwa kwa wingi na wanachama, ndipo safari yangu ya kisiasa ilipoanza kukua na kuingia rasmi kwenye kinyanganyiro cha Ubunge katika Jimbo la Kwela.

SWALI: Unauzungumziaje mchakato wa uchaguzi mkuu kwa upande wako?

JIBU: Bado naamini kuwa nilishinda katika uchaguzi ule na wananchi wa Jimbo la Kwela wanaamini hivyo kwani tangu Oktoba 25 hadi 30, Kata 26 kati ya 27 nilikuwa niko mbele kwa kupata kura 1700 dhidi ya mgombea wa CCM wakati wakisubiri Kata ya Milepa ambayo ilikuwa haijapiga kura kutokana na kuchomwa kwa masanduku ya kupigia kura.

Kutokana na sintofahamu iliyojitokeza ya kuchomwa kwa masanduku ya kupigia kura ndilo jambo ambalo nilikuwa na shaka nalo juu ya uhalali wa masanduku hayo kuhusika katika kata ile.

Wasiwasi wangu; yalikuja kujidhihirisha kuwa ni ya kweli kwa sababu mgombea wa CCM anatoka kwenye kata ile na jambo lingine la kisikitisha ni kwamba uchaguzi wa Rais uliendelea wakati wa ubunge na diwani ulisitishwa.

Swali ambalo nimekuwa nikijiuliza ni kwamba masanduku ya kura za rais hayakuchomwa lakini ya mbunge na diwani ndio yalichomwa? Wakati yote yalikuwa yamebebwa kwenye gari moja.

Kutokana na sintofahamu iliyotokea ilisababisha CCM kuonekana imeshinda kwenye kata hiyo kwa kura 2400 juu ya Chadema iliyopata kura 1116 na kwamba kutokana na matokeo hayo, Chadema ilikuwa inashinda uchaguzi huo kwa kura zaidi ya 400 kutokana na yale ya kata 26 lakini mkurugenzi alimtaja mgombea wa CCM kuwa mshindi.

Baada ya kufuatilia tulibaini matokeo aliyokuwa anayatangaza mkurugenzi hayakuwa yanaendana na yale ya vituoni, baada ya ubishani mkubwa mkurugenzi aliamua kumtangaza Aloyce Ignace Malocha kuwa Mbunge wa jimbo hilo.

Kitendo cha Malocha kutangazwa kuwa mbunge lilisababisha chama chetu kwenda mahakamani kufungua kesi ya kulalamikia utofauti wa matokeo.

Siku chache baada ya kesi hiyo kufunguliwa Mahakama iliondoa shauri hilo kutokana na Chadema kushindwa kulipa kwa wakati gharama za kuendeshea kesi.

SWALI: Nini matarajio yako kisiasa kwa siku zijazo?

JIBU: Lengo la kugombea ubunge lilikuwa kuwasaidia wananchi wa Jimbo la Kwela, lakini bado nina nia hiyo na nitagombea ubunge katika Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2020 Mungu akinijalia uzima.

Nitagombea tena kwa sababu ndoto yangu ni kuwatumikia wananchi wa Kwela na ninaamini kupitia siasa jimbo hilo litaweza kuwa sehemu salama ya kuishi tofauti na ilivyo sasa.

Kwa sasa ninashirikiana na wananchi wa jimbo hilo kutatua matatizo yanayowakumba kupitia madiwani na kambi rasmi ya upinzani bungeni. Nipo kwenye maandalizi mazuri ya kujitengenezea mtandao ndani ya chama ili kufanya dira yetu ya Chadema inatekelezwa.

SWALI: Unadhani ni kwanini CCM kinaendelea kubaki madarakani?

JIBU: Kwanza vyama vya upinzani vimekuwa na changamoto kubwa kutokana na CCM kutojiandaa kisaikolojia kukubali ushiriki wa siasa za vyama vingi.

CCM wamekuwa wazito sana kukabidhi madaraka hata pale wanapoonekana wameshindwa na upinzani. Mfano majimbo ambayo vyama vya upinzani vinashinda kunakuwa na ucheleweshwaji wa matokeo na Jeshi la Polisi kutumia nguvu nyingi.

Ndio maana hata kwenye uchaguzi wa halmashauri na majiji sehemu ambayo CCM wana idadi kubwa ya madiwani hakuna urasimu wowote unaotokea tofauti na sehemu za vyama vya upinzani mfano ni Uchaguzi wa Meya wa Jiji la Dar es Salaam.

Hivyo siamini kama CCM wanaamini kuwa njia mojawapo ya wao kuondoka madarakani ni sanduku la kura na hata yanayoendelea huko Zanzibar ni kutoamini kwao.

SWALI: Unaizungumziaje kasi ya Rais John Magufuli?

JIBU: Binafsi natofautiana na wengine kimtazamo kuhusiana na serikali ya Magufuli kwa sababu hakuna kitu kipya ambacho imekifanya ambacho hakijawahi kuzungumzwa na upinzani

Tangu mwaka 2010 hadi 2015 Chadema kimekuwa chama kikuu cha upinzani na kila hotuba yake bungeni ilikuwa ikisisitiza kupunguza matumizi yasiyo ya lazima, ununuzi wa magari ya kifahari na mambo mengine mengi na ndicho kinatendeka sasa hivyo unaweza kusema kuna jambo jipya hapo.

Chadema kwa kipindi kirefu imekuwa ikizungumzia serikali ya awamu ya nne kughubikwa na rushwa jambo ambalo lilikuwa likiungwa mkono na ripoti ya Mkaguzi na Mdhibiti wa Hesabu za Serikali (CAG) kila mwaka japo hakuna hatua yoyote iliyokuwa ikichukuliwa.

Chadema haipingi anachokifanya Rais Magufuli inaunga mkono hususani katika kupunguza matumizi ya serikali na kupambana na rushwa. Namshauri Rais Magufuli asiishie kwenye kutumbua vijipu vidogo bali aguse majipu makubwa ambayo hayajaguswa ili kudhihirisha dhamira yake kama ni kweli katika kuleta maendeleo nchini.

SWALI: Kutokana na kasi hiyo ya Rais Magufuli, unadhani Chadema bado inayo nafasi ya kushika dola katika uchaguzi ujao?

JIBU: Bado naamini kuwa Chadema kupitia Ukawa, inayo nafasi ya kuongoza nchi kwenye uchaguzi ujao kutokana na kukua na kuimarika kwa vyama vya upinzani na kufanikiwa kupatya nafasi ya kuongoza halmashauri mbalimbali pamoja na majiji makubwa jambo ambalo halikupata kutokea huko nyuma.

Kwa hiyo wananchi watatupima kupitia nafasi muhimu walizotupa, sina shaka halmashauri na majiji tuliyoyapata yatakuwa chachu ya utekelezwaji wa sera tulizokuwa nazo kwenye ilani yetu ya 2015 kama vile elimu, afya, kilimo pamoja na kusimamia vizuri fedha za umma.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
588,000SubscribersSubscribe

Latest Articles