23.3 C
Dar es Salaam
Saturday, April 20, 2024

Contact us: [email protected]

Viongozi wa Afrika na kauli za ‘Never Again’

Paul KagameAprili 7, 1994.  Miaka 22 iliyopita.  Kwa wananchi wa Rwanda pamoja na Waafrika wanaofuatilia masuala ya bara hili, hiyo si siku ya kuisahau hata kidogo.

Ni siku ambayo mauaji ya zaidi ya watu laki nane, wengi wao wakiwa Wanyarwanda wenye asili ya Kitusi, walianza kuuawa na Wahutu wenye msimamo mkali.  Yanajulikana kama mauaji ya Kimbari ambayo yalitikisa Afrika na ulimwengu kwa ujumla.

Mauaji haya ambayo yalianza baada ya Rais wa Rwanda, Juvenal Habyarimana na Rais wa Burundi, Cyprian Ntaryamira, kuuawa baada ya ndege yao kutunguliwa Aprili 6, 1994, yalidumu kwa kipindi cha siku 100.  Vikosi vya RPF, chini ya uongozi wa Jenerali Paul Kagame, ndivyo vilivyoyakomesha mauaji haya, baada ya dunia nzima kugeukia upande mwingine na kutochukua hatua zozote za kuyazuia, japo uwezo huo walikuwa nao.

Sina hakika kama waliona aibu baadaye, ila viongozi kadhaa wa dunia ambao walikuwa na uwezo wa kuyazuia mauaji hayo lakini hawakuyazuia, walimiminika Rwanda na kwenda kutoa “pole” kutokana na mambo yaliyowasibu jirani zetu hawa.  Wote walikuwa na kauli moja: “Never Again”, wakisisitiza kwamba haitatokea tena mauaji kama haya, kwani yaliweza kuzuiliwa na dunia haikuyazuia.

Wiki iliyopita, Rais wetu John Pombe Magufuli, ameongeza idadi ya viongozi ambao wametembelea Rwanda na kujumuika kutoa ile kauli ya “Never Again”.  Aliungana na Wanyarwanda wengine pamoja na Rais Paul Kagame kuadhimisha miaka 22 ya mauaji ya Kimbari yaliyotokea mwaka 1994.  Magufuli naye alisisitiza kwamba mauaji ya makusudi ya watu kutoka makundi mengine hayatakiwi kuruhusiwa kujirudia.

Ni kauli ambayo tumeshaisikia sana na ambayo ina maana nzito sana endapo itazingatiwa.  Kauli hii ukiachilia mbali wananchi wa Rwanda wenyewe kuisema mara kwa mara, imesemwa pia na viongozi wengine ndani na nje ya Bara la Afrika na tuliiamini kauli hii. Miaka 22 baadaye, najiuliza swali moja:  Kweli tumeishi kuitenda kauli hii?  Kweli tunazuia mauaji ya makundi yanayoweza kubadilika na kuonekana kama mauaji ya Kimbari?  Kweli tunazuia mauaji katika Bara letu la Afrika?

Nashangazwa sana na namna Waafrika wengi, hasa viongozi wetu, walivyo wepesi sana kusahau ahadi zao, na kusahau wajibu wao kwa jamii iliyowachagua.  Mauaji yaliyotokea Rwanda yalitikisa sana dunia kiasi kwamba kila aliyekuwa akikanyaga katika ardhi ya nchi ile, alisema “never again”.  Cha kushangaza ni kwamba ukipita muda mchache tu, yale yote yanasahaulika na hata kiongozi mwingine akionyesha dalili za kutaka kuleta machafuko, basi itafanyika kila mbinu alimradi ionekane tu kwamba hawawezi kuingilia masuala ya nchi nyingine.

Ndiyo; hapa ninaizungumzia Burundi.  Rais Pierre Nkurunziza alipoanza mambo ya ajabu ajabu huko Burundi, viongozi wake walinyamaza kimya.  Pengine walinyamaza kutokana na ukweli kwamba wao wenyewe wana matatizo lukuki katika nchi zao na hivyo kumnyooshea mwenzao kidole ingekuwa na ugumu mkubwa.

Nakumbuka kwamba ni kiongozi mmoja tu ndiye aliyepata ujasiri wa kusimama hadharani na kusema kwamba kinachoendelea Burundi kitasababisha mauaji ya kimbari na kwamba dunia haitakiwi kukubali hali hiyo itokee.  Kiongozi huyu alisisitiza kwamba watu wanatakiwa kujifunza kwa Rwanda, kwani kutokana na uroho tu wa madaraka, kundi moja la watu likaishia kuwaua kwa wingi kundi lingine na kuiacha nchi hiyo ikiwa imejaa mafuvu ya binadamu kwenye makumbusho yake.

Kiongozi huyo mwenye ujasiri ni Rais wa Rwanda, Paul Kagame.  Alisimama na alihoji.  Akahoji alipo Rais wa Burundi, akahoji walipo wengine ambao wangeweza kulisemea hilo, akahoji pia sababu za watu kuendelea kuuawa kwa sababu tu ya mtu mmoja anayedhani kwamba asipokuwa mtawala yeye, basi hakuna mwingine tena awezaye.

Ushupavu huu wa Rais Kagame katika kuhoji mambo kama hayo, ndio ushupavu ambao tulitaka kuona viongozi wetu wengine wakiwa nao.  Badala yake, viongozi wengine wako bize kujitafutia madaraka yao wenyewe na kushiriki kwenye chaguzi zsizo na mashiko, ili tu waitwe ‘mheshimiwa rais’.  Halafu wakitoka hapo na kubahatika kutembelea nchi kama Rwanda, wanatangaza “Never Again!”

Kusema kweli, sisi wananchi wa Bara la Afrika tumechoka.  Tumechoka kuwa na viongozi ambao hawawezi kuwakosoa wenzao hadharani wanapokosea.

Tumechoka kuwa na viongozi ambao mmoja akituhumiwa kwa kusababisha uhalifu wa kibinadamu, wengine wanamkingia kifua na kudai kwamba hata mahakama yenyewe inayomshitaki inawalenga Waafrika tu na hivyo wajitoe.  Wanawasahau mamilioni ya wananchi ambao wapo katika hali ngumu kutokana na huyo kiongozi mmoja wanayemlinda.

Tumechoka kuwa na viongozi ambao mwenzao akitakiwa kukamatwa na kupelekwa kujibu mashitaka kwa Kaizari, wao wanahusika kumtorosha kwa ndege na kumfikisha nyumbani kwake salama kabisa.  Wanasahau kwamba mtu huyo anatakiwa kuhukumiwa kwa matendo yake na kama hakuyatenda yanayosemwa, basi mahakama hiyo ndiyo itakayomsafisha.

Tumechoka kuwa na viongozi ambao wakipata upinzani wa kawaida tu nchini mwao, basi wanahakikisha kwamba yule anayesababisha upinzani huo anadhibitiwa vilivyo, ikiwamo hata kumzuia kutoka nyumbani kwake kwa zaidi ya mwezi.  Wanasahau kwamba nyuma ya mtu huyo wapo watu wengine wengi tu ambao hali hiyo inawasababishia wazidi kujenga chuki na kuzidi kuuimarisha upinzani wao.

Tumechoka kuwa na viongozi ambao wakipingwa kidogo tu na wale walio chini yao basi wanatangaza kuwafukuza kazi, hatua inayosababisha machafuko makubwa kati ya wanaowaunga mkono mahasimu hao wawili.  Wanasahau kabisa kwamba ugomvi wao ni mauti ya watu wao.  Hawalijali hilo, wanachokijali ni kila wanachokitaka wao, kwa maslahi yao binafsi na si kwa maslahi ya wale wanaowaamini.

Tumewachoka viongozi ambao utaalamu mkubwa walio nao si wa kuchaguliwa kwenye maboksi ya kura, bali wao wamebobea katika kupindua Serikali zilizowekwa kihalali madarakani.  Wakiona yamewashinda, wakiona vita inatokea, wakiona uhasama umezidi, basi wanabwaga manyanga na kukimbilia nchi ‘rafiki’ kwenda kujificha.  Wanasahau kabisa kwamba kiongozi lakini awajibike kutokana na matendo yake na badala yake wanachokijali ni uhai wao na wa watoto wao na si uhai wa wale wanaowapigania.

Inashangaza kwamba kwa viongozi wetu hawa, yaliyotokea Rwanda miaka 22 iliyopita wanayaona kama historia tu ya kufikirika na si kitu cha kujifunza kutokana nayo.  Ifike mahala hizi kauli za “Never Again” zionyeshe matunda.  Waanze kusutana wao kwa wao ili mwisho wa siku hata wakidai kwamba hayatatoka tena na sisi tuweze kuwaamini.

 

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles