24.2 C
Dar es Salaam
Friday, April 26, 2024

Contact us: [email protected]

NAMNA YA KUTAMBUA THAMANI ILIYOMO NDANI YAKO

 

Na Christian Bwaya,

UMEWAHI kujikuta kwenye mazingira ambayo hujui kwa hakika ufanye nini? Fikiria unataka kufanya uamuzi wa kazi gani inakufaa. Unatumia kigezo gani kufanya uamuzi?

Mara nyingi tunapokuwa kwenye mtanziko kama huu, tunakwenda kuomba ushauri kwa watu tunaowaamini. Wakati mwingine hatuombi ushauri moja kwa moja lakini tunachunguza kitu kinachokubalika na wengi.

 Hata hivyo, si mara zote kilicho maarufu kwenye macho ya jamii kinakufaa. Wakati mwingine hicho kinachokubaliwa na wengi, hakikupi furaha. Nikupe mifano kadhaa.

Umewahi kufanya kazi zenye heshima lakini hujisikii riziko ndani yako? Unapata kipato kizuri na watu wengine wanatamani kufanya unachokifanya lakini wewe mwenyewe hufurahii?

Unakuta umesoma vizuri lakini huoni thamani ya kile ulichokisoma. Zaidi ya kutaja chuo ulichosoma na idadi ya vyeti ulivyonavyo huoni namna gani elimu yako inakusaidia kutoa mchango kwa jamii.

Lakini pia inawezekana umejitahidi kupenda hicho ulichokisoma. Ni kawaida ukifanya kitu kwa muda fulani akili inaweza kukulazimisha kukipenda. Shida inakuwa ubunifu kazini. Unapofanya kitu ambacho si kusudi lako huwezi kuwa na ubunifu zaidi ya kukariri kile ulichofundishwa na mwalimu wako. Unakuwa kama umefungwa na nadharia.

Kwa hakika maisha hutuwekea mazingira ya kutulazimisha kufanya kisichotoka ndani. Tunajikuta tukifanya mambo yasiyoendana na kile kilichomo ndani yetu. Tunakuwa wepesi sana kusikiliza maoni ya watu wengine kuliko kujua kile kilichojificha ndani yetu.

Matokeo yake tunaishi maisha ya wengine. Tunawaiga wale tunaodhani wanaheshimika kwenye jamii. Tunafanya tunachofikiri watu wanakitarajia kwetu. Tunasoma kozi fulani kukidhi matakwa ya watu. Tunajikuta tunataka kufanya kazi zinazotarajiwa na jamii. Tunaishi makusudi ya watu wengine.

Tunasahau kuwa binadamu ni mtu wa pekee. Wewe unayesoma hapa ni mtu wa pekee. Mungu ameweka vitu vya pekee ndani yako. Unahitaji kuvijua ili vikuongoze kufanya maamuzi ya msingi katika maisha.

Tufanye nini kutambua vitu alivyoviweka Mungu ndani yetu? Kuna mambo mengi ya kuzingatia. Hapa naleta kwako maswali matatu unayohitaji kuyajibu.

Una vipaji gani?

Kila mtu ana vipaji vyake. Unaweza usikifahamu kipaji chako lakini hiyo haimaanishi huna. Tunapoongelea kipaji usifikiri vitu vikubwa ukachanganyikiwa.

Kipaji ni ule uwezo wa kufanya vitu kwa namna rahisi ambayo watu wengine hawawezi. Ni ule ujuzi unaokuwa nao bila hata kufundishwa sana.

Kwa mfano mwimbaji. Hahitaji kwenda kusomea ili ajue namna gani aimbe. Ni uwezo wa kuzaliwa nao. Akienda shule kujinoa zaidi inakuwa vizuri. Lakini elimu inakuwa kama inajazia kitu ambacho tayari anacho tayari. Asiye na kipaji anapokwenda kusomea kitu inakuwa kama kumfundisha sungura namna ya kupaa angani kama kunguru.

Tafakari vipaji alivyokupa Mungu. Pata nafasi ya kujikagua ndani yako. Una kipaji gani? Je, ni kuwashawishi watu? Kuchora? Mbunifu? Fundi? Mwandishi? Mwalimu? Biashara? Tambua kipaji chako.

Kitu gani kinakuvutia?

Pengine kujua kipaji inaweza kukuwia vigumu kwa sasa. Najua si kazi rahisi na wakati mwingine inahitaji muda. Lakini angalau kila mmoja wetu anaweza kujua kile anachopenda kukifanya. Nikikuuliza unavutiwa na nini kwenye maisha huwezi kupata shida.

Kila mtu ana vitu vinavyomvutia. Ndivyo hata wewe ulivyo. Kuna vitu vinakuvutia. Unapenda kuvifanya vitu fulani kwenye muda wako wa ziada. Mfano mimi hapa napenda kuandika. Nikiwa kwenye mapumziko napenda kuandika. Ndiyo furaha yangu kujieleza.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles